Habari za Punde

Serikali kutafakari upya utoaji wa tenda kwa kampuni zitakazoshindwa kuheshimu mikataba

Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiangalia maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} Gombani Chake Chake Pemba na kuonya Mkandarasi asiyezingatia Muda wa Mkataba hatopewa tenda nyengine.
Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo la ZRB Pemba kutoka Kampuni ya Advent Construction Mhandisi Frenk Mohan akimpatia maelezo Mh. Hemed juu ya ujenzi wa Jengo hilo hapo Gombani
Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akionyeshwa Ramani ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya ZRB Gombani litakavyokuwa baada ya kukamilika Ujenzi wake.
Mh. Hemed akiwaagiza wakandarasi kukamilisha kazi zao kwa mujibu wa Mikataba wakati alipoyatembelea majengo ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} na Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Chake Chake Pemba
Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akilikagua jingo la Shirika la Utangazaji liliopo Mkanjuni Chake chake Pemba na kumuagiza Mkandarasi kukamilisha kazi kwa haraka ili kuwaondoshea usumbufu wanahabari wa Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiitembelea Bara bara ya Kijiji cha Kipapo na Mgelema ambayo tayari imeshakuwemo kwenye Mpango wa Wizara wa Ujenzi wa Kiwango cha Lami.

Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar wakimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed aliyepata fursa ya kuikagua Bara bara ya Kiji cha Kipapo hadi Mgelema.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa indhari ya  kutozipa Tenda  Kampuni au Taasisi zozote  iwe za Kibinafsi  na hata zile za Umma zinazopewa jukumu la Kusimamia Miundombinu ya Ujenzi  wa Miradi ya Maendeleo na zikashindwa kuheshimu  pamoja na kuzingatia muda wa utekelezaji wa Mikataba yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa  Hemed Suleiman Abdulla  alitoa indhari hiyo alipofanya ziara maalum ya kutembelea maendeleo ya Ujenzi wa Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} liliopo Gombani  sambamba na lile la Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} liliopo Mkanjuni Chake Chake Pemba.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema tabia ya baadhi ya Wahandisi wababaishaji wanaopenda kutafuta sababu zisizo na msingi wakati hushangiria kutia saini Mikataba ya Tenda wanazopewa kwa sasa hawatakuwa na nafasi tena.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiagiza Kampuni ya Frenk Mohan inayojenga Jengo la ZRB Gombani na Chuo cha Mafunzo kinachojenga Jengo la ZBC Mkanjuni kukamilisha majengo hayo ndani ya muda mfupi ujao, vyenginevyo Serikali haitakuwa na muda wa kuwapatia tena fursa kama hizo.

Alisema Wafanyakazi wa ZRB na ZBC wamekuwa na usumbufu wa Afisi za kufanyia Kazi ndani ya Kisiwa cha Pemba hali iliyopelekea Serikali kuridhia Ujenzi wa Majengo hayo na haitafurahia kuona Wahandisi waliopewa nafasi hiyo wanaendelea kutoa sababu zisizokubalika na Serikali.

“ Inasikitika kuona Jengo la ZRB lilipangiwa kukabidhiwa Serikalini Mwezi Disemba 2020 lakini bado halijafikia mazingira ya kukamilika na lile la ZBC tayari limeshapindukia Miezi Mitatu sasa”. Alisema Mh. Hemed Suleiman.

Alimuelekeza Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar aangalie Mikataba ya Ujenzi na pale itakapothibitika uzembe wa Mkandarasi kutotimiza wajibu wake atoe Taarifa Serikalini ili Kampuni hiyo ityolewe kabisa katika orodha ya Taasisi zinazopewa jukumu la kuendesha Miradi Visiwani Zanzibar.

Mapema Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza alisema Jengo hilo la Ghorofa Sita litakapokamilika litasaidia kuondosha  usumbufu wa nafasi za Kazi kwa Watendaji wa Taasisi hiyo inayosimamia Mapato ya Taifa.

Nd. Meza alisema mfumo wa Jengo hilo katika sehemu ya chini itazingatia kutoa huduma za Kibenki na Ghala, wakati ile ya pili na Nne zitatumiwa na Wafanyakazi wakati ghorofa ya Tano na sita zitatoa huduma kwa Viongozi na Wajumbe wa Bodi ya Mapato Zanzibar.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa Jengo kubwa la Kisasa umekuja kutokana na mabadilikon ya utendaji wa Shirika hilo.

Mkurugenzi Chande alisema Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na Studio Mbili zitakazokidhi mahitaji ya kutangazia pamoja na vipindi kwa vile Studio mpya itajengewa mazingira ya kutoa matangazo ya moja kwa moja kutegemea matukio yatakayojiri.

Alisema Studio hizo zitakwenda sambamba na Ofisi za Wafanyakazi huku Wahandisi wakazingatia Wananchi wenye mahitaji maalum watakaofika studio hizo kupata huduma za mawasiliano, matangazo na huduma nyengine.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuanza mara Moja Ujenzi wa Bara bara ya Kipapo hadi Mgelema ili kutekeleza agizo la Serikali ililolitoa la kutaka kazi hiyo ianze mara baada ya kumalizika kwa Bara bara ya Ole Kengeja.

Akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Mgelema baada ya kuikagua bara bara hiyo Mh. Hemed ametoa muda usiozidi  saa 12 kuanzia sasa kukutana na Uongozi wa Bodi ya Mfuko wa Bara bara kwenye Makaazi yake Pagali Chake Chake Pemba ili kulijadili suala la Bara bara hiyo iliyokuwa kero kubwa kwa Wananchi wa Maeneo hayo.

Alisema Bara bara ya Kipapo hadi Mgelema bado ninastahiki ijengwe ili kuwaondoshea shida Wananchi waliojenga matumaini makubwa kwa Serikali kutokana na ahadi na Mikakati yake ya kuwatumikia wakati wote.

Alifahamisha kwamba inatia huruma kuona Wananchi wa Vijiji hivyo hasa Kina Mama Wajawazito wanafikia hatua ya kujifungua Majumbani kwa kukosa usafiri wa kuwapeleka kwenye Vituo vya Afya pamoja na Hospitali jambo ambalo ni hatari kwa Maisha.

Mapema Mhandisi wa Ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasliano na Usafirishaji Mhandisi Khamis Masoud alisema Ujenzi wa Bara bara hiyo tayari umeshaingizwa ndani ya Mpango wa Wizara kwa ajili ya Ujenzi wa Kiwango cha Lami.

Mhandisi Khamis alisema Wizara inayosimamia Mawasiliano ya Bara bara imeshajipanga kutumia shilingi Milioni Mia 500,000,000/-  kwa ajili ya hatua za Ujenzi wake huku Mfuko wa Bara bara ukitenga shilingi Miklioni 200,000,000/- ili zitumike kwa hatua ya awali ya bara bara hiyo kupitika hata kipindi cha mvua.

Alisema ujenzi wa Bara bara hiyo kwa kiwango cha Lami hadi kukamilika kwake utahitaji jumla ya  shilingi Bilioni Mbili Nukta Mbili.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.