Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wakishangilia katika Mkutano wa kampeni wa kuwanadi Wagombea wa Jimbo la Magomeni huko Uwanja waJitini ulioko Magomeni.
Na.Mwashungi Tahir Maelezo Zanzibar.
MWENYEKITI Mstaafu wa Mkoa wa Mjini Kichama Borafya Silima amewataka wanachama wa jimbo la Magomeni kuwachagua viongozi wanaofaa ili waweze kuleta maendeleo katika jimbo hilo.
Ameyasema hayo huko katika uwanja wa Jitini ulioko Jimbo la Magomeni wakati alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi akiwanadi wagombea wa Ubunge. Wawakilishi na Madiwani.
Amesema Chama cha Mapinduzi ni chama ambacho kina utaratibu wa mipango pamoja na maazimio mahsusi ya kufanya kazi zake za kuwaletea wananchi wake maendeleo kwa kutekeleza ilani .
“Chama cha Mapinduzi ni chama ambacho kinafuata utaratibu wa kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kutekeleza ilani”, alisema mwenyekiti huyo.
Aidha alisema wanachama wa chama hicho wanampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein katika awamu ya saba kwa kutekeleza vyema majukumu yake na kutimiza ahadi zake kwa kipindi cha miaka kumi.
Hivyo amewataka wananchi wa jimbo hilo kuwapa ridhaa wagombea hao ili waweze kuleta mabadiliko ikiwemo kuimarisha njia za ndani , kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana pamoja na kuwawezesha akinamama katika vikundi vya ujasiriamali na mambo mengine mengi ya maendeleo.
Pia amewaomba wanachama wa jimbo la Magomeni kutoa mashirikiano kwa viongozi kwani chama cha Mapinduzi kinapenda umoja na mshikamano ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Nae Mwenyekiti wa CCM Jimbo hilo Mahmoud Juma Ali amewaasa vijana kuepuka kushawishiwa na watu wasiotaka maendeleo na kuwa makini ili ifikapo tarehe 28 mwezi huu kushiriki kwenda kupiga kura kwa kuchagua chama cha Mapinduzi ili kiweze kuleta ushindi kwa kishindo.
Nao viongozi hao wakinadi sera zao wameahidi iwapo watapewa ridhaa na kuingia madarakani watahakikisha changamoto zinazowakabili wananchi katika jimbo hilo kwa kuhakikisha watasimama imara na kuwa mstari wa mbele katika kuzitatua ili jimbo hilo liweze kuimarika zaidi.
No comments:
Post a Comment