Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amewaapisha Viongozi Aliowateu Hivi Karibuni.

 

Mawaziri Wateule wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walioteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakiwa katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar wakisubiri kuapishwa kutoka (kulia) Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Ndg. Salum Yussuf Ali, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar  Mhe. Omar Said Shaaban, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.Mhe.Dkt. Saada Mkuya Salum. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amewaapisha Mawaziri watatu aliowateua Machi 03, mwaka huu, kushika nyadhifa katika Wizara tofauti za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mawaziri walioapishwa ni  Dk. Sada Mkuya Salum anaekuwa Waziri katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Nassor Ahmeid Mazrui (Wizara Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto) pamoja na Omar Said Shaaban atakaeiongoza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

Uteuzi wa Mawaziri hao unakamilisha idadi ya Mawaziri 16 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya Wizara hizo (tatu) kuwa wazi tangu pale Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alipotangaza Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza                Novemba 19, 2020.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Salum Yussuf Ali kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) baada ya kumteua February 10, 2021.

Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa  na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamoja na  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.

Wengine ni pamoja na Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Vyama vya Saisa pamoja na wanafamilia.

Rais Dk. Mwinyi amewaapisha Viongozi hao kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Vifunguvya 42, 43 (1) (2) na 44 vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka1984.

Katika hatua nyengine, wakizungumza na vyombo vya habari, Mawaziri hao wamesema wamejipanga kumsaidia Rais Dk. Mwinyi ili kukidhi matarajio makubwa waliyonayo Wazanzibari katika kupata maendeleo.

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Sada Mkuya Salum alisema atahakikisha utekelezaji wa  sera ya uchumi  unafanyika kuambatana na  usimamizi mzuri wa mazingira yaliopo.

Aidha, alisema atahakikisha sera ana sheria zote zitakazotungwa na kutekelezwa znchini inazingatia masuala yote mtambuka.

Nae, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban alisema atafanya kila juhudi kuhakikisha Zanzibar inarejea katika hadhi yake ya kuwa kitovu cha Biashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Alisema ili kufanikisha azma ya Uchumi wa Buluu, atahakikisha Zanzibar inanufaika na malighafi zote za bahari.

“ Chini ya usimamizi wa Rais, tumejipanga kutoa huduma bora kwa wananchi”, alisema Waziri wa Afya ,Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Nassor Ahmeid Mazrui.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.