Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuendelea Kuimarisha Amani kwa Azma ya Kuleta Maendeleo Nchini -Alhaj Dk.Hussein Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Kijiji Bwejuu baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa ilifanyika katika Masjid Jamaa Bwejuu Wilaya ya Kusini Unguja. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuendelea kuimarisha amani kwa azma ya kuleta maendeleo nchini.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Ijumaa Bwejuu, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba maendeleo hayawezi kupatikana nchini kama hakuna amani.

Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka wananchi kutokubali amani iliyopo kuondoka kwani hakuna haja ya kuona amani iliyopo inatoweka kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Aliongeza kuwa zipo nchi ambazo amani imepotea na ni mfano tosha wa kuthibitisha kwamba amani ina umuhimu mkubwa wakati wote  kwani inapotoweka hakuna shughuli yoyote inayoweza kufanyika zikiwemo zile za maendeleo na hata ibada.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba wananchi wote kwa pamoja wana jukumu kubwa la kuilinda na kuidumisha amani iliyopo ili sitoweke.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kwa kila mmoja kwa nafasi aliyonayo kuendelea kumuombea dua ili aweze kuongoza kwa haki sambamba na kuweza kutekeleza dhamira yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Mwinyi Mabrouk alieleza haja kwa wananchi wote kuendeleza amani, umoja na mshikamano.

Alieleza kwamba suala la umoja na mshikamano limepewa msisitizo mkubwa katika Qur-an tukufu pamoja na hadithi za Mtume Mohammad (S.A.W) hivyo, waumini wote wana wajibu wa kudumisha na kuendeleza amani na umoja miongoni mwao.

Sambamba na hayo waumini wa msikiti huo walieleza kufarajika kwao kwa uwamuzi wa Alhaj Dk. Mwinyi wa kwenda kusali nao pamoja sala ya Ijumaa katika msikiti wao hii leo.

Katika maelezo yao, waumini hao walieleza kuridhika na juhudi kubwa za kuwaletea maendeleo zinazochukuliwa na Alhaj Dk. Mwinyi na kuahidi kuendelea kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu ampe nguvu zaidi za kutekeleza majukumu yake.

Mara baada ya sala hiyo ya Ijumaa Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na ndugu, jamaa na marafiki katika msiba wa Bi Zainab Makame Pandu, dada wa Mzee Mussa Makame Pandu maarufu Dere hapo hapo kijijini kwao Bwejuu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.