Habari za Punde

MAJALIWA: UJENZI WA RELI YA SGR UMEBAKIZA KM. 61 KUTOKA MORO - DAR *Asema Serikali itatekeleza miradi yote iliyoianzisha

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) umebakiza km.61 tu za ukamilishaji kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam na kwamba ifikapo Desemba, 2020 mtu anaweza kusafiri kwa kiberenge kutoka Pugu hadi kituo cha Kwala, Morogoro.

“Mkurugenzi Mkuu ameniambia mpaka sasa mmeshatandika reli kwa umbali wa kilometa 144, kati ya kilometa 205 za kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Hii ni hatua kubwa sana.”

 

Alitoa kauli hiyo jana (Jumatano, Novemba 18, 2020) alipotembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha SGR kilichopo mkoani Morogoro. Ujenzi wa kipande Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 90 ukijumuisha maandalizi ya awali, uundaji wa ndani (survey), usanifu wa awali na wa kina na ujenzi pamoja na maandalizi ya majaribio.

 

Waziri Mkuu aliwahakikishia Watanzania kuwa miradi yote iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekelezwa ili ikamilike kwa wakati kama ilivyokuwa imepangwa.

 

Alisema Watanzania wana imani ya Serikali yao kwamba itasimamia miundombinu na miradi yote nchini ili iweze kukamilika baada ya kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji katika kipindi cha miaka mitano iliyoisha.

 

“Watanzania mmeridhia Serikali hii iendelee kwa kumpigia kura nyingi sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli, wabunge na madiwani, hii ina maana kwamba mlitaka Serikali na kazi zake ziendelee, tunachapa kazi, msiwe na mashaka, hawa wawakilishi wenu watakuja kusema mnataka nini na tutaleta.”

 

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo umeleta manufaa makubwa sana ikiwemo kutoa fursa za ajira na kuboresha uchumi wa nchi, na pindi utakapokamilika, utapunguza muda wa kusafiri barabarani kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kutoka saa tatu hadi saa moja na nusu.

 

Pia, alisisitiza kwamba hadi kufikia Aprili, 2021 treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakuwa imeshaanza kutoa huduma na kurahishisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo katika maeneo hayo.

 

Waziri Mkuu alisema kuwa huu ni wakati wa Watanzania kujipanga kufanya biashara ili kukuza uchumi wao kwa sababu kituo hicho kitakuwa kinahudumia watu zaidi ya 800 na kuegesha magari zaidi ya 150.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikagua kituo cha mizigo na karakana ya reli Kwala ambacho kitatumika kwa ajili ya kufanya ukarabati na kuunganishia treni ndefu za mizigo zinazofikia urefu wa kilomita mbili.

 

Waziri Mkuu alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa kwa kasi ni muendelezo wa maajabu yanayoendelea kutokea nchini kutokana na maono ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka kuibadilisha nchi na kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania.

 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa alisema katika eneo hilo kuna jumla ya majengo 16 yanayohusisha karakana za ukarabati wa mabehewa, vichwa vya treni, stoo, jengo la utawala, jengo la madereva, kantini pamoja na majengo mengine ya kanzidata, mifumo ya mawasiliano na mekaniki.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

S. L. P. 980,

41193 - DODOMA.

ALHAMISI, NOVEMBA 19, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.