Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais, Mhe Hemed afungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa, katika ukumbi wa Halmashauri Wilaya ya Kaskazini “B” Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr Hussein Ali.
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa wakimsikiliza kwa makini Mheshimiwa Hemed Suleiman aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar kwenye Ufunguzi wa Mkutano wao.
Waziri wa Habari , Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kuufungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa, katika ukumbi wa Halmashauri Wilaya ya Kaskazini “B” Bumbwini.

Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unaguja Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mhmoud aliteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Baraza la vijana ili kuhakikisha changamoto na mapendekezo yanayowahusu vijana yanazungumzwa na kufikishwa sehemu husika katika wakati muafaka

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr Hussein Ali Mwinyi alitoa kauli katika hotuba iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa, katika ukumbi wa Halmashauri Wilaya ya Kaskazini “B” Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema Serikali imeanzisha Baraza la Vijana kupitia sheria nambari 16 ya mwaka 2013 ikiwa na dhamira ya kuzalisha vijana wazalendo, kuwafinyanga pamoja na kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadae.

Aidha Mhe. Hemed alisema Baraza la vijana ni kiungo na ni jukwaa la kuwasilisha na kuwasemea vijana juu ya mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo yao, ili kufikishwa sehemu husika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwasihi vijana kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vitendo viovu, akitolea mfano matumizi ya dawa za kulevya, ongezeko la maambukizi ya VVU na ukimwi, pamoja na matendo ya udhalilishaji, kwani vijana ndio asilimia kubwa wanaongoza katika matendo hayo.

Akiwanasihi viongozi wapya wa Baraza hilo Mhe. Hemed amewataka kuzingatia majukumu yao ndani ya baraza ili kujenga mustakbali mwema kwa vijana wanaowaongoza na wahakikishe wanaisoma sheria na kanuni ya kuanzishwa baraza hilo

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Habari , Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita, alisema kwa kuwa wakazi wa Zanzibar zaidi ya asilimia 70 ni vijana, wizara anayoiongoza imejipanga kuona sekta ya vijana inakuwa ni agenda namba moja, kwa ajili ya maslahi ya Taifa.

Waziri Tabia alisema wizara inafahamu changamoto mbali mbali zinazowakabili vijana , hivyo wamejipanga  kuzitatua changamoto hizo, hasa ile ya ajira na kuwataka vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Uchumi wa Buluu, na hata wa viwanda.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Vijana anaemaliza muda wake Ndugu Khamis Kheir alimshukuru Rais wa Awamu ya saba Mhe. Dr Ali Muhamed Shein kwa kuona umuhimu wa kuanzisha baraza hilo kwa maslahi mapana ya Zanzibar.

Aidha aliiomba Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo kuhakikisha wanazitatua changamoto zinazowakabili vijana, lakini pia kusaidia kusimamia na kuendeleza miradi inayoanzishwa na vijana hao ili kuunga mkono juhudi zao.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.