Habari za Punde

Uzinduzi wa Kitabu cha Kocha Bora Kilichoandikwa na Kocha Gullam Abdalla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwa na Kitabu cha Kocha Bora baada ya kukizindulia leo katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar na kulia kwake ni Mtunzi wa Kitabu hicho Kocha Gullam Abdalla hafla hiyo imefanyika leo 9/10/2020 Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua kitabu cha “Mwalimu bora wa  Soka’ na kusema kuwa kitabu hicho ni chuo kwa wachezaji wa mpira wa miguu pamoja na walimu wa mchezo huo ndani na nje ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Jijini Zanzibar, katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kitabu hicho kilichoandikwa na Kocha Gullam Abdalla Rashid, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali pamoja na wanamichezo wakiwemo wanasoka wakongwe wa Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein ambaye pia, aliwahi kuwa mwanamichezo maarufu hapa Zanzibar katika ujana wake alisema kuwa kitabu huandikwa ili kisomwe, hivyo ana amini kuwa kitabu hicho kitavutia idadi kubwa ya wasomaji kwa sababu mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini una mashabiki wengi.

Alisema kuwa mwandishi wa kitabu hicho hakukiandika kwa kubahatisha bali amekiandika kwa umahiri na weledi mkubwa kwa sababu yeye ni mwanasoka wa zamani sana tangu anasoma skuli ya msingi ya Gulioni hapa Zanzibar.

Alisema kuwa mtunzi wa kitabu hicho Kocha Gullam Abdalla Rashid amecheza mpira katika vilabu maarufu hadi timu ya Taifa ya Zanzibar na Taifa ya Tanzania ambapo mafanikio hayo ameyapata kutokana na heshima na nidhamu kubwa  katika soka.

“Ni mtu mwenye nidhamu sana, na hakuwahi kumpiga mtu kibuyu hata siku moja wakati akicheza mpira kwani alikuwa anacheza mpira kwa ustaarabu mkubwa”alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alimpongeza na kumshukuru Kocha Gullam kwa kumchagua yeye kuwa mwandishi wa dibaji ya kitabu chake hicho ambapo Dk. Shein alieleza kuwa kitabu hicho kitatoa mchango mkubwa katika kuendeleza  mpira wa miguu hapa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla kwa kuwahamasisha wapenzi wa mpira wa miguu ili wawe walimu bora.

Aliongeza kuwa fani ya michezo inahusisha mafunzo ya vitendo pamoja na taaluma ya nadharia na vitendo na nadharia vikiunganishwa pamoja vinaleta ufahamu unaokamilika, hivyo kitabu hicho kitampelekea msomaji anayekisoma na baadae akaingia kiwanjani kujua nini anachokifanya katika mpira wa miguu.

Hivyo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wanamichezo wote kukinunua kitabu hicho hasa ikizingatiwa kwamba kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwani hilo lina faida yake kwa mwanasoka au mshabiki wa soka wa hapa hapa nchini iwapo anajua kusoma na kwa vile anaamini wengi wao wanajua kusoma hivyo watafaidika kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa tayari Kocha Gullam ameshafungua milango kwa wenziwe wengine waweze kuandika zaidi na kusisitiza haja kwa wengine kuandika historia ya mchezo wa mpira wa miguu hapa Zanzibar, kuandika kuhusu wapenzi, mashabiki na mpezi bora wa mpira wa miguu.

Alieleza kuwa maarifa na ujuzi mkubwa katika michezo ni jambo muhimu sana kwa mchezaji kuwa nayo lakini hata hivyo ili kuyapata maarifa na ujuzi kunahitajika kuwepo miundombinu bora vikiwemo viwanja vya kujifunzia na kufanyia mazoezi na ndio maana Serikali anayoiongoza ikafanya juhudi ya kuhakikisha hilo linaimarika.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein pia, alisisitiza haja ya kuwaandaa vijana katika soka kwani nchi mbali mbali duniani zilizopata mafanikio zimeanza na utaratibu huo hivyo, ipo haja ya kuwaandaa vijana na ndio maana Serikali imeshaanzisha mchakato.

