Habari za Punde

Mh Hemed azindua rasmi mpango wa chanjo ya kutokomeza Kipindupindu Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wananchi waliohudhuria katika uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Kipindupindu uliofanyika katika Viwanja vya Magirisi Meli Nnne Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

 Mhe. Hemed akiwa Pamoja na Mhe. Omar Said Shaaban kwa niaba ya Waziri wa Afya na Muwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani Dk. Tigest Ketesela Mengestu akizindua rasmi mpango wa Chanjo ya Kutomeza Kipindupindu Zanzibar.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezitaka Taasisi zenye dhamana ya utekelezaji wa mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar kusimamia wajibu wao kwa kutekeleza miongozo na mikakati ya kutokmeza maradhi hayo.

Mhe. Hemed alieleza hayo katika hafla maalum ya uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya kupindupindu iliyofanyika katika Viwanja vya magirisi melinne wilaya ya Magharib “B” Unguja.

Alisema serekali imeamua kutekeleza mpango huo wa chanjo katika shehia Hamsini na nane(58)zilizomo katika wilaya (09) kati ya wilaya kumi na moja (11) Unguja na Pemba.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais aliwataka wananchi waliolengwa na mpango huo kupitia shehia zao kujitokeza kwa wingi katika zoezi liloanza hivi karibuni.

Alifafanua kuwa,utekelezaji wa mpango huo wa chanjo ni moja kati ya mikakati mikuu ya Serekali ili kufikia lengo lake la kuhakikisha Zanzibar inaondokana na Maradhi ya kipindupindu kwa asilmia mia moja ifikapo mwaka 2028.

“Serekali kupitia ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mashirikiano na wadau wa Taasisi mbalimbali imetayarisha mpango maalum wa kutokomeza maradhi ya kipindupindu hapa Zanzibar ifikapo mwaka 2028”Alisema Mhe.Hemed

Alisema,taarifa zinaonyesha kuwa, mpango wa utekelezaji huo umekua ukitumika katika kuondoa Maradhi hayo akitolea mfano Nchi zilizowahi kutumia chanjo hiyo Ikiwemo Uganda,Msumbiji,Sudan, Indonesia pamoja na Haiti.

Makamu wa Pili wa Rais alibainisha kwamba,uzoefu unaonesha maradhi ya kipindupindu huenea katika maeneo mengi kutokana na Miundombinu dhaifu, matumizi madogo ya vyoo,kuzagaa kwa uchafu unaopelekea kuchafua vyanzo vya maji na chakula.

“Kutolewa kwa chanjo hii haina maana tuache kudumisha usafi, kwani usafi ndio njia pekee ya kuepukana na maradhi mbalimbali yakiwemo ya mripuko”Alisema Makamu wa Pili.

Pamoja na mambo mengine,Mhe.Hemed alisema tafiti tofauti zinaonyesha kuwa,chanjo za aina hii zinapotolewa katika mazingira ya nchi zetu inauwezo wa kulinda jamii dhidi ya kipindupindu kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano.

Aliwahakishia wananchi kwamba,chanjo hiyo inayotolewa na serekali ni salama kwani imethibitshwa ulimwenguni pamoja na Taasisi za Afya zilizopo hapa nchini.

Mhe. Hemed aliitaka jamii Iliolengwa na mpango huo kuhakikisha inapata dozi zote mbili za chanjo kwa zaidi 90%ili kuzuia kutokea tena kwa miripuko ya kipindupindu hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa,serekali imekuwa ikitumia gharama ya kutibu athari zitokanazo na maradhi hivyo,ameitaka jamii na wananchi kwa ujumla kuitikia wito wa serekali kwa kuwapeleka watoto pamoja na wahusika wote kupata chanjo hiyo.

Akimuwakilisha Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watot Mhe. Omar Said Shaaban alisema kufanyika kwa zoezi hilo la chanjo Zanzibar ni muendelezo katika kuwakinga wananchi wake ambapo wadau mbali mbali wamekuwa wakijitokeza kuunga mkono jitihada hizo za serikali.

Mhe. Omar alisema kuwa kadri ya watu wanavyozidi kuchanjwa ndio huongeza ufanisi katika suala zima la kuwakinga watu wake jambo ambalo linaipunguzia jukumu serikali ya kutumia nguvu kubwa katika kutibu watu wake.

“Zanzibar ina historia kubwa katika utekelezaji wa chanjo mbali mbali na kupata mafanikio, Hivyo nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupata chanjo hii” Alisema Mhe. Omar

 

Nae, Mkurugenzi Mkuu kutoka wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia, na watoto Abdalla Suleiman Ali alieleza kuwa utoaji wa chanjo ya kipindupindu sio jambo geni kutolewa Zanzibar kwani zoezi kama hilo limefanyika mwaka 2009 na mwaka 2010 kwa lengo la kuiihifadhi jamii kutokana na athari zinazosababishwa na maradhi hayo.

Alisema zoezi hilo ambalo limezinduliwa rasmi Julai 04 mwaka huu litafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza limeanza kuanzia Julai 03 hadi Julai 07 na awamu ya pili itanmza Julai 31 mwaka huu hadi kufikia Agosti 04 Mwaka huu.

Akitoa Salamu za Shirika la Afya Duniani (WHO) Mwakilishi Mkaazi anaefanyia kazi zake nchini Tanzania Dk. Tigest Ketesela Mengestu aliipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua nzuri inayoendelea kuzichukua  katika kuwalinda watu wake dhidi ya maradhi mbali mbali.

Alisema Maradhi ya Kipindupindu yamekuwa yakiathiri watu takribani Millioni Moja Nukta Tatu (1.3) mpaka Millioni Nne duniani kila mwaka hivyo, Shirika la Afya duniani limeamua kuja na mpango huo wa kutekeleza Chanjo ili kuinusuru jamii ya watu wengi wanaoathiriwa na Maradhi hayo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.