Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuwachukulia Hatua kwa Watumishi waliotia Dosari Miradi ya Maendeleo.

Na Hamida Kamchalla, Tanga.

MKUU wa mkoa wa Tanga Adam Malima  amesema ofisi yake itajipanga kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kufuatia dosari zilizojitokeza kwenye miradi ambayo imekataliwa na kutokuzinduliwa wakati wa kukimbiza mwenge wa uhuru mkoani humo.

Malima aliyasema hayo juzi wakati akikabidhi mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Steven Kagaigai katika wilaya ya Same ambapo alibainisha kuwachukulia hatua watumishi waliosababisha hizo ikiwa ni pamoja na kurekebisha miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi.

Aidha alimuomba kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa Josephine Mwambashi kutokuwa na shaka kuhusu kuwachukulia hatua  watumishi hao huku akimuhakikishia kutimiza jambo hilo.

"Hata hivyo miradi mitano haikufunguliwa na mwenge wa uhuru kutokana na sababu mbalimbali zilizobainika, ofisi yangu imejipanga kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria kwa wale wote waliosababisha dosari hizo" alisema.

"Hivyo basi, naomba nimuhakkishie kiongozi wa mbio hizi kwa mwaka 2020/21 kuwa asiwe na wasiwasi kuhusu kuwachukulia hatua watumishi wote waliosababisha dosari alizoziona kwenye miradi hiyo, lakini pia jambo kubwa ni kuirekebisha ili iwatumikie wananchi na kutimiza lengo lililokusudiwa" aliongeza.

Awali akiukabidhi mwenge huo, Malima alifafanua kwamba, umekimbizwa katika mkoa huo umbali wa kilomita 1197 ambapo kiongozi wa mbio hizo na enzake watano walitembelea, kuzindua na kuweka mawe ya misingi katika miradi sitini na saba iliyogharimu kiasi cha zaidi ya sh bilioni kumi na nne.

Hata hivyo alitoa mchanganuo wa fedha hizo kuwa ni pamoja na nguvu za wananchi sh milioni mia mbili na ishirini na tatu, halmshauri za wilaya sh milioni mia saba na sitini na mbili, serikali kuu sh bilioni kumi na moja na milioni mia tano na wafadhili sh bilioni moja na milioni mia nane na thelathini na saba.

Wilaya tatu ambazo miradi yake imekataliwa na mwenge ni pamoja na Muheza mradi wa barabara, Kilindi mradi wa maji na Lushoto mradi wa mabweni huku wilayani Tanga kukiwa na mradi wa barabara ambao unahitajika kufanyiwa marekebisho madogomdogo

Mwenge wa uhuru ulipokelewa mkoani Tanga mwezi mei, 28 ukitokea Visiwani katika mkoa wa Kaskazini Pemba na kukabidhiwa na mkuu wa mkoa Salama Mbarouk Khatib ambapo umekimbizwa ndani ya wilaya nane za mkoa huu hadi juni 5 ulipokabidhiwa kwa  mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.