Habari za Punde

Serikali itaendelea kuzingatia jinsia wakati wa uteuzi wa watendaji nafasi za viongozi

Washiriki wa Kongamano wakifutilia hotuba ya Rais iliosomwa na Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba yake  iliyotolewa  katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika Ukumbi wa sheikh Idrissa Abdulwakili Kikwajuni.
Washiriki wa Kongamano wakifutilia hotuba ya Rais iliosomwa na Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba yake  iliotolewa  katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika Ukumbi wa sheikh Idrissa Abdulwakili Kikwajuni.
Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii wazee jinsia na watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazurui akiwakumbusha washiriki wa kongamano kuachana na fikra potofu zinazopelekea kumosesha haki za msingi mwanamke katika kongamano la siku ya maadhimisho ya wanawake duniani lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akihotubia katika kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake duniani lililofanyika katika ukumbi ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili Kikwajuni ambapo Mhe. Hemed alimuwakilisha Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.
 


Na Kassim Abdi OMPR

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane itaendelea kuzingatia jinsia wakati wa uteuzi wa watendaji mbali mbali katika nafasi za uongozi.

Amesema serikali itahakikisha inawashirikisha wanawake kikamilifu kwa  kushiriki moja kwa moja katika kila sehemu yenye nafasi ya kupitisha na kutoa maamuzi.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza hayo kupitia hotuba iliosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake dunaini lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili Kikwajuni.

Mhe. Hemed alieleza kwamba ni jamii ina kila sababu ya kuipongeza kwa dhati serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa jitihada inazozichukua katika kuinua hali na hadhi ya wanawake Zanzibar kutokana na suala la ushiriki na kutoa maamuzi kuingizwa ndani ya katiba ya Zanzibar.

“Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu 21(2) kimeleza kwamba kila mzanzibar anayohaki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu yeye maisha yake na yanayolihusu Taifa”

Hata hivyo, Makamu wa Pili wa Rais alifafanua kuwa katiba ya Zanzibar imendelea kumthamini mwanamke akitolea mfano kifungu namba (67(1) kimeleza uwepo wa wajumbe wa baraza la wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia arubaini (40%) ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo ya uchaguzi.

Alisitiza kuwa maamuzi hayo ya kikatiba yamechangia kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika baraza la wawakilishi hali iliosababisha suala la ushiriki nwa wanawake katika maamuzi kuanishwa katika sheria na sera tofauti.

Aidha, Mhe. Hemed alisema Pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi lakini bado zipo baadhi ya changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo  ya wanawake.

Akitolea mfano baadhi ya changamoto hizo alizitaja pamoja na kuwepo kwa mifumo ndani ya vyama vya siasa isiyotoa kipaumbele kwa wanawake kushika nafasi za uongozi hali inayopelekea kukosekana kwa usawa baina ya wanawake na wanaume na wanaume katika nafasi za uongozi.

Pia, alisema baadhi ya wanawake hujitokeza kugombea nafasi mbali mbali lakini kitu kibaya kinachojitokeza ni kukumbwa na changamoto ya udhalilishaji jambo ambalo hupelekea baadhi yao kukata tamaa.

“Niseme tu pia mifumo ya malezi ya watoto ndani ya jamii isiojenga uthubutu wa kujiamini kwa motto mwanamke pamoja na kuwepo mfumo dume unaompa kipaumbele mwanamme na kujenga fikra potofu dhidi ya mwanamke ni changamoto nyengine”.

Sambamba na hayo, Makamu wa pili wa Rais alieleza kuwa umefika wakati sasa kila mmoja wetu kubadili fikra na mitazamo juu ya suala muhimu la ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi na maamuzi, na kuongeza kuwa kuna haja kwa jamii nzima kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Afya ustawi wa jamii wazee jinsia na watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazurui aliwaomba wananchi kuachana na fikra potofu ili kuisaidia serikali kufikia malengo yake ya kuwashirikisha wanawake katika ngazi za maamuzi.

Waziri Mazuru alieleza kuwa, ni miaka arubaini na sita sasa (46) tangu umoja wa mataifa ulipoanza kuazimisha siku hii tangu mwaka 1991 ambapo kwa Zanzibar siku hii ilianza kuazimishwa mara baada ya kuanzishwa kwa idara ya maendeleo ya wanawake kikiwa ni chombo cha kuratibu juhudi za kufikia usawa kwa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake Zanzibar.

Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 08 Machi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “BADILI FIKRA:IMARISHA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA MAAMUZI KWA MAENDELEO ENDELEVU”.

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.