Habari za Punde

Wachunaji wa Ngozi Watakiwa Kuwa na Leseni.Na Mbaraka Kambona, Singida

Wataalamu wa Mifugo wanaosimamia machinjio nchini wametakiwa kuhakikisha wachunaji wa Ngozi za Wanyama wawe ni wale waliopata mafunzo na wamepewa Leseni ya uchunaji ili ngozi inayochunwa iwe na ubora utakaofaa kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Stanford Ndibalema alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutekeleza mikakati ya sekta ya mifugo kuendana na Ilani ya Chama Tawala kinachofanyika Mkoani Singida Disemba 16-17, 2020.

Dkt. Ndibalema alisema kuwa ubora wa ngozi unaanzia shambani, hivyo wajibu wa kwanza ni wa Mfugaji mwenyewe kuhakikisha wanyama wanapatiwa matunzo mazuri ikiwemo chakula, chanjo na kuogeshwa kwa wakati ili kuwakinga na magonjwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndibalema, Serikali imeshatunga Sheria na kanuni ambayo inawataka wachunaji wa ngozi wawe ni watu wanaotambulika na wamepewa leseni ya uchunaji ili kazi ya uchunaji iwe rasmi na ifanywe kwa weledi ili kupata ngozi bora na yenye thamani sokoni.

“Sehemu kubwa ya machinjio nchini zinamilikiwa na Serikali za Mitaa, hivyo niwaombe viongozi wa serikali za mitaa na hasa Wataalamu wanaosimamia machinjio kuhakikisha wale wanaojishughulisha na uchunaji wa ngozi wawe wamepata mafunzo na wamepewa leseni ya uchunaji, tunaamini hayo yote yakizingatiwa ngozi hazitaharibiwa wakati wa uchunaji na hivyo tutapata ngozi bora itakayokuwa na thamani sokoni,” alisema Dkt. Ndibalema

Naye, Afisa Mifugo kutoka Mara, Denis Ishengoma alisema kuwa ili afya ya Wanyama iwe bora na kutoa mazao mazuri ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wachunaji wa ngozi na Halmashauri itenge bajeti ya kuboresha afya za mifugo.

“Ngozi zinazalishwa lakini nyingi hazina ubora na thamani ya kuuzika sokoni, hivyo naiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inasimamia eneo hili vyema ili mazao ya ngozi yawe na ubora na yatafutiwe masoko ndani na nje ya nchi,” alisema Ishengoma

Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo kutoka Mkoani Morogoro, Gasper Msimbe alisema kuwa sheria ya utambuzi wa mifugo na ufuatiliaji Namba. 12 ya Mwaka 2010 imeelekeza eneo la kuweka alama kwa mnyama hivyo Halmashauri zielimishe wafugaji wasiweke alama katika maeneo ambayo yataharibu thamani ya ngozi.

“Ili kuhakikisha hawa wafugaji wanatii, tunaiomba Wizara iweke kanuni kwamba mifugo iliyowekwa alama inayopunguza thamani ya ngozi isipelekwe kuuzwa mnadani, hii itakuwa njia moja wapo ya kudhibiti uwekaji wa alama katika maeneo ambayo yanaharibu thamani ya ngozi,” alisema Dkt. Msimbe

Aidha, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo, Kanda ya Kusini Magharibi, Rukwa, Dkt. Kaini Kamwela alisema kuwa wakati umefika sasa kama nchi kuwa na mkakati mzuri wa kibiashara wa zao la ngozi utakaoweza kuainisha mambo mbalimbali yatakayowezesha ngozi kuuzwa nje ya nchi.

Awali akifungua Kikao kazi hicho cha siku mbili, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Deogratius Yinze aliwataka wataalamu hao wa mifugo kuhakikisha wanaendelea kutoa utaalamu wao ili kuendeleza sekta ya mifugo iweze kuleta tija katika uzalishaji na kuchangia vyema katika uchumi na pato la taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.