Habari za Punde

SERIKALI KUTOA ELIMU YA KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI KWA WANANCHI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza na  wakazi wa  Kijiji cha Maore kilichopo katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja kwa ajili ya kuzungumza na Wananchi hao
Mbunge wa Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malecela akimpongeza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja pamoja na Uongozi wa Wizara hiyo kwa kukubali  kufanya ziara katika jimbo hilo ili kutatua kero za wananchi wanaosumbuliwa na uvamizi wa tembo katika maeneo yao.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Wakazi wa Kijiji cha Maore kilichopo katika  Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ambapo amewahakikishia Wananchi hao kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inatatua  kero ya Tembo kuingia kwenye maeneo ya makazi yao
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Maore kilichopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja leo wakati alipokuwa akizungumza nao namna ya kukabiliana na Wanyapori wakali na Waharibifu


Naibu Waziri wa Malialisi na Utalii Mhe. Mary Masanja amesema  Serikali imeanza kutoa elimu kwa Wananchi  namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kupitia Wataalamu wa masuala ya Wanyamapori ikiwa lengo ni  kulinda usalama wa Wananchi na mali zao.

Naibu Waziri Mhe.Masanja ametoa kauli hiyo leo katika kijiji cha Maore kilichopo Wilaya ya Same  Mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakikumbwa na  uvamizi wa Tembo katika maeneo yao.

’’Serikali inasikitika inapoona Wananchi wake wanateseka na  wanyamapori  wakali kama vile tembo, Tumetafuta mbinu mbadala ya kuhakikisha Wananchi mnafundishwa namna bora ya kukabiliana na Wanyamapori hawa, amesisitiza Mhe. Masanja.

Amesema  mbali ya kutolewa kwa elimu hiyo ya kukabiliana na Wanyamapori hao, Serikali itagawa vifaa maalum kwa ajili ya kuwafukuza tembo wanapofika katika maeneo yao ikiwa  pamoja na kuwapatia namba ya simu za  askari watakaokuwa   wakipatiwa taarifa  pale tembo wanapovamia maeneo yao ili waje kutoa msaada kwa haraka kabla tembo hawajasababisha madhara kwa Wananchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Mary amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Kushirikiana na Wizara ya Ardhi itatenga  maeneo maalumu kwa ajili ya Mifugo ili  kuepusha wananchi kukumbwa na changamoto ya kuharibiwa mali zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.