Mwashungi Tahir    Maelezo       15/3/2021. 
Mwakilishi wa viti maalum  Jimbo la Dimani Maryam Saleh Ali  amewataka wananchi wa jimbo hilo kuondoa muhali pale vinapotokea vitendo vya udhalilishaji ndani ya maeneo yao wanayoishi.
Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya udhalilishaji na kuwataka wanapofikwa na kadhia hiyo kujitokeza kutoa ushahidi ili hatua za mara moja  ziweze kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo. 
Amesema matukio haya ya udhalilishaji bado yanaendelea kukithiri nchini  na kuwataka wananchi hao kuondosha muhali iwapo suala hilo limemtokezea na kuhofia kama mume atampa talaka iwapo kamdhalilisha mwanawe wa kike au wa kiume. 
"Tuondosha muhali ili vitendo hivi viweze kumalizika pale vinapotokea  na tukiendelea kunyamaza havitoweza kumalizika vitendo hivyo", alisema Diwani huyo. 
Hivyo amewaasa akinamama kutolifumbia macho suala hilo kwani katika awamu ya nane ya Rais wa Zanzibar Dkt Husein Mwinyi  amelisimamia kidete suala la udhalilishaji na kuhakikisha linamalizika mara moja. 
Akitoa mada ya udhalilishaji Mwanasheria kutoka chama cha wanasheria  (ZAFELA) Time Asaa Khamis amesema kazi ya Zafela ni kutoa elimu ya kisheria  inayomgusa mwanamke na mtoto ili aweze kufunguka wakati anapokutana na vitendo hivyo. 
Amesema pia wanaendelea kutoa msaada  kwa wanaofikwa na masuala ya kubakwa, mirathi,malezi ya watoto pale wanafamiliya wanapoachana, mali walizozichuma wanafamilia na mambo mengine. 
Nao wananchi wa jimbo la Dimani wamefurahishwa kwa kupatiwa elimu na wameahidi watakuwa katika mstari wa mbele kusimamia haki zao pale zinapostahiki na kuondoa muhali wakati anapofikwa na vitendo vya udhalilishaji.

No comments:
Post a Comment