Habari za Punde

Mhe Hemed akutana na uongozi wa Jumuiya ya Taasisi za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi Mpya wa Jumuiya ya Taasisi za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) na ule uliomaliza muda wake wakati walipofika ofisini kwake vuga jijini Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Jumuiya  ya TAHLISO Ndugu Peter Josphet Niboye akimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa jitihada zake anazozichukua katika kukuzua Elimu Nchini pamoja na msimamo wake dhidi ya kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

Mwenyekiti wa Jumuiya  ya TAHLISO Ndugu Peter Josphet Niboy Kushoto akimkabidhi Mheshimiwa Hemed Suleiman Ripoti Maalum ya Utekelezaji wa  jukumu lao wakati walipishika wadhifa wa kuiongoza Jumuiya ya TAHLISO.

Picha na - OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameupongeza uongozi wa Jumuiya ya Taasisi za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) unaomaliza muda wake kwa mafanikio makubwa waliyoyapata katika kusaidia maendeleo ya Wanafunzi Vyuoni.

Mheshimiwa Hemed  ameyasema hayo, wakati akizungumza na viongozi wa taasisi hiyo wanaomaliza muda wao na kuwatambulisha viongozi wapya waliochaguliwa wakati walipofika ofisini kwake vuga jijini Zanzibar.

Amesema mashirikiano waliyoyaonyesha kati yao na viongozi wa vyuo pamoja na serikali kuu  yameisaidia sana serikali kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu  nchini akitolea mfano suala la upatikanaji wa mikopo.

Mheshimiwa Hemed ameendelea kuwasihi viongozi hao kuendeleza ushirikiano kati yao ili Taifa liweze kupata maendeleo zaidi hasa katika sekta  ya elimu, na kuwaeleza kuwa Serikali inawaamini vijana kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kufanikisha  maendeleo ya taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa viongozi wapya  wa taasisi hiyo waliochaguliwa kujenga uzalendo kwa kuachana na muhali katika uwajibikaji wao kwa kuunga jitihada za viongozi wa serikali hasa kwenye kupiga vita rushwa, ubadhirifu, uzembe, uhujumu wa uchumi mambo ambayo yanazorotesha ufanisi katika majukumu yao.

Kuhusu elimu nchini, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vyuo vikuu  kwa kutambua kuwa ni eneo muhimu lenye mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya Taifa.

Amewataka viongozi hao kuendelea kueleza mema yanayofanywa na Serikali zote mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akitolea mfano  kuhubiri faida za Muungano wa Tanzania ulioasisiwa totea mwaka 1964.

Mheshimiwa Hemed amewahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kutoa mashirikiano na kuwaeleza kuwa inafurahishwa kuona taasisi mfano wa hizi zikiwajibika vyema, na kuwataka wasisite kuomba ushauri kutoka serikalini pale watakapohitaji.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya  hiyo Ndugu Peter Josphet Niboye amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa jitihada zake anazozichukua katika kukuzua Elimu Nchini pamoja na msimamo wake dhidi ya kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

 Akigusia suala la mafanikio ya taasisi hiyo, Ndugu Niboye amesema katika kipindi cha  Uongozi wao wamefanikiwa kutatua changamoto mbali mbali za wanafunzi huku wakihubiri suala la Amani, utulivu na kuondosha migomo ya wanafunzi hali iliosaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kupatikana kwa utulivu vyuoni.

Uongozi wa jumuiya ya taasisi za wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania, wamekuwa wakishirikina na taasisi mbali mbali za serikali, tokea kuasisiwa kwake.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.