Habari za Punde

Wanafunzi Wote Waliokuwa Hawakuhudhuria Shule Kuanzia 1 Marchi 2021 Kuazia Shule za Msingi na Sekondari Wazazi Wao Kuchukuliwa Hatua.

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

KUFUATIA kitendo cha  wanafunzi 25 wa kata ya Malezi waliomaliza darasa la saba na kufaulu kuingia kidato cha kwanza kutohudhuria masomo kuanzia januari mwaka huu, onyo kali limetolewa kuhusu Mtendaji wa kata hiyo pamoja na wazazi.

Wazazi wa kata hiyo wanahusishwa na tuhuma za kuwashawishi na kuwakataza watoto wao kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho kwa lengo la kufeli na kudaiwa kuwaozesha huku Mtendaji wa kata hiyo akiwa hatou taarifa yoyote juu ya kinachotokea kwa upande wa elimu.

Akisoma risala mbele ya Mbunge wa Handeni mji Reuben Kwagilwa, Ofisa Elimu kata hiyo George Silas alisema kutokana na kata hiyo kutokua na shule ya sekondari baadhi ya wazazi wanachukulia changamoto ya umbali wa kufuata shule kata ya Kwenjugo ambapo kuna takribani kilomita 6 kuwa kigezo cha kuwakataza watoto wao kuacha kwenda.

"Changamoto tuliyonayo hapa ni baadhi ya wananchi hawana uelewa kuhusu umuhimu wa elimu, kutokana na hili huamua kuwafanya watoto wao kutohudhuria masomo na kusababisha utoro na hata wengine kuacha kabisa shule" alisema Silas.

"Na kutokana na changamoto hii pia huwakataza watoto wao wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi, niseme kwamba kwa hali hii sasa inaonekana kuna ukinzani kati ya maelekezo ya Rais kuhusu elimu na mitazamo duni ya wazazi, tunahitaji kubadilika" aliongeza.

Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Handeni Mussa Mkombati amemuagiza diwani wa kata ya Malezi kusimamia suala hilo na kuhakikisha wanafunzi ambao hawajahudhuria shule tangu zimefunguliwa wanakwenda mara moja na wale ambao ni watoro kurudi huku akisisitiza kuwa mzazi atakayekaidi agizo hilo achukuliwe hatua.

Mkombati alisema wazazi wanapaswa kuwahimiza na kuwaandaa wanafunzi kwa kuwajengea msingi wa kupenda shule ikizingatiwa kwamba hakuna urithi wa mtoto wa kudumu kama elimu hivyo kitendo cha kuwaacha wanazembea ni kuwapotezea malengo na kuua nguvu kazi ya Taifa la baadae.

"Nitoe agizo kwa mtendaji kuhakikisha watoto wote hao 35 wanaotakiwa kwenda shule waende, uwepo wako hapa utakua hauna maana kama unaangalia wanapotea na hatua huchukui, wazazi wenzangu wenye watoto hawa wapelekeni watoto shule mtakuja kuona faida yake baadae sio leo, kesho watakuja kuwasaidia" alisema Mkombati.

Agizo la Mkombati limekuja kufuatia lalamiko la Ofisa elimu msingi Elizabeth Kiraya kusema kuwa kuna wanafunzi 25 wa kata ya Malezi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza walipatiwa msaada wa sare za shule na Mkurugenzi wa Handeni mjini lakini hadi sasa hawajahudhuria shuleni na wazazi wao hawajafika kutoa taarifa yoyote.

Kiraya pia alibainisha kwamba katika takwimu zilizopo imeonesha kuwa kata hiyo imefanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa darasa la saba na hali hiyo inatokana na utoro wa mara kwa mara wa wanafunzi huku akiwaomba viongozi ngazi za chini kutoa ushirikiano katika kuhakikisha watoto hao wanahuduria masomo kuanzia darasa la awali.

Takwimu tulizonazo zinatuonesha kata inayofanya vibaya ni hii Malezi, na hili linajionesha dhahiri hapa leo kwani muda huu ni wa masomo lakini watoto karibu wote wanaostahili kuwepo huko wako hapa, niwaombe viongozi hapa myusaidie kuhakikisha hawa watoto wanakwenda shule" alisema Kiraya.

Hata hivyo Mbunge wa jimbo hilo Kwagilwa alisema serikali inatoa ada kwa ajili wanafunzi wasome bure lakini inakua ni kinyume cha afizo la Rais na kutoa agizo la wanafunzi wote wanaostahili kwenda shule wafanye hivyo kuanzia jumatatu huku akisisitiza kuchukuliwa hatua wote watakaokaidi ikiwa ni pamoja na wazazi wao.

Baada ya kuzungumza na wananchi hao Kwagilwa alikabidhi bati 54 kwa ajili ya kumalizia shule ya sekondari ya kata pamoja na kukagua mradi wa maji ulioanza kutekelezwa katika mtaa wa Kilimilang'ombe na kusema kuwa umegarimu kiasi cha shilingi milioni 247.5 na unatarajiwa kumalizika mwezi wa tano mwaka huu.

"Tenki hili la maji linalowekwa hapa lina ujazo wa lita laki moja ambalo ni sawa na lile lililojengwa kule mtaa wa Malezi, kwahiyo ndani ya kata hii mtakua na lita laki mbili ambazo zitahifadhiwa, zikishuka zikiisha zinajazwa nyingine, kwahiyo hili tenki litahudumia hapa na Kwediziwa, lakini mradi huu tunataka ukamilike mwezi wa tano" alibainisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.