Habari za Punde

Mapinduzi Cup yavuna mil 496

 NA MWAJUMA JUMA

JUMLA ya shilingi milioni 496.178,400 zimekusanywa katika michuano ya kombe la Mapinduzi yaliyofanyika visiwani Zanzibar mwaka huu.

Michuano hiyo ambayo iloshirikisha timu tisa yalimalizika Januari 13 mwaka huu na Yanga kutwaa ubingwa kwa ushindi wa penanti 4-2.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa VIP Amaan Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo Imane Duwe alisema kuwa fedha hizo zinatokana na makusanyo ya milangoni pamoja na wadhamini.

Alisema kuwa Kati ya fedha hizo fedha za makusanyo ya milangoni ni shilingi milioni 256,478,400 na wadhamini ni shilingi milioni 239,700,000, ambapo Azam pekee alitoa shilingi milioni 150.

Alifahamisha kwamba katika fedha za milangoni shilingi milioni 79,245,000 ni makusanyo yaliyotokana na mchezo wa fainali Kati ya Simba na Yanga.

Aidha alisema kuwa katika fedha hizo walitumia shilingi milioni 354,474,500 kwa shughuli mbali mbali ikiwemo gharama za taa ambazo kwa siku wanatumia shilingi milioni 1,500,000.

Matumizi mengine ni pamoja na gharama za kuwalipa waamuzi, malazi, chakula kwa timu pamoja na usafiri wa ndani ambao kwa siku walikuwa wakilipa 150,000.

Hata hivyo alisema kuwa mbali na matumizi hayo fedha ambazo zimebakia ni shilingi milioni 141,703,900.

Akizungumzia kuhusu mashindano yote kwa jumla alisema yalifanikiwa kwa kiasi licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zilijitokeza.

"Mashindano yalikuwa mazuri na yamefanikiwa lakini kulijitokeza changamoto ndogo ndogo ambazo waliweza kukabiliana nazo", alisema.

Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Simba, Yanga, Azam, Namungo na Mtibwa kutoka Tanzania Bara na kea Zanzibar ni Mlandege, Malindi, Jamhuri na Chipukizi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.