Habari za Punde

Wakuu wa Wilaya wa Unguja na Pemba Watakiwa Kwenda Kuwatumikia Wananchi na Kuimarisha Ulinzi Katika Wilaya Zao - Dk Mwinyi

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wakuu wa Wilaya wapya aliowaapisha Ikulu leo na kuwataka kwenda kufanya Kazi na kuimarisha Ulinzi na Usalama katika Wilaya zao.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wakuu wapya wa Wilaya  walioapishwa kuhakikisha kunakuwepo ulinzi na usalama wa kutosha katika Wilaya zao.

Dk. Mwinyi ametoa maelekezo hayo wakati alipowaapisha Wakuu wa Wilaya kumi (10) za Unguja na Pemba, katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Disemba 28, mwaka 2020 Rais Dk. Mwinyi alifanya mabadiliko ya Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 11 za Zanzibar kwa kumteua Marina Joel Thomas kuwa Mkuu wa Wilaya Kati Unguja, Issa Juma Ali (Mkoani), Hamida Mussa Khamis (Magharibi ‘B’) na CDR Mohamed Mussa Seif kuwa Mkuu wa Wilaya Micheweni Pemba.

Wengine walioteuliwa na kuapishwa ni Rashid Simai Msaraka (Mjini Unguja), Sadifa Juma Khamis (Kaskazini ‘A’), Aboud Hassan Mwinyi (Kaskazini ‘B’), Rashid Makame Shamsi (Kusini Unguja), Mgeni Khatibu Yahya (Wete) na Abdalla Rashid Ali Wilaya ya Chakechake Pemba.

Alisema viongozi hao wakiwa Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na  Usalama katika Wilaya zao, wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwepo Ulinzi na Usalama wa kutosha wakati huu ambapo matukio mbali mbali ya uhalifu yakiwa yameshamiri.

Alieleza kuwa nchi haiwezi kupata maendeleo yoyote endapo   hakutakuwepo na amani na usalama  na kubainisha kuwepo kwa matukio mengi ya uhalifu, ikiwemo wizi wa mazao pamoja na mifugo, kiasi ambacho baadhi ya wananchi wameamua kuachana na kilimo au ufugaji.

Aliwataka Wakuu hao wa Wilaya kusikiliza migogoro mbali mbali inayowakabili wananchi pamoja na kutoa haki  kwa mambo yalio ndani ya uwezo wao na kuwataka kuyapeleka katika ngazi zinazohusika mambo yalio nje ya uwezo wao, akibainisha umuhimu wa kuondokana kabisa na migogoro iliyo ngazi za chini (shehiya).

Aidha, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala ya Usafi ndani ya Wilaya zao, kwa kigezo kuwa sekta ya Utalii ikiwa ndio mhimili wa Uchumi wa Zanzibar , inategemea zaidi kuwepo kwa usafi katika maeneo yote ya nchi.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi aligusia suala la Udhalilishaji wa watoto na wanawake kijinsia na kusema kuwa ni tatizo linalohitaji ushirikiano kati ya jamii, asasi za kiraia na wadau wote wa mapambano dhidi ya udhalilishaji , ikiwemo Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Mahakama.

Aliwataka wadau hao kuja na mipango mipya katika ushughulikiaji wa tatizo hilo linaloendelea kushamiri kila kukicha.

Aidha, aliwataka Wakuu hao wa Wilaya kufanya juhudi katika kuinua viwango vya elimu ndani ya Wilaya zao, kwa kuhakikisha kunakuwepo miundombinu bora, idadi ya walimu wanaotosheleza pamoja na vifaa vya kufundishia vilivyo katika hali nzuri.

Alisema katika miaka ya nyumba kulikuwa na mashindano yaliosaidia kuinua viwango vya wanafunzi kielimu, hivyo akabainisha umuhimu wa jambo hilo.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kwenda kufanya kazi kwa kujituma pamoja na kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yao, akibainisha kuwa wao sio viongozi wa kukaa ofisini muda wote.

“Ni muhimu kuwatembelea watu kwa kuwa kuna changamoto mbali mbali zinazowakabilia katika maeneo yao”, alisema.

Vile vile aliwataka viongozi hao  kuitekeleza kikamilifu Ilani ya CCM

ya 2020 -  2025 pamoja na kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi mkuu zinatekelezwa kikamilifu, akibainisha  na mwamko mkubwa walionao wananchi katika kupata maendeleo kwa haraka.

Pamoja na kuwashukuru Viongozi hao kwa kukubali uteuzi huo, Dk. Mwinyi aliwataka kuwa mstari wa mbele katika kukamilisha wajibu wao pamoja na kuwaondolea kero wananchi.

Hafla hiyo ya kiapo iliwashirikisha viongozi mbali mbali wa Kitaifa akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu,  Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na  Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji.

Wengine ni   Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Kinana, Wakuu wa Mikoa mitatu ya Zanzibar,  Makamanda wa vikosi vya Ulinzi na Usalama, Askofu Dickson Kaganga pamoja na wanafamilia,

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.