Habari za Punde

ZEC yajipanga na uchaguzi mdogo jimbo la Pandani na kwa nafasi ya udiwani wadi ya Kinuni

 Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pangawe (kushoto) akimkabidhi fomu ya uteuzi Mgombea wa Udiwani Uchaguzi Mdogo Wadi ya Kinuni Salama Rajab Msangi tarehe 04 Machi, 2021 katika Ofisi ya Uchaguzi ya WIlaya ya Magharibi " B" Maisara Mjini Zanzibar ( Picha na Jaala Makame Haji - ZEC)
 

Na Jaala Makame Haji- ZEC

Mgombea wa Udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi Bi Salama Rajabu Masinga amekuwa wa kwanza kuchukuwa fomu ya uteuzi kugombea nafasi ya Udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Kinuni unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Machi,2021.

Akizungumza katika hafla ya uchukuaji fomu ya Uteuzi iliyofanyika Maisara katika Ofisi ya Uchaguzi ya Wilaya Magharibi “B” Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pangawe Suluhu Ali Rashid alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar haitoandikisha Wapiga Kura Wapya kwa ajili ya kushiriki katika Uchaguzi Mdogo huo  na badala yake wapiga kura walioandikishwa katika Daftari la Kudumu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2020 ndio watakaohusika kupiga Kura katika Uchaguzi Mdogo huo

Aidha, Bwana Suluhu aliviomba vyama vyengine vya Siasa kujitokeza kuchukua fomu za uteuzi ili viteuliwe na Tume kushiriki katika Uchaguzi kwa ngazi ya Uwakilishi Jimbo la Pandani na Udiwani Wadi ya Kinuni

Naye, Mgombea wa Udiwani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Salama Rajabu Masinga aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoelekezwa na Tume ya Uchaguzi katika ujazaji wa fomu za uteuzi kwa kufuata Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pandani aliwataja Wagombea Wa Uwakilishi waliochukuwa fomu za uteuzi kuwa ni Mohammed Juma Ali kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Said Hamad Ali Demokrasia Makini, Prof. Omar Fakih Hamad ACT Wazalendo na Ali Hamad Omar wa ADA TADEA

Mgombea wa Uwakilishi Masoud Ali Said  na Mgombea wa Udiwani Kassim Ali Abdalla kupitia chama cha Wananchi CUF wanatarajiwa kuchukuwa fomu za Uteuzi kesho tarehe 5 Machi, 2021 katika Ofisi ya Uchaguzi ya Wilaya ya Wete saa tano asubuh na saa tisa alasiri Ofisi ya Uchaguzi Wilaya ya Magharib “B” iliyopo Maisara Unguja


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.