Habari za Punde

Wakuu wa Mikoa Watakiwa Kuandaa Utaratibu Maalum Kusikiliza Kero na Kuzitafutia Ufumbuzi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kumaliza kuwaapisha Wakuu wa Mikoa wa Zanzibar katika hafla iliofanyika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3/12/2020

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wakuu wa Mikoa wapya wa Zanzibar kuwa na utaratibu maalum unaotambulika wa  kusikiliza kero za wananchi  pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

Dk. Mwinyi ametoa ushauri huo leo Ikulu jijini Zanzibar katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa wapya, watakaohudumu katika Mikoa mitano ya Zanzibar.

Walioapishwa ni  Ayoub Mohamed Mahamoud Mkoa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid (Kusini Unguja), Idrissa Kitwana Mustafa (Mjini Magharibi), Salama Mbarouk Khatib (Kaskazini Pemba) pamoja na Mattar Zahor Masoud , mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema viongozi hao wana jukumu la kuandaa utaratibu maalum utaowawezesha wananchi kuwasilisha kero mbali mbali zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka, huku akiwataka kutokuwa sehemu ya kero hizo kwa kigezo kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaojihusisha katika migogoro mbali mbali ikiwemo ya ardhi.

Aidha, aliwataka viongozi hao kuondokana na utamaduni wa kuoneana aibu au muhali,  pamoja na kuwataka kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo iliomo Mikoani mwao  hata kama miradi hiyo inatekelezwa na Wizara za Serikali.

“Mradi wowote unaofanyika katika Mkoa wako ni mradi wako una jukumu la kufuatilia hata kama unatekelezwa na Wizara……”, alisema.

Alisema viongozi hao wana jukumu la kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na kumalizika kwa wakati, akibainisha kuwepo miradi kadhaa ikiwemo wa ZUSP  (unaogharimu US Dolla Milioni 93) ambao utekelezaji wake hauridhishi kwa msingi kuwa  umetekelezwa chini ya viwango katika maeneo mbali mbali.

Dk. Mwinyi aliwataka Wakuu hao wa  Mikoa kujiridhisha iwapo miradi inayotekelezwa katika Mikoa yao inaendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Sambamba na hayo, aliwataka viongozi hao kuzifuatilia kwa karibu Manispaa na Halmashauri zilizomo Mikoani mwao kutokana na utendaji wa kazi usioridhisha, kiasi cha kushindwa hata kukusanya taka pamoja na kusimamia makusanyo ya fedha.

Aidha, alisema pamoja na kuwepo miradi ya Wizara katika Mikoa yao, wana jukumu la kubuni miradi mipya  ili kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na kumtaka kila mmoja kuwa sehemu ya utekelezaji kwa vitendo ahadi alizozitowa kwa wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi mkuu uliopita.

Akigusia suala la Uwajibikaji kwa watendaji, Rais Dk. Mwinyi aliwakumbusha viongozi hao wajibu walionao katika kuwasimamia wafanyakazi wao ili kila mmoja aweze kutekeleza wajibu wake na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi,  akibainisha kuwepo dhuluma,manyanyaso na udhalilishaji kwa wananchi.

Vile vile alitaka kuwepo mifumo bora ya ukusanyaji mapato ili yaweze kutatua matatizo mbali mbali katika sehemu zinazohusika, sambamba na kuwataka kuwa wabunifu, kuondokana na urasimu na kusisitiza umuhimu wa kusimamia vyema dhamana zao katika taasisi zote za ukusanyaji  mapato.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliwataka viongozi hao kupiga vita rushwa na kuondoa ubadhirifu katika matumizi ya mali za serikali, sambamba na kuondoa wizi katika maeneo mbalimbali , huku akisema makusanyo na fedha za Bajeti zimekuwa zikipotea sana.

Aidha, alisema kuna changamoto kubwa katika suala la utiaji saini mikataba ya miradi mbali mbali nchini, ikiwemo ile ya Wizara za Serikali,  ambapo Wizara ya Fedha imekuwa ikihodhi jukumu hilo.

Alisema hakuna ulazima kwa Wizara hiyo kuingia  mkataba katika kila Mradi wa Wizara, akibainisha hatua hiyo inaviza utendaji kutokana na ufuatiliaji duni, akitolea mfano wa mradi wa mashine ya MRI katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja iliyoshindwa kutengenezwa kwa wakati kwa vile mkataba wake ulisainiwa na  Wizara ya Fedha.

“Inatia mashaka kila mradi mkataba wake lazima uingizwe na Wizara Fedha” alisema.

Akiahidi kufuatilia utendaji wa  Wakuu hao wa Mikoa hao, Dk. Mwinyi aliwataka kufanyakazi kwa utaratibu mpya wa ubunifu na  utatuzi wa kero za wanachi ili kila senti ya serikali iweze kutumika vizuri. 

Mapema, Dk. Mwinyi aliwakumnbusha viongozi hao  jukumu linakowakabili katika kusimamia Mikoa kuwa sio jambo dogo, hivyo akawataka kutekeleza wajibu huo kwa kujituma ili kutekeleza vyema Ilani ya CCM pamoja na kuondoa kero mbali mbali za wananchi.

Aidha, aliwashauri wasichelewe kujifunza majukumu yao na kufanyakazi zinazowakabili, akitaka kuweka kipaumbele  suala la ulinzi na Usalama kwa mashirikiano  na vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Aliwataka kusimamia kikamilifu Manispaa na Hamashauri zilioko Mikoani mwao, akibainisha kuwepo mapungufu makubwa katika usimamizi.

Nao, Wakuu wa Mikoa mitano ya Zanzibar, walisema wameajianda kutekeleza kikamilifu majukumu yote ya kazi zao, ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Viongozi mbali mbali wa kitaifa walihudhuria katioka hafla hiyo, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu  Mkuu Kiongozi Dk. Abdulahamid Yahya Mzee, Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk.Mwinyi Talib Haji, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid ,Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab,  Viongozi wa Idara maalum za Serikali ya Zanzibar pamoja  wana familia.

 Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.