Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed aridhishwa na utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf}

Mratibu wa Tasaf  Unguja Nd. Makame Ali Haji akitoa Taarifa fupi ya utekelezaji wa Tasaf Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alipofanya ziara Makao Makuu ya Tasaf  Mazizini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiutembelea   Mradi wa upandaji Miti na mboga mboga la Wananchi wa Kijiji cha Kitogani waliopata msukumo kupitia Mradi wa Tasaf.
Mheshimiwa Hemed Suleiman akiridhika na matokeo ya Mradi wa Shamba Darasa la Wana Kaya wa Kijiji cha Kizimkazi Dimbani  unaotekelezwa kupitia Mfuko wa Tasaf.
Muonekano wa Bwawa la Kufugia pamoja na umwagiliaji la Wananchi wa Kijiji cha Mtende kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf}
Wananchi wa Kijiji cha Mtende wakielezea changamoto zinazowakabili Kijiji pao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla ikiwa ni pamoja na Migogoro ya Ardhi inayowasumbua kutekeleza Miradi yao ya Maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akielezea kuridhika kwake na Tasaf jinsi ilivyowaunganisha Watanzania kuwa wamoja bila ya kujali itikadi zao alipozungumza na Wananchi wanaotekeleza Miradi ya Tasaf  iliyomo Mkoa Kusini Unguja.

Picha na – OMPR – ZNZ


Na Othman Khamis OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema anaendelea kupata moyo kuona Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} umekuwa daraja la kuwaunganisha Wananchi katika harakati zao za kimaisha bila ya kujali tofauti za Kidini, Kisiasa au maeneo wanayotoka.

Alisema miradi tofauti ya Kijamii inayotekelezwa na Wananchi ndani ya mfumo wa Umoja na Mshikamano kupitia Mfuko wa Tasaf katika maeneo tofauti Tanzania Bara na Zanzibar, Mijini na Vijijini imeleta faraja na kupunguza ukali wa maisha hasa kwa Wananchi wa Kaya Maskini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alitoa faraja hiyo wakati alipofanya ziara maalum ya kukagua Miradi ya Wananchi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Tasaf  ya shamba la Upandaji wa Miti na mboga mboga la Kitogani, Shamba darasa la Wanakaya wa Kijiji cha Kizimkazi Dimbani pamoja na Mradi wa  Bwawa la Ufugaji pamoja na umwagiliaji la Wakaazi wa Kijiji cha Mtende.

Alisema hamasa ya Wananchi bila ya kujali tofauti zao imeleta faraja kubwa kwa Serikali Kuu iliyojitolea kwa nguvu zake kuendelea kushirikiana na Wananchi hao katika kuona kero na changamoto zinazowakabili zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu na kuleta tija.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kutokana na kasi kubwa ya maendeleo inayoshamiri maeneo tofauti Nchini Viongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya wanapaswa kutafakari njia za kuzingatia upatikanaji wa soko la ushindani kwa bidhaa zinazozalishwa na Wananchi katika maeneo yao.

Alisema tafakari hizo ni vyema zikaenda sambamba na Halmashauri za Wilaya  kuhamasisha kuanzisha Ulinzi Shirikishi utakaosaidia kulinda Miradi ya Wananchi hasa Akinamama ambayo inapaswa kuheshimika ili kutowavunja moyo kutokana na juhudi pamoja na hamasa walizonazo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alivitaka Vyombo vya Ulinzi kwa kushirikiana na Vikundi Shirikishi kujiepusha na uzoroteshaji wa Kesi za wahujumu wa Miradi ya Jamii kwa vile wahalifu si Watu wanaopaswa kufumbiwa macho.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewahakikishia Wananchi hao kwamba Serikali Kuu kupitia Mikoa, Wilaya na hata Shehia kwamba itaendelea kutafuta njia muwafaka itakayokidhi mahitaji ya Wananchi hao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakwaza.

Akizungumzia shamba Darasa la Matunda, Mboga Mboga na vyakula vya nafaka liliopo Kizimkazi Dimbani Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Wanachama wa Kikundi hicho ni vyema wakaitumia vyema elimu waliyoipata ili izidi kunufaisha maeneo mbali mbali.

Alisema licha ya eneo lao dogo la Darasa lakini utaalamu wanaoupata unaweza kuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa Miradi ya ujasiriamali Kitaalamu kwenye vikundi vingi vya Ushirika ndani ya Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja kwa ujumla.

Kuhusu migogoro ya Ardhi ya Wananchi wa  Kijiji cha Mtende Mheshimiwa Hemed aliwaeleza Wananchi hao kwamba atamuagiza Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Jimbo lao watenge muda muwafaka utakaotoa fursa kwao kujadili masuala hayo.

Alisema Serikali itatoa maamuzi sahihi baada ya ripoti ya majadiliano hayo na yale masuala yaliyopelekwa Mahakamani  watalazimika kuwa na subra kwa ajili ya  kuipa haki Mahakama kutoa maamuzi sahihi yasiyopendelea upande wowote.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana na Uongozi pamoja na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Kanda ya Unguja hapo Mazizini ambapo alisema Zanzibar lazima iendelee kubakia kuwa mfano bora wa utekelezaji wa Miradi ya Tasaf katika Nyanja ya  Kimataifa.

“ Nategemea kipindi hichi cha Pili katika Tasaf ya Awamu ya Tatu kitakuwa mfano mzuri mno”. Alifahamisha Mtendaji Mkuu huyo wa Shughuli za Serikali akiwa pia Msimamizi Mkuu wa Tasaf Zanzibar.

Alisema kwa vile Watendaji hao wamepewa jukumu la kuwahudumia Wananchi  wanyonge hawanabudi kuendelea kuwa waaminifu  kama walivyofanya katika Tasaf Awamu za vipindi vilivyotangulia.

“ Wananchi lazima waendelee kuwezeshwa  kwa vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} ni muhimu kwa kubadilisha maisha yao”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatiwa matumizi bora ya Fedha  za Serikali Mfuko wa Tasaf ikiwa miongoni mwake kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi anavyotilia mkazo jambo hilo hata kama itakuwa shilingi Moja wakati ni ya Serikali iendelee kuheshimiwa.

Akitoa Taarifa fupi Mratibu wa Tasaf  Unguja Nd. Makame Ali Haji alisema Utekelezaji wa Tasaf Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili tayari imeshaanza kwa hatua ya uhakiki wa Wanakaya Wapya watakaoingizwa kwenye Mradi huo.

Nd. Makame alisema jumla ya Kaya 34,962 zimeandikishwa katika zoezi la awali ikiwa ni sawa na asilimia 85% na limepangwa kukamilika rasmi ifikapo Mwezi Januari Mwaka ujao unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa Wiki hii.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.