Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amewakaribisha Wawekezaji Kutoka Inchini Indonesia Kuwekeza Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe.Prof.Ratlan Pardede, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha alipofika Ikulu leo 2-3-2021 kwa mazungumzo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe.Prof. Ratlan Pardede, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe.Prof. Ratlan Pardede, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Indonesia kuja kuekeza Zanzibar kutokana na kuwepo mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane anayoiongoza.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Indonesia nchini Tanzania Profesa Ratlan  Pardede wakati alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kufanya mazungumzo na  Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Pardede kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imedhamiria kuimarisha uchumi wake hivyo iko tayari kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo ikiwemo Indonesia.

Alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na Indonesia hasa katika uimatrishaji wa sekta ambali mbali za maendelo hivyo, Serikali anayoiongoza imewacha milango yake wazi kwa wawekezaji wa Indonesia kuja kuekeza Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Pardede kwamba Zanzibar ina maeneo kadhaa ya kushirikiana na Indonesia hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa  kiuchumi.

Akimueleza kuhusu Sekta ya uwekezaji alisema kuwa Zanzibar iko tayari kuwakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuekeza katika sekta ya Bandari ukiwemo mradi ambao hivi sasa umo kwenye upembuzi yakinifu wa Bandari ya Mangapwani/Bumbwini mara tu utakapokuwa tayari kuanza.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba mbali ya uwekezaji katika sekta hiyo pia, kutokana na nchi hiyo kupata maendeleo makubwa katika sekta ya utalii, Zanzibar pia, inawakaribisha wawekezaji katika sekta hiyo kuja kuekeza  hapa nchini.

Alieleza kwamba Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio kadhaa vya utalii hivyo, milango yake iko wazi kwa wawekezaji wa sekta hiyo kutoka Indonesia kuja kuekeza.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Indonesia kwa kufungua kiwanda cha kusarifu majani makavu na yaliyoanguka wenyewe ya mkarafuu kiliopo Mgelema, Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Indonesia kujenga kiwanda cha mwani hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba bidhaa hiyo inalimwa kwa wingi hapa nchini lakini bado wakulima wake hajanufaika na bei ya zao hilo sambamba na kutokuwepo kwa soko la uhakika.

Hivyo, Rais alieleza haja ya kiongozi huyo kuzungumza na wawekezaji wa Indonesia kwa azma ya kulipa thamani zao hilo kwa kuwa na soko la uhakika ikiwa ni pmaoja na kuanzisha kiwanda hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi pia, alizungumzia juu ya zao la karafuu na kumueleza Balozi huyo wa Indonesia jinsi Serikali anayoiongoza inavyofanya juhudi ya kuliimarisha zao hilo na kumueleza haja ya kuimarisha soko la bidhaa hiyo kwa Indonesia.

Nae Balozi wa Jamhuri ya Indonesia nchini Tanzania, Ratlan Pardede alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuitangaza zaidi Zanzibar kwa wawekezaji wa Indonesia.

Balozi Pardede alitumia fursa hiyo kumpa pole Rais Dk. Mwinyi kufuatia msiba wa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, uliotokea hivi karibuni na kueleza kwamba nchi yake inaungana na wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima katika msiba wa kiongozi huyo.

Aidha, Balozi Pardede alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mwanzo mzuri aliouonesha katika uongozi wake sambamba na kuonekanwa kwa mwanga wa matumaini na mafanikio makubwa katika siku mia moja za uongozi wake.

Katika maelezo yake, Balozi huyo wa Indonesia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba nchi yake tayari imeshasaini Hati kadhaa za Makubaliano (MOU) na Zanzibar ikiwa na nia ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Balozi Pardede alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba atahakikisha wawekezaji kutoka Indonesia wanakuja kuekeza katika miradi kadhaa hapa nchini ukiwemo mradi wa bandari kuu ya Mangapwani/Bumbwini mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.

Katika mazungumzo hayo, Balozi huyo wa Indonesia alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua mbali mbali zitakazochukuliwa na nchi yake katika kuhakikisha inaiunga mkono Zanzibar katika kufikia malengo yake ya kukuza uchumi wake.

Pamoja na hayo, Balozi huyo aliipongeza kasi ya Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na kuahidi kuiunga mkono hasa ikizingatiwa kwamba Indonesia na Zanzibar zote ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA).

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.