Habari za Punde

Mwakilishi wa jimbo la Tunguu kushirikiana na wanachama katika kuitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo

 Na Maulid Yussuf  - WEMA

Mkoa wa Kusini Unguja.

Mwakilishi wa jimbo la Tunguu kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi, Mhe Simai Mohammed Said amesema  ataendelea kushirikiana na wanachama wa chama hicho katika kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi kwa vitendo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupongezwa na viongozi wa jimbo la Tunguu ilioandaliwa na wanachama wa jimbo hilo  katika ukumbi wa kijeshi Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, amesema  mashirikiano ndio njia pekee katika kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Amesema awamu ya nane ni awamu yenye mabadiliko katika kila sekta hivyo akiwa mwenye dhamana ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  amewaahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa kutekeleza majukumu aliyopangiwa ili kuleta heshima kwa jimbo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM jimbo la Tunguu bwana Khatibu Ramadhani  amesema jimbo la Tunguu limesimama kidete kuhakikisha jimbo hilo linabaki kuwa ni la chama cha Mapinduzi pamoja na kuhakikisha CCM inashinda.

Aidha amewataka viongozi na wanachama wa CCM kufanya kazi ya kujitolea ndani ya chama Chao na kutokubali kubabaishwa pamoja na kuhakikisha wanaendelea kuwahamasisha vijana wao ili kuondosha kabisa upinzani ndani ya jimbo lao na Zanzibar kwa ujumla.
 
Nae katibu wa CCM jimbo la Tunguu bi Sharifa Maabadi  amempongeza Mwakilishi wa jimbo hilo kwa kuwaweka pamoja wajumbe na wanachama wote wa CCM wa  jimbo  la Tunguu kwani wanaamini ukaribu huo ni ishara ya kushirikiana katika  kuleta maendeleo  ya uchumi wa bluu nchini.

Aidha wamemuomba Mwakilishi huyo  wa jimbo hilo kua karibu na Wanachama wake kwani wana imani nae kutokana na dhamana ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, hivyo wamemtaka kuifanyia kazi kwa bidii nafasi hiyo.

Katika hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha mchana, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.