Habari za Punde

Tume ya Kitaifa ya Kuratibu Dawa za Kulevya Zanzibar Yamuaga Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume Hiyo.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Saada Mkuya Salum akimkabidhi cheti cha shukurani na ukumbusho aliekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Migombani



Na.Raya Hamad – OMKR

Heshima, nidhamu na uzoefu umepelekea Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kuonekana inatekeleza majukumu yake na kuleta mabadiliko makubwa kwa watendaji na jamii inayoitumikia. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt.Saada Mkuya Salum ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hio Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis kwenye ukumbi wa mkutano Migombani.

Dkt.Saada amesema ujasiri na kujiamini kwake kumepelekea hata watendaji wa Tume kuonekana wapo tayari muda wote kwenye kutekeleza majukumu yao na kufikia malengo kwa mujibu wa majukumu yao ya kazi katika kudhibiti dawa za kulevya, na kupelekea kuiletea heshima nchi yetu kitaifa na kimataifa.

Aidha Dkt Saada amemshukuru Bi. Kheriyangu kwa utumishi wake na namna alivyoweza kuisimamia taasisi yake pamoja na kuwa shughulikia vyema vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya kuona wanapata nafuu

‘kumtoa mtu katika mazingira hatarishi ya matumizi ya dawa za kulevya na ukamtengeneza akarudi katika hali yake ya awali na kuanza kuaminiwa na familia na marafiki sio masihara,tumeona ubunifu wa kazi nzuri wanazozifanya huku akizionesha mfano wa kazi hizo’ alisisitiza Dkt.Saada.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi Khadija Khamis Rajab amesifu jitihada zilizooneshwa na mkurugenzi huyo na kumuomba kuendelea kutoa ushirikiano na ushauri pale panapohitajika.

Akitoa shukurani kwa viongozi wakuu na wakuu wa Taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifaya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis amesema mashirikiano aliyoyapata yamemuwezesha kufanyakazi zakek wa ufanisi.

Kheriyangu amesisitiza kuwa maamuzi yote aliyokuwa akiyatoa yalikuwa yanapitia kwenye vikao kazi kwa pamoja jambo ambalo limeiwezesha Tume hiyo kupata mafanikio makubwa katika utendaji wa majukumu yake.

Aidha amejifunza mengi ya msingi ikiwemo maisha ya kijami ikwa vile wakati anateuliwa 2013 alikuwa anatokea kwenye jeshi la polisi jambo hili litamsaidia kufahamu namna ya kupambana na wahalifu wakati wa kuendelea na majukumu yake katika jeshi la polisi kwa vile tayari anamtandao mzuri na wanajamii.

Nae Mkurugenzi Mtendaji mpya Luteni Kanal Burhani Nassoro wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ameahidi kushirikiana na watendaji na wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa na mtangulizi wake kubuni mbinu mpya katika kusimamia majukumu ya Tume hio.

Akitoa shukurani kwa niaba ya wakurugenzi na wafanyakazi Mkurugenzi Mtendaji Tume ya UKIMWI Zanzibar Dkt. Ahmeid Mohamed Khatib Reja amemshukuru mkurugenzi anaeondoka na kusema kuwa ameacha alama ya upendo na nidhamu iliyodumisha maelewano kwa watendaji na wafanyakazi.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imemzawadia cheti cha shukurani pamoja na zawadi nyengine ikiwa ni kuonesha upendo na shukurani kwa muda wote alioitumikia tume hio.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Kheriyangu Mgeni Khamis aliteuliwa mwaka 2013 kuitumikia tume hio hadi April 2021 ambapo anakwenda kuendelea na majukumu mengine ya kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.