Habari za Punde

NIC yatoa Milioni 14.7 kufanikisha Mapinduzi Cup

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan King akimakaribisha Waziri Tabia Maulid Mwita kwenye mkutano na viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) uliofanyika Ofisi ya Wizara Migombani
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Bima la Taifa Tanzania Dkt. Elirehema Doriye akimueleza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jinsi walivyojiandaa katika kuimarisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi
Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita akilipongeza Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) kwa mchango waliotoa katika kufanikisha mashindano ya kombe la Mpinduzi katika mkutano uliofanyika Ofisini kwa Waziri Migombani.
Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita akilipongeza Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) kwa mchango waliotoa katika kufanikisha mashindano ya kombe la Mpinduzi katika mkutano uliofanyika Ofisini kwa Waziri Migombani.

Baadhi ya waalikwa walioshiriki mkutano wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na viongozi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Ofisini kwa Waziri Migombani.

Picha na Makame Mshenga


Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limetoa mchango wa shilingi 14, 700,000 kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya soka ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka huu yanayotarajiwa kuanza tarehe 5.1.2021 katika kiwanja cha Amani, Mjini Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye alimueleza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita kwamba wameamua kuyapa msukumo mashindano hayo baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaribisha Mashirika, Wafanyabiashara na wadau wa michezo kuchangia mashindano hayo.

Alisema lengo la mchango huo ni kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano na zawadi ya mchezaji bora kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu tisa, nne kutoka Zanzibar na tano kutoka Tanzania Bara.

Mkurugenzi Doriye alimuahidi Waziri Tabia Maulid Mwita kwamba NIC itaendelea kuwa washirika wa karibu wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa miaka mengine ijayao.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Wizarani kwake Migombani, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alilishukuru Shirika la Bima la Taifa Tanzania kwa msaada huo na ahadi walizotoa kwa miaka ijayo katika kuendesha mashindano hayo.

 Alisema mchango wa shilingi milioni 14 na laki saba waliotoa utasaidia sana katika kufanikisha mashindano ya mwaka huu ambayo yemekua endelevu tokea yalipoanzishwa kitaifa mwaka 2007.

Waziri Tabia aliwaeleza viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania kuwa Serikali imeazimia kuimarisha michezo mbali mbali ikiwemo Ligi kuu ya Zanzibar na michango ya wadau inahitajika katika kufanikisha lengo hilo.

Aliahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Shirika hilo na amewakaribisha kutumia vyombo vya Habari vilivyochini ya Wizira hiyo katika kuimarisha shughuli zao za kibiashara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.