Habari za Punde

SMZ Imeamua Kubadilisha Matumizi ya Mashamba ya Mpira Yalioko Kichwele na Selem Kuwa Maeneo ya Viwanda.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akitembelea Shamba la Kilimo cha Mpira katika Kijiji cha Kichwele Mkoa wa Kaskazini Unguja akitowa agizo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo Zanzibar Bi. Maryam Juma Abdalla wakati wa ziara yake hiyo na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.Mhe Omar Said Shaban na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeamua kubadili matumizi mashamba ya mpira yalioko Kichwele na Selem na kuwa ‘maeneo ya viwanda’ kufuatia mashamba hayo kutotumika ipasavyo na kuleta tija kwa Taifa.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo baada ya kufanya ziara ya kutembelea mashamba ya Mpira ya Selem  (Mkoa wa Mjini Magharibi) pamoja na Kichwele lilioko Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema mashamba  hayo yenye wastani wa ukubwa wa Hekta 638 yamekuwa na tija ndogo kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji baada ya  miti yake kuzeeka, pamoja na mwekezaji  kukabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo madeni yatokanayo na mkopo wa Benki, kushindwa kulipa fedha za Serikali na stahiki za wafanyakazi.

Alisema Serikali imechukua maamuzi ya makusudi wa kuyageuza mashamba hayo kuwa maeneo ya Viwanda kwa vile yamekuwa  hayalinuishi Taifa , sio kwa ajira wala kuingizia kipato  Serikali.

Alisema azma ya Serikali ni kuwa na viwanda vingi ili wananchi waweze kupata ajira, hivyo kuwepo kwa mashamba makubwa kama hayo bila ya kuzalisha sio jambo muafaka.

“Serikali imeona ni jambo la busara kutafuta wawekezaji na kuyatengeneza kuwa maeneo ya viwanda na tayari kuna baadhi ya wawekezaji wamejitokeza kwa ajili hiyo”, alisema.

Alisema  ni vyema eneo hili likatumika kwa shughuli zitakazoleta tija na kubainisha kuwa hilo ni  eneo  zuri  linalohitaji fedha  kuliboresha kwa shughuli za viwanda.

Alisema ni vyema kwa Serikali kutekeleza mpango huo kwa vile utafanikisha upatikanaji wa ajira kwa vijana, hatua aliyoinasibisha na ahad aliyoitowa katika Kampeni za Uchaguzi mkuu ya  kutengeneza ajira 300,000 nchini.

Aidha, alisema kutokana na mazingira yaliopo nchini, hakuna sababu ya kila kitu kutoka nje ya Zanzibar na kubainisha umuhimu wa baadhi ya bidhaa kupatikana hapa hapa.

Aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuwa tayari kuipokea nia  njema ya Serikali inayolenga kuleta tija kutokana uingizaji wa mapato pamoja na ajira kwa vijana, pamoja na  kuagiza uongozi wa Mikoa hiyo kuitangaza nia hiyo.  

Rais Dk. Mwinyi aliwahakikisha wananchi kuwa itayashughulikia kikamilifu matatizo yote yalioachwa na Mwekezaji kabla ya mipango mipya ya kubadili matumizi ya maeneo hayo haijaaanza.

Aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kuyawekea utambulisho (beacons) mashamba hayo, sambamba na Wizara ya Kilimo ,Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo  kuyakabidhi ZIPPA kwa shughuli zote za Uwekezaji.

Alisema hivi sasa ZIPA inapaswa kuwa kituo kimoja kwa ajili ya shughuli za  Uwekezaji ili kuondokana na urasimu usio na lazima.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Maryam Abdalla Sadalla alisema kuna Hekari zipatazo 1270 za mashamba ya Mpira Unguja na Pemba.     

Aidha, alisema uendeshaji wa mashamba hayo katika eneo la Kichwele na Selem yalikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo Mwekezaji kushindwa kulipa deni la Serikali la US Dolla 400,000  kwa miaka minne, deni la mkopo wa PBZ la Us Dolla 60,000 pamoja na malipo ya wafanyakazi kwa takriban miezi mitano, kutokana na kushuka kwa uzalishaji.

Nae, Mkuu wa Mkoa Kaksazini Unguja, Ayoub Maohamed Mahamoud, aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliotolewa katika ziara hiyo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.