Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais aendelea na ziara yake kisiwani Pemba asisitiza maslahi ya Wazanzibari ni zaidi kuliko vyama vya siasaMakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea na siku ya pili ya ziara yake Kisiwani Pemba kwa kukutana na Wananchi wa Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Wete Mkoa wa Kasksazini Pemba.

Maalim Seif alianza kwa kukutana na Wananchi wa makundi mbali mbali ambao ni Viongozi wa Serikali,viongozi wa Dini,Watu mashuhuri, Wazee, Vijana, wanawake na Watu wenye mahitaji maalum (walemavu), kutoka Wilaya ya Micheweni na baadae Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Makamo wa kwanza wa Rais wa  Zanzibar alikutana na Wananchi wa Wilaya ya Micheweni katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Karume Micheweni, na baadae kumalizia Wilaya ya Wete ambapo alikutana na Wananchi wa Wilaya hio katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete.

Katika Wilaya zote mbili Makamo wa Kwanza aliendelea kuwakumbusha Wananchi asili ya Zanzibar, tunu za Zanzibar, historia ya Zanzibar sambamba na kuonesha umuhimu wa kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika jamii zao kwani Wazanzibar ni wamoja.

Katika kusisitiza jambo hilo Maalim Seif alisema;

"Najua kuleta umoja muda mwengine ni kazi ngumu na inaweza kuchukua muda, lakini jambo litakalotufikisha huko ni dhamira zetu njema".

Maalim Seif amewaambia Wananchi hao kwamba nikweli yapo maumivu na madhila mengi ambayo yalishafanyika lakini bado ipo haja ya kuyazika ya nyuma na kuyasahau, na  kuongezea kwa kusema;

 "Wazanzibari kama kuumia tulishaumia sana kama kuteseka tulishateseka sana kwasasa tunasema sasa basi, tuamue kushirikiana na kujenga nchi yetu".

Kuhusu uhasama unaotokea kutokana na vyama vya siasa Maalim alifafanua kwa kusema,

 "Uhasama wa vyama vya siasa ulianza miaka mingi tangu enzi za Afroshiraz party, ila hatupaswi kufukua makaburi haya, wala hatupaswi kuifata historia mbaya na badala yake tuungane tuipeleke Zanzibar katika mustakbali mwema, Zanzibar ni yetu".

Maalim aliendelea kusisitiza kwamba ingawa Katiba inaturuhusu kila mtu awe na chama chake cha siasa, lakini  uwepo wa Vyama vya siasa visitutoe katika dhamira njema ya Uzanzibari wetu, kwani maslahi ya Wazanzibar ni zaidi kuliko vyama vya siasa.

Baada ya hotuba yake Makamo wa kwanza alitoa fursa kwa Wananchi wa Wilaya hizo kutoa michango yao ama kuuliza swali na kuyatolea ufafanuzi.

Akiwa Wilaya ya Micheweni Maalim Seif alifika kijiji cha Wingwi Njuguni kukagua soko la samaki la NJUGUNI.


Mwisho wa Ziara yake siku ya Leo Makamu  wa Kwanza wa Rais alitembelea sehemu maalum ya uwekezaji wa Viwanda Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.