Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, Amewasimamisha Kazi Wakurugenzi Wote wa Halmashauri za Wilaya Unguja.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake wa majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasimamisha kazi  Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya za Unguja  na baadhi ya Wakurugenzi wa Taasisi na Idara za Serikali, pamoja na Watendaji wote watakaobainika kuhusika  katika matukio ya Wizi, kutowajibika na Ubadhirifu wamali za Serikali.

Dk. Mwinyi amewasimamisha kazi Watendaji hao katika Mkutano wa Majumuisho uliofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakili, Kikwajuni Jijiji Zanzibar, baada ya kukamilishaziara yake katika Mikoa mitatu ya Unguja, ambapo alitembelea na kukagua Miradi mbali mbali ya Maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili  wananchi .

Akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Chama (CCM) na Serikali, Dk, Mwinyi alisema amewasimamishwa kazi Wakurugenzi , Watendaