Habari za Punde

ZRB yaja na mbinu ya kidigital ukusanyaji Mapato

  

Muarubaini wa upotevu wa mapato ya Zanzibar umepatikana, baada ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kujiandaa kisasa zaidi kwa kuja na mfumo maalum wa ukusanyaji mapato kwa walipa kodi kwa kutumia njia ya kidigital.

 

Mfumo huo ambao hivi sasa upo katika majaribio kwa takriban kwa wafanyabishara 130 visiwani Zanzibar, unatajwa kuwa ni mageuzi makubwa katika ongezeko la kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliofikia kiwango cha kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi.

 

Meneja Uhusiano na huduma kwa mlipa kodi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Shaaban Yahya Ramadhan akizungumza na Mwandishi wa Makala haya amesema majaribio ya mfumo huo wa ukusanyaji wa kodi kwa mashine za kidigital, yameanza kuonesha mafanikio.

 

Alisema katika kipindi cha February 2021 kipindi ambacho mfumo huo umo katika majaribio, Bodi imeweza kukusanya zaidi ya shilling 51 bilion ikiwa ni zaidi ya asilimia 100 ya makadirio ya sh 45 bilion ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.

 

“Hali hii inaonesha wazi kwamba pindi tukifanikiwa kuutumia mfumo huu tutaweza kupiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapati ya serikali, hatimae upelekaji wa huduma za kijamii kwa wananchi utaweza kufanyika kwa kiwango kikubwa kutokana na pato letu kuongezeka”alisema Yahya.

 

Yahya amesema mashine hizo ambazo zinatarajiwa kutumika katika ukusanyaji wa kodi, zitakuwa na uwezo wa hali juu,kutokana na mfumo wake utaunganishwa moja kwa moja na mfumo wa ZRB, ambapo mfanyabishara atakuwa hawezi kudanganya hata kidogo.

 

Alisema kila kitakachofanywa kupitia mashine hizo kitaonekana na ZBR kuanzia utoaji wa risiti, viwango vya mauzo, muda wa kutumika mashine, nani amepewa mashine, nani anatumia nani haitumi, hivyo ni wazi kwamba ile mianya yote ya upotevu wa mapato itaondoka.

 

“Lazima tukiri kwamba jambo lote kuingia sehemu linataka utaalam kiundani kabisa ndio maana tumeanza kutoa mashine 130, kwa ajili ya kuangalia kasoro zitakazojitokeza hatimae tuchukue hatua za maboresho kabla ya kupewa wafanyabishara wote”alisema.

 

Yahya amesema kwa kuwa suala hilo ni la kisera hivi sasa Serikali ipo katika maandalizi ya sera za matumizi ya mashine hizo, ambazo zinatarajiwa kuanza katika  mwaka wa fedha 2021-2022 pindi taratibu zote zitakapokamilika.

 

Alisema serikali itakapokamilisha tu taratibu hizo, mashine hizo watapatiwa zaidi ya wafanyabiashar 7,000 waliosajiliwa na ZRB   ili kuanza matumizi, huku akisisitiza kabla ya matumizi watapatiwa mafunzo maalum.

 


Hata hivyo ifamike kwamba (ZRB) ni taasisi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ilianzishwa chini ya sheria Namba 7 ya mwaka 1996 kuwa ni taasisi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na vianzio vya ndani ya nchi.

 

ZRB inasimamia kodi ya Ongezeko la thamani (VAT), ushuru wa Hotel na nyumba za kulaza wageni, ushuru wa mikahawa na kutembeza wageni, kodi ya ushuru wa stempu (stamp duty), ushuru wa bidhaa za mafuta na nishati.

 

Kodi nyengine ni kodi ya miundo mbinu, ada za bandari lakini pia ZRB imepewa uwakala wa kusimamia na kukusanya ada mbali mbali kama kodi ya ardhi, ada za usajili wa vyombo vya moto, ada za leseni za njia na leseni za udereva na ada ya usafiri wa anga.

 

Hata hivyo Yahya amesema moja ya mafanikio ya ZRB ni kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbali mbali zilivyelezwa na Sheria No 5 ya usimamizi wa kodi, ambayo inaeleza kuwa kila mfanyabishara aliyefikia mtaji wa sh milion 2, ana wajibu wa kulipa kodi.

 

Amesema takwim zinaonesha kwamba mwaka 2017-2018 ZRB imekusanya shilling 410.34 bilion sawa na asilimia 103 ya makadirio ya ukusanyaji wa shilling 396.24 bilion, mwaka 2018-2019 ZRB wamekusanya shilling 438.33 bilion sawa na asilimia 90.35 ya makadirio ya ukusanyaji wa shilling 485.16 bilion.

 

Mwaka 2019-2020 ZRB imekusanya shilling 486.75 sawa na asilimia 80.41 bilionya makadirio ya ukusanyaji wa shilling 605.23 bilion, kiwango ambacho kinadaiwa kupungua ikichangiwa na maradhi ya korona.

 

“Hata hivyo kuanzia mwezi Julai 2020 hadi Feberuary 2021, ZRB tumekuwanya shilling 251 bilion ikiwa ni sawa na makadirio ya ukusanyaji wa shilling 441 bilion, kushuka huku pia kumechagiwa na maradhi ya korona, ila kwa sasa hali inaonekana kuwa nzuri, tunatarajiwa mapato kuongezeka”alisema.

 

Yahya amesema mafanikio mengine, ZRB imefanikiwa kutoa elimu ya mlipa kodi kwa kuwafikia Wafanyabishara mbali mbali pamoja na wananchi Mjini na Vijijini, hatua ambayo alidai kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ukusanyaji w akodi kila mwezi.

 

“Tunaamini elimu tuliyotoa pamoja na elimu inayotolewa na Rais wetu, Dk Husein Ali Mwinyi juu ya umuhimu wa suala la kulipa kodi itasaidia kwa kiasi kikubwa makusanyo kuongezeka siku hadi siku”alisema.

 

Alisema malengo ya ZRB ni kuona kwamba kila mfanyabishara na wananchi wanatambua umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari bila shuruti, akisisitiza kwamba kufanya hivyo ni kuisaidia serikali kufikia malengo ya utoaji wa huduma kwa jamii.

 

“Lakini mafanikio mengine sisi ZRB na TRA sasa tumekuwa tunawasiliana vyema katika utendaji wa kazi zetu, mfano tukitoa elimu ya mlipa kodi sote huwa mahala pamoja, hili linasaidia sana kuwatoa hofu walipa kodi wetu juu ya uwepo wa taasisi hizi mbili za mapato”alisema.

 

Katika kuhakikisha kuongezeka kasi ya uwajibikaji  serikali ilipunguza baadhi ya viwango vya kutozea kodi ikiwemo, kupunguza kiwango cha kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 15, sambamba na kupunguza kiwango cha ushuru wa hoteli kutoka kiwango cha asilimia 18 hadi asilimia 12.

 

Changamoto

 

Miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni pamoja na ukusayaji wa kodi kwa njia ya risiti za karatasi hasa katika baadhi ya maeneo ikiwamo Hoteli za kitalii.

 

Alisema katika Hoteli hiyo ZRB inakosa idadi kamili ya wageni wanahudumiwa na Hoteli hizo kwa kila siku, pamoja na kujua idadi ya siku wanazolala katika Hoteli hizo.

 

“Kwa kweli mfumo huo ni mgumu sana hivyo tunadhani kwamba muarubaini wa hayo ni kuja kwa mfumo wa Kidigital ambao utakuwa na uwezo wa kujua kila kitu”alisema.

 

Viongozi wadau waeleza

 

Rais wa Zanzibar, Dk Husein Ali Mwinyi ni namba moja kati ya viongozi wakuu wa Serikali wanaelezea umuhimu wa kulipa kodi pamoja na athari zake kwa taifa, ambapo moja katika hotba zake alisema bila ya ukusanyaji wa kodi nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo.

 

Dk Mwinyi alisema yeye si muumuni wa kodi kubwa, hivyo atahakikisha hakuna kuongezeka kwa kodi, badala yake wataangalia njia ya kushusha viwango vya kodi, ili kila mmoja aweze kulipa kodi kwa hiyari.

 

“Niwaombe wananchi watambue kuwa huduma za kijamii, kama vile elimu, Afya, maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu na mambo mengine mengi yanayofanywa na Serikali yanategemea fedha zitokanazo na kodi, hivyo tujitahidi kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili malengo yetu hayo yameweze kufanikiwa”alisema.

 

Waziri wa nchi, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed ameataka wasimamizi wa ukusanyaji wa mapato kuhakikisha wanasimamia vyema zoezi hilo ili kuona hakuna uvujaji wa mapato ya Serikali.

 

Alisema suala hilo linawezekana pindi watendaji hao wa Serikali wakafuata taratibu ziliopo katika ukusnayaji wa mapato hayo, ambayo ni msingi wa kufikia maendeleo nchini.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watembeza watalii, Seif Mirskry ameiomba kutofikiria kuongeza viwango vya kodi na kusema huu ni wakati wa wafanyabiashara kupata tahfifu kutokana na athari ya gonjwa wa Covid-19 ulioikumba Dunia.

 

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara sekta binafsi Mkurugenzi Mtendaji kutoka MD-QBC Khamis Ali Said amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni hali iliopo hivi sasa ambapo hakuna utaratibu wa kurudishiana kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

 

Alisema   kuna umuhimu kwa serikali zote mbili kukaa pamoja na kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo kwa msingi kuwa lina athari kubwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

 

“Kwa kweli kuja kwa mfumo wa ulipaji kodi kwa njia ya mashine ni mzuri, ila tunaiomba serikali nayo kutupunguzia kiwango cha kodi ili nasi tufaidike na serikali ifaidike pia”walisema baadhi ya wafanyabiashara ambao wameanza kutumia mashine kwa majaribio.

 

Makala hii imeandaliwa na Haji M. Moh'd

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.