Habari za Punde

MABORESHO BANDARI YA KIGOMA YAONGEZA SHEHENA, MAPATO, YAIPIKU MWANZA

 

TPA KIGOMA                                                                                                                                               

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Mhandisi Deusidedit Kakoko amesema maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari ya Kigoma yameanza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa shehena ya mizigo pamoja na mapato. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Bandari ya Kigoma, Mhandisi Kakoko alisema shehena na mapato katika bandari hiyo yameongezeka kiasi cha kuipiku Bandari ya Mwanza ambayo ndiyo iliyokuwa ikiongoza kabla ya maboresho hayo. 

Alisema Bandari ya Kigoma ambayo inahusisha bandari zote zilizopo katika Ziwa Tanganyika imeanza kufanyiwa maboresho kuanzia mwaka 2016/17 ikihusisha ujenzi wa magati,  ununuzi wa mitambo,  ujenzi wa maghala na majengo ya abiria pamoja na ujenzi wa ofisi za kisasa za makao makuu ya Bandari hiyo ambazo ziko katika hatua za mwisho kukamilika.

Aliongeza kuwa maborsho hayo yalisukumwa na kasi kubwa ya ongezeko la mahitaji ikilinganishwa na miundombinu iliyokuwepo. 

Alisema bandari za Ziwa Tanganyika zimekuwa kiungo kikubwa cha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za DRC,  Burundi na Zambia, biashara kubwa ikiwa ni mazao yanayozalishwa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo alisema bandari hizo zimekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa wananchi wa mikoa inayozunguka Ziwa Tanganyika kwani mazao yao yanapata wanunuzi wengi wanaovutiwa na maboresho ya bandari.

Alisema pia bandari hizo pamoja na kuanza kazi kwa reli kumesaidia kupunguza bei za bidhaa ambazo husababishwa na gharama kubwa za usafirishaji. 

Alisema bado kuna maboresho zaidi yanaendelea katika bandari Kuu ya Kigoma yanahusisha ujenzi wa gati ya maboti ya Kibirizi,  gati ya abiria na makasha na ujenzi wa bandari Kavu ya Katosho.

"Tumekusudia kuifanya bandari ya Kibirizi na Kigoma kuwa ya mizigo ya nje na ile ya Katosho itakuwa ya ndani, " alisema Kakoko. 

Alisema matarijio ya kuongezeka zaidi kwa shehena na abiria ni makubwa kutokana na maboresho ya meli yanayotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Huduma za Meli zikiwemo MV Mwongozo,  MV Liemba na MT Sangara

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.