Habari za Punde

kutotoa nafasi kwa Watendaji wenye tabia ya kukumbatia dhambi, ubadhirifu, uzembe.Mhe.Hemed

Na.Othman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais Mteule wa Zanzibar  Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah alisema Wananchi wa Zanzibari wanapaswa kujenga matumaini makubwa kwa Serikali Mpya itakayojizatiti kuwajibika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo.

Alisema uwajibikaji huo utakaozingatia kutotoa nafasi kwa Watendaji wenye tabia ya kukumbatia dhambi, ubadhirifu, uzembe pamoja na wizi ndio mfumo utakaotumiwa na Serikali chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah alitoa kauli hiyo akizungumza na  Wanahabari muda mfupi baada ya kula kiapo cha Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kufuatia Uteuzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na hapo hapo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid kulitamka jina lake lililowasilishwa na Rais wa Zanzibar mbele ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la kuteuliwa kwake kuwa Mtendaji Mkuu wa Serikali.

Alisema Viongozi, Watendaji wa Umma pamoja na Wananchi lazima waelewe kwamba kasi ya upatikanaji wa huduma muhimu za msingi za kustawisha Jamii na kukuwa kwa uchumi itategemea ushirikiano mkubwa utakaohusisha Serikali na Wananchi.

Mh. Hemed alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa kumuamini kumpa jukumu hilo zito ambalo amehaidi atalitekeleza kwa nguvu zake zote ili ile kiu ya Wazanzibari ya kuiona falsaha ya yajayo yanafurahisha iweze kufikiwa katika muda mfupi.

Makamu wa Pili wa Rais Mteule huyo wa Zanzibar aliwathibitishia Wananchi wote kwamba katika utekelezaji wake wa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Serikali hatakuwa tayari kuona Mtendaji aliyepewa dhamana ya kuwatumikia Wananchi anazembea katika nafasi yake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla kabla ya Uteuzi huo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.