Habari za Punde

Kuelekea Michuano ya CHAN, Ulega awataka Watanzania kuunga Mkono Taifa Stars

Na Beatrice Sanga, MAELEZO.Dar.Januari 4, 2021.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega, amewataka watanzania kuunga mkono  Timu ya Tanzania (Taifa Stars) ili iweze kufanya vizuri katika fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, yanayohusisha wachezaji wa ndani (CHAN) yanayotarajia kufanyika Januari 16 hadi Februari 7 mwaka huu nchini Cameroon.

Katika Michuano hiyo, Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepangwa Kundi D pamoja na Zambia, Guinea na Namibia.

Akizungumza katika viwanja vya Gymkana Jijini Dar es Salaam alipotembelea kushuhudia mazoezi ya timu hiyo iliyo katika maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), ikiwa ni sehemu ya maandilizi ya michuano ya CHAN itakayofanyika Cameroon Ulega amesema ipo haja kwa watanzania kuunga mkono timu hiyo.

“Niwaombe watanzania wote tuunge mkono timu yetu ya Taifa, wachezaji wanayo ari kubwa sana ya kufanya vizuri” ,Amesema Ulega.

Hata hivyo, Ulega amesisitiza nidhamu na hali ya kujituma kwa wachezaji zaidi ya wanavyofanya katika vilabu vyao hali itakayowezesha kufanya vizuri katika mchezo unaofuata, na kupelekea timu   kupata ushindi na hatimaye kuweza kuiwakilisha vizuri Tanzania.

“Tunataka wachezaji wajitume zaidi ya wanavyojituma katika vilabu vyao, kwanza wao katika watanzania milion 60 wao ndo wale 30 wachache wanaotuwakilisha wote, kwa hiyo hilo ni njambo lisilokuwa la kawaida, watakapocheza kwa jitihada watapata nafasi ya kujiuza wao wenyewe.” Amesema  Ulega.

Amesema Serikali itahakikisha vijana wengi wanapata fursa ya kwenda kucheza nje ya nchi ili kuleta mabadiliko ya michezo hasa wa mpira wa miguu, na kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitano ijayo soka linakuwa kwa kiwango cha hali ya juu zaidi.

Ulega ameongeza kuwa serikali  kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo inaendelea kufuatilia kwa karibu timu ya taifa na kuwa karibu na viongozi wa timu hiyo ili kuhakikisha inapata ushindi na inafanya vizuri katika michezo yake yote inayofuata

“Hii timu ni ya watanzania na jambo kubwa ni kuwaonesha  watanzania namna ambavyo sisi Serikali tunaifuatilia kwa karibu sana timu yetu, wote tumemsikia Mhe. Rais namna ambavyo anawiwa kuona mafanikio ya michezo,  ndio maana hatua kwa hatua ni lazima kuhakikisha timu ya taifa tunaifuatilia kila siku, kila muda na kila wakati ili kujua kinachoendelea.

Taifa stars ipo kambini ikijiandaa na Michuano ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, yanayohusisha wachezaji wa ndani (CHAN) yatakayofanyika Januari 16 hadi Februari 7 nchini Cameroon ambapo kabla ya michuano hiyo, Taifa stars Januari 10 na 13 itakutana na timu ya Taifa ya Congo katika mechi ya kirafiki ikiwa ni maandalizi ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.