Habari za Punde

TANTRADE IMEPANIA KUENDELEZA VIWANDA MKOANI TANGA

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

SERIKALI Mkoani Tanga imedhamiria kufufua na kuanzisha viwanda vipya kwa lengo la kukamilisha dhana ya nchi ya viwanda ikiwa ni pamoja na kuwapatia wananchi ajira.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Matin Shigella aliyasema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya kufungua kikao cha wamiliki na wazalishaji wa sekta ya viwanda Mkoani hapa kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Shigella alisema kuwa wanaendelea kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye viwanda vilivyokufa Mkoani Tanga ili kuendana na Tanzania ya viwanda lakini pia aliongeza kuwa wana mpango pia wa kuanzisha viwanda vipya ili kuwapatia wananchi ajira kwa wingi.
"Tuna kiwanda cha chuma, mbao pia tuna kiwanda cha Mkumbara kule Korogwe na cha chai kule Lushoto ambavyo vyote viko chini ya serikali na bahati nzuri kuna wawekezaji walioonyesha nia, lakini sio tu kufufua viwanda vya zamani, tuna mpango wa kuanzisha viwanda vipya ili kutoa ajira na kuendana na tekinolojia ya kisasa" alisema.
Aidha aliishukuru TANTRADE kwa kuwaletea wadau wa biashara mkoani hapa kwani itawasaidia kueleza na kupatiwa ufumbuzi wa changamoto zao na kuwapa fursa ya kushiriki katika maonyesho ya tano ya viwanda yanyotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

"Niwashukuru sana TANTRADE kwa kutuletea warsha hii katika mkoa wetu wa Tanga kwani Tanga ni viwanda na viwanda ni Tanga lakini poa tutaweza kupata fursa ya kushiriki maonyesha mwezi desemba mwaka huu na hii inatupa fursa pia kwa wamiliki wa viwanda na mkoa kwa ujumla kwakuwa unapoongeza uzalishaji, utaongeza vitendea kazi pamoja na wafanyakazi" alieleza.

Naye naibu mkurugenzi mkuu wa TANTRADE Latifa Khamis alieleza kwamba lengo la mamlaka ni kusikiliza na kutatua changamoto za wenye viwanda mkoani hapa ili viwanda viweze kukua na kuendelea kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

"Kama tunavyofahamu Tanga ina viwanda ambavyo vilikuwa vikizalisha na bidhaa zake kuuzwa mpaka kwenye soko la Afrika mashariki, hivyo tumeamua kuja kusikiliza changamoto zao ili tuzitatue tunataka kuona viwanda mkoani Tanga vinakua na kuendelea" alisema.

Khamis alisema kuwa watashirikiana kwa ukaribu na mkoa kuhakikisha wanatimiza agizo la Rais la kutekeleza kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda lakini pia aliongeza kuwa watashirikiana kuandaa maonyesho makubwa ya viwanda ya kitaifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.