Habari za Punde

Mbunge wa jimbo la Tunguu afanya ziara Ubago kusikiliza kero za wananchi

 Bahati Habibu   Maelezo    Zanzibar       29/12/2020.

Wananchi wa Shehia ya Ubago Wilaya ya Kati  wameuomba Uongozi wa Jimbo la Tunguu kukaa na Serikali ili kuweza kulipatia ufumbuzi tatizo la mgogoro wa mipaka baina ya Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Wananchi wa Shehia hiyo.

Wamesema wanasikitishwa na vitendo vinavyofanywa na Kambi ya Jeshi ya ubago kwa kuweka mipaka yao katika Mashamba ya Watu na Makaazi ya wanakijiji hao jambo ambalo linasababisha Migogoro na Wananchi.

Wameyasema huko katika Tawi la CCM Ubago wakati Mbunge wa Jimbo la Tunguu Mh. Khalifa Salum Suleiman alipofanya ziara ya kutoa shukurani baada ya kuchaguliwa na kuzisikiliza kero  zao.

Amesema Viongozi wa Kambi hiyo wamevunja nyumba za familia nne na kuziacha bila makaazi jambo linalosababisha  kuishi maisha ya kubahatisha na kurudisha nyuma maendeleo yao.

 

‘’Tumevunjiwa nyumba zetu,tukapelekwa katika nyumba za Vijiji lakini baadae tumehamishwa na muda huu hatujuwi pa kuishi na Watoto wetu kwa hiyo tunaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itusaidie tumechoka’’walisema Wanakijiji hao.

Hata hivyo wamesema tayari wameshapeleka malalamiko yao  katika Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja ili kutafuta  suluhu ya mgogoro huo lakini hadi leo haujapatiwa ufumbuzi.

Nae Mbunge wa Jimbo la Tunguu Mh. Khalifa Salum Suleiman ameahidi kuishauri Serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro huo ili kuondosha usumbufu wanaoupata Wananchi hao.

 

Mbali na hayo amewataka Wananchi kushirikiana na Viongozi wao wa Jimbo katika kuzitafutia ufumbuzi Changamoto zinazowakabili ikiwemo Maji, Barabara na Umeme na kuahidi kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

 

Mbunge wa Jimbo la Tunguu amefanya ziara katika Kijiji cha Mwerakiongoni na Ubago na kukabidhi Mipira ya Maji na mifuko ya saruji ambapo vitu vyote vimegharimu sh.milioni moja na laki 3.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.