Habari za Punde

Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Habari Lajionea Ujenzi wa SGR

Na Shamimu Nyaki -WHUSM, Morogoro.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wametembelea Mradi wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Morogoro - Dodoma ambapo wamefurahishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa kwa kasi.

 

Akizungumza kwa niaba ya baraza hiloNovemba 27, 2020 Mkuu wa msafara ambaye  ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Petro Lyatuu, amesema kwamba ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa kuwa wajumbe wa baraza wamejifunza kwa vitendo namna mradi unavyotekelezwa hatua kwa hatua.

 

"Tumekua na siku nzuri leo tumejifunza kwa kuona jinsi Serikali inavyotekeleza mradi huu, tumeona hatua iliyofikiwa katika ujenzi ikiwemo usimikwaji wa nguzo za umeme pamoja na utandikaji wa mataruma ya reli, naamini tutakua mabalozi wazuri katika kuelimisha na kushawishi wengine waje wajifunze na kuona kazi inayofanyika hapa" amesema Bw. Lyatuu.

 

Kwa upande wake Mhandisi Msaidizi wa Mradi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Christopher Mangwe'la amesema kuwa Mradi huo unatekelezwa kutoka Jijini Dar es Salaam  mpaka Mwanza ambapo kwa awamu ya kwanza mradi unatekelezwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na awamu ya pili unaanzia Morogoro hadi Dodoma ambapo mpaka sasa kipande cha kutoka Morogoro hadi Dodoma ujenzi umefikia asilimia takriban 48.

 

Mhandisi Mangw'ela ameongeza kuwa mradi huo una jumuisha vivuko takriban 110 pamoja na madaraja takriban 168.

 

"Reli hii itakua na uwezo wa kutembea kilometa takriban 160 kwa saa na ina mahandaki manne ambayo mawili kati ya hayo yana urefu wa mita zaidi ya 800" alisema Mhandisi Mangwe'la.

 

Vile vile, wajumbe hao walipata nafasi ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza Mataruma ambacho kipo Wilaya yaKilosa, Mkoani Morogoro.


Wakiwa kiwandani hapo, Mhandisi Salim Mustapha kutoka TRC aliwaeleza kuwa kiwanda hicho kwa siku kina uwezo wa kuzalisha mataruma 1,152 ambapo kwa muda wa mchana kinazalisha mataruma takriban 576.

 

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Jamii, Bi.Verity Rwakyendera kutoka Kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza mradi huo amesema kuwa mbali na kutekeleza mradi huo pia imekuwa ikisaidia jamii iliyopo karibu na mradi ambapo imefanikiwa kuchimba visima vya maji ambavyo vinatumiwa na wakazi wa maeneo yanayozunguka mradi.

 

Bi Verity ameongeza kuwa Kampuni hiyo pia imejenga matundu ya vyoo 20 katika shule ya msingi Kidete pamoja na zahanati katika Kijiji cha Gulwe.

 

Naye mjumbe wa baraza hilo, Bi.Flora Mwenyembegu amesema kuwa amefurahishwa na ziara ya kutembelea mradi huo wa kimkakati huku akisifu namna wataalam wazawa walivyopata nafasi katika kutekeleza mradi huo.

 

Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unasimamiwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRC) huku mkandarasi akiwa ni Kampuni ya Yapi Merkezi pamoja na Korea Railroad Corporation (Korail) na unatarajiwa kukamilika mwaka 2021 kwa gharama ya takriban Shilingi Trilioni saba.






 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.