Na Munir Shemweta, SUMBAWANGA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa agizo kwa kila halmashauri nchini kutoa hati zisizopungua mia moja kwa kila mwezi.
Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Rukwa tarehe 19 Julai 2021 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi sekta ya ardhi nchini, Dkt Mabula alisema halmashauri kupitia idara zao za ardhi zinatakiwa kuandaa hati zisizopungua mia moja kwa mwezi katika yale maeneo ambayo viwanja vyake vimepimwa.
‘’kule ambako viwanja havijapimwa watendaji wake wanaweza kueleweka lakini mtu ana viwanja mia moja halafu anashindwa hati za idadi hiyo na wakati mwingine anatoa hati kumi tu huku akiwa amejiwekea lengo la kutoa hati mia moja’’ alisema Naibu Waziri wa Ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, hatimiliki za ardhi zisipotoka na kumilikisha kwa wamiliki wa ardhi migogoro haitaisha na matokeo yake ni kuwepo umilikishaji mara mbili (Double allocation).
Alimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Rukwa Swagile Mfinanga kumpatia taarifa ya uandaaji hati kwa kila halmashauri yake kufikia mwisho wa mwezi wa nane na kusisitiza kuwa, hatu hiyo pia itafika mikoa yote kwa kuangalia idadi ya viwanja vingapi vimepimwa na wamiliki wangapi wameomba lakini hawajapatiwa na kama hawajaomba mara ngapi watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri husika wamekwenda kuahamasisha ili wamiliki waombe kupatiwa hati.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aligawa Ankara za malipo ya kumilikishwa ardhi kwa baadhi ya wananchi wapatao 593 waliopimiwa maeneo yao katika kata ya Momoka Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwaambia wakazi wa kata ya Momoka katika manispaa ya Sumbawanga kuwa, wamefanya jambo zuri la kukubali kupimiwa maeneo yao ili baadaye waweze kumilikishwa na Wizara ya Ardhi inawaunga mkono kwa kuwa uamuzi waliofanya utawasaidia kuepukana na migogoro ya mipaka na wakati huo kutumia hati watakazopata katika shughuli za maendeleo kama vile kuchukulia mikopo benki.
No comments:
Post a Comment