Alisisitiza kwamba suala la kuhifadhi miundombinu ya michezo ni jambo lililoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo, ni jambo la faraja kuona kwamba juhudi za kuhusisha tasnia ya michezo Zanzibar zimeleta mafanikio.

Dk. Shein pia alitumia fusra hiyo kukitaka chama cha mpira wa miguu  Zanzibar (ZFF), kubadilika hasa katika uongozi wake ili michezo iweze kufanikiwa hapa nchini.

Rais Dk. Shein alimsisitiza Kocha Gulam kuendelea kutunga vitabu vyengine na yeyote yule ambaye yuko tayari kutunga yeye atashirikiana nae kwani na yeye kwa upande wake ameshaanza kuandika mambo kadhaa kuhusu michezo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo uzalendo wa kuzibeza timu za nyumbani badala ya kuzifuatilia zaidi timu za Ulaya huku akieleza haja ya timu kuziita majina ya nyumbani.

Nae Waziri Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume alisema kuwa kitabu hicho kitakuwa nguzo muhimu kwa wale wote watakao taka kujifunza soka.

Aliongeza kuwa kitabu hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya mpira wa miguu hapa Zanzibar na kuweza kusaidia kusimamia soka.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Omar Hassan King kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kufanikiwa kuimarisha sekta ya michezo katika uongozi wake ndani ya miaka kumi.

Alieleza kuwa ndani ya miaka kumi ya uongozi wa Dk. Shein amefanya mambo mengi katika kuimarisha michezo ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya michezo hapa nchini kwa kuvijenga upya viwanja vya michezo na vyengine kuvifanyia ukarabati mkubwa kama vile kiwanja cha Mao tze Dong, Gombani na kiwanja cha Amani.

Pia, ameanzisha viwanja katika Wilaya za Zanzibar ambavyo vipo baadhi tayari vimeshaanza kutumika kama vile kiwanja cha Kitogani Wilaya ya Kusini Unguja, kiwanja cha Kishindeni Wilaya ya Micheweni na Kangani Wilaya ya Mkoani.

Alisema kuwa Zanzibar imeimarika kutokana na kuongezeka kwa michezo, kufufua FA Cup na kufufua vuguvugu michezo maskulini na kuanzisha Idara za micehzo na kuongeza wataalamu wa michezo huku akieleza kuwa kuwepo wka siku maalum ya mazoezi ya tarehe mosi Januari ya kila mwaka pia ni ubunifu wake Rais Dk. Shein.

Mapema akisoma Wasifu wa Mwandishi na Maelezo ya Kitabu hicho Mwalimu Suleiman Mamoud Jabir alisema kuwa Kocha Gulam ni mwanamichezo wa muda mrefu ambaye aliwahi kuwa mchezaji, mwalimu na hatimae kuwa kiongozi katika taasisi mbali mbali za michezo ndani na nje ya Zanzibar.

Alisema kuwa kitabu hicho alichokitunga kina Sura 11 ambazo kila Sura imeeleza mambo mbali mbali kuhusu mpira wa miguu, ukocha ama utaalamu, ufundishaji, mpango wa mazoezi na mafunzo katika msimu wa mchezo huo, umuhimu wa uzima wa mwili, ustadi na umakini katika soka pamoja na mambo mengineyo ya soka.

Nae Mtunzi wa Kitabu hicho Kocha Gulam  Abdalla Rashid alitoa pongezi na shukurani wka Rais Dk. Shein kwa kumuunga mkono katika utungaji wa kitabu chake hicho pamoja na kuwashukuru watu mbali mbali waliomsadia akiwemo Wazir Mahmoud Thabit Kombo na wanafamilia pamoja na wachezaji wenzake wa zamani hukua kisema kuwa utunzi wa kitabu hicho umechukua muda wa miaka 30.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.