Habari za Punde

Serikali Itaendelea Kushirikiana na Jumuiya ya Wazee kwa Azma ya Kuhakikisha Wazee wananufaika.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo, yaliofanyika katika Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongezauongozi wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA), uliofika Ikulu kwa mazungumzo na Rais pamoja na kumpongeza.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jumuiya hizo zinahitajika kutokana na umuhimu wake mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wake kwa Serikali kwani si mambo yote Serikali inaweza kuyafanya.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya hizo kwa azma ya kuhakikisha wazee nao wananufaika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana kutokana na vitambulisho vinavyotolewa kwa ajili ya wazee.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alipokea pole iliyotolewa na uongozi wa Jumuiya hiyo kufuatia kifo cha Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Seif Sharif Hamad kilichotokea hivi karibuni.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Naibu Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeida Rashid Abdallah kwa ushirikiano wake mzuri anaouonesha kwa Jumuiya za wazee na kumtaka kuendelea na moyo wake huo.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Injinia Zena Ahmed Said alitoa pongezi kwa Jumuiya hiyo kwa malengo waliyonayo na kusisitiza haja ya kuendelea kuungwa mkono ili iweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Mapema viongozi wa Jumuiya hiyo walimpongeza Rais Dk.Hussein kwa ushindi wake mkubwa alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020 sambamba na mafanikio yaliyoanza kupatikana.

Uongozi huo pia, ulitumia fursa hiyo kumpa pole Rais Dk. Mwinyi kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia hivi karibuni na kusema kwamba msiba huo ni wa watu wote.

Katika maelezo yao, viongozi hao walieleza matarajio yao makubwa kutokana na uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.

Naibu Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeida Rashid Abdallah alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wazee wanapewa kipaumbele.

Katibu wa Jumuiya Amani Suleiman Kombo, alieleza kwamba Jumuia ya Wazee Zanzibar imeundwa kwa ajili ya maslahi ya wazee wa Zanzibar ambapo lengo lao kuu ni kuwasaidia wazee kupata mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu inayowahusu wazee kama vile masuala ya afya ya kibinaadamu ambapo pia, jumuia hiyo hufanya shughuli za kuwasaidia Wazee  kiuchumi na kijamii.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.