Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Amelifungua Jengo la Jipya la Abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar Terminal III.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kulifungua jengo jipya la Abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar  Terminal III  (kulia kwa Rais) Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyia Kazi zake Zanzibar Mhe. Xie Xiaowu na Waziri wa Ujenzi Usafirishaji na Mawasiliano Zanzibar Mhe. Dk. Sira Ubwa, hafla hiyo imefanyika katika jengo hilo


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa na miundombinu bora ya kisasa ya usafiri ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa ndani ya nchi kupitia vyanzo vya ndani na nje ya nchi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa jengo jipya la abiria na eneo la maegesho ya ndege katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (Terminal III), lililopo Kiembesamaki Unguja ambapo viongozi kadhaa walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia, ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi na viongozi wengine  na wananchi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa na kiwanja cha ndege kikubwa na cha kisasa ni kivutio kizuri kwa wageni wanaokuja hapa nchini kwa shughuli mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Alieleza kuwa katika sekta ya usafiri wa anga nchini, Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kuendeleza ubora wa miundombinu yake kama ambavyo inaonekana katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ambao kwa sasa una vituo (Terminals) vitatu.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa viwanja vya ndege ni injini za maendeleo ya kiuchumi duniani, kwa samabu ni vichocheo vya kukuza na kuimarisha utalii pamoja na uhusiano wa kibiashara kitaifa na kimataifa.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kwa kutilia maanani umuhimu huo wa viwanja vya ndege katika maendeleo ya nchi umefanya jitihada mbali mbali za kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.

Alisema kuwa wakati alipoingia madarakani mwaka 2010 aliahidi kuikamilisha kazi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Dk. Amani Abeid Karume.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo jipya la uwanja wa ndege huo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020 ibara ya 94 kifungu (a)  ambapo Serikali ya Mpinduzi ya Awamu ya Saba iliagizwa kutekeleza ujenzi huo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza mwezi wa Februari 2011 lakini licha ya changamoto mbali mbali za hapa na pale zilizojitokeza katika hatua za ujenzi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefarajika kwa kuzitatua changamoto hizo na kufikia mafanikio hayo ya kulizindua jengo hilo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa badala ya ile gharama ya Dola za Kimarekani 70.4 milioni kwa mkataba wa mwanzo, mradi huo mpaka kukamilika kwake umegharimu dola za Kimarekani 128.75 milioni.

Aliongeza kuwa Serikali ililazimika kuongeza mambo kadhaa ya marekebisho katika jengo pamoja na sehemu ya nje ya jengo hilo ili kuupa hadhi ya juu uwanja huo na uweze kuhudumia ndege za aina zote.

Alisema kuwa kutokana na haja hiyo Serikali ilibidi kusaini mikataba miwili ya nyongeza na kampuni ya BCEG wa kwanza ukiwa na fedha za nyongeza zenye thamani ya Dola za Kimarekani 11,828,674.71 na wa pili wenye thamani ya Dola za Kimarekani 46,518,414.8.

Alisema kuwa fedha hizo za nyongeza jumla ya Dola za Kimarekani milioni 58.35 zinalipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Bajeti yake ya ndani kwa ajili ya uendelezaji wa mradi huo na hadi sasa Serikali hiyo inaendelea vizuri katika malipo hayo.

Aliongeza kuwa hivi sasa uwanja huo wa ndege una uwezo wa kupokea ndege kubwa tatu aina ya “CODE E” kwa wakati mmoja ambapo pia, huduma zote ambazo zinastahiki kuwepi katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha kisasa tayari yapo.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Ujenzi ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya Jamhuri ya Watu wa China kwa moyo wao wa kindugu waliouonesha kwa kukubaliana na Serikali kuendelea na ujenzi huo kwa kukubali kusaini na Serikali mikataba hiyo ya nyongeza.

Aliupongeza uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Wakandarasi wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale waliotoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Wizara ya Fedha, Kilimo, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Kampuni ya Coastal Dredging inayomilikiwa na S.S. Bakhresa Group Companies na Meneja  wa Mradi huo Mhandisi Yassir De Costa. Pia, aliipongeza Kampuni ya ADPI ya Ufaransa ambayo ndiyo Mshauri Muelekezi katika ujenzi huo

Aidha, alieleza kuwa jengo hilo lenye viwango vya kisasa lina mifumo mbali mbali ya teknolojia inayokwenda na wakati ikiwemo mifumo ya kupokelea mizigo, mifumo ya kubaini ishara ya kuzuka kwa moto ambayo imejengewa ndani ya kituo hicho ambapo pia, ndege yoyote inaweza kutua na kupata huduma bila ya usumbufu pamoja na kuwepo kwa maduka yasiyotoza ushuru (Duty free shops).

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa jengo hilo litasaidia sana kuongeza abiria na mizigo kwa sababu lina uwezo wa kuchukua abiria milioni 1.6 kwa mwaka ambalo litapunguza msongamano wa abiria katika kituo cha Pili cha uwanja huo.

Rais Dk. Shein aliwashauri viongozi na watendaji wa kiwanja hicho kufahamu kwamba mwelekeo wa Serikali wa baadae uwe ni kuzikaribisha zaidi ndege kubwa ambazo zitakuwa zinachukua abiria wengi na kuingiza mapato.

Alitoa wito kwa wananchi hasa wae walio kwenye utumishi wa umma wanapopata nafasi ya kutembelea nchi za wenzao wajifunze yale mazuri ya manufaa ambayo wao bado hawajawanayo ili waje kuyaanzisha hapa nchini kwa kuongeza ubora kama alivyofanya Rais wa Mwanzo wa Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapindzi Marehemu Mzee Abeid  Karume.

Aliwasisitiza watendaji kuwa wazalendo, wajibikaji, ujuzi na wenye bidii katika kazi zao za kuendesha uwanja huo huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya wajibu wake katika jitihada za kwuapatia maendeleo wananchi wa Zanzibar hivyo kuna haja ya kuzienzi na kuzithamini jitihada hizo.

“Naamini kwamba kiwanja chetu cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume na kile cha Pemba vitaweza kufikia ubora kama ule wa “Heathrow” kilioko London Uingereza, au “Changi” kilioko Singapore na vinginevyo ambavyo ambavyo vinatajika kuwa viwanja bora na vyenye shughuli nyingi duniani.  

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaimarisha Dira mpya kwa wananchi kwa kupata ajira sambamba na kuongezeka kwa pato la  Taifa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa  alisema jengo hilo la aina yake litaongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini, sambamba na kuondoa manung’uniko kutoka kwa wageni juu ya ufinyu wa nafasi uliokuwa ukiukabili uwanja huo.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaimarisha soko la Utalii na hivyo kuwa sababu ya masoko mapya ya utalii kuongezeka kutokana na kuwepo kwa huduma hiyo muhimu.

Aidha, alisema Wizara ya Fedha na mipango itaendelea na jukumu la kutafuta fedha ili kutekeleza miradi mbali mbali inayobuniwa, akibainisha umakini wa Wizara hiyo, na kutolea mfano wa juhudi zilizofanyika ili kupata Dola Milioni 58.3 ikiwa ni ongezeko la gharama za ujenzi wa jengo hilo.  

Mapema Katibu Mkuu  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafiri Mustafa Aboud Jumbe Mwinyi alitoa historia ya usafiri wa ndege hapa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

Katibu Mkuu huyo pia, alieleza kuwa jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.6 kwa mwaka ambalo litamudu ongezeko la wageni hasa watalii ambao wamekadiriwa  na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kufikia 850,000 kwa mwaka kutoka idadi ya mwaka uliopita mnamo Disemba 2019 walikuwa 538,000.

Alieleza kuwa  Wizara yake hivi sasa inaendelea na ukamilishaji wa mambo madogo madogo yaliobakia ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya uendeshaji wa viwanja, ujenzi wa uzio wa kulihifadhi eneo hilo, uunganishaji wa njia ya kutoka eneo hio hadi njia kuu pamoja na kufanywa ukaguzi wa pamoja baina ya ICAO, IATA na Kampuni za ndege zitakazotumia jengo hilo ili kujiridhisha na kuanza kulitumia rasmi.

Aidha, alieleza namna ujenzi huo ulivyoonza ambapo saini ilitiwa mnamo mwaka 2010 huku Seriikali ikigundua mapugufu kadhaa mnamo mwaka 2012 ambapo hatua mbali mbali baada ya hapo zilichukuliwa.

Kwa malelezo ya Katibu Mkuu huyo jengo hilo lina ukubwa wa mita za mraba 25000,lina milango minne (Gates) ambazo kwa kitaalamu inaitwa Mikonga mikubwa na midogo ya kupitia abiria wanaoondoka au kuwasili ambacho pia kina barabara ya kurukia ndege yenye ukubwa wa mita za mraba 36,000.

Pia, kuna kumbi za abiria wa ngazi mbali mbali na kuna eneo la maegesho ya gari lenye ukubwa wa mita za mraba 8,818 ambalo linna uwezo wa kuegesha gari 214 kwa wakati mmoja.

Nae Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Xie Xiaowu alitoa pongezi kwa Serikali ya Ma;pinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais Dk. Shein kwa kukamilisha mradi huo na kuahidi kuwa Jamhuri ya Watu wa  China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.   

Sherehe hizo za ufunguzi wa jengo jipya la abiria na eneo la maegesho ya ndege katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (Terminal III), zilipambwa na ngoma pamoja na nyimbo mbali mbali za wasanii wakiongozwa na msanii maarufu wa bongo flava kutoka Dar es Salaam Aslay Isihaka Nassor maarufu Aslay.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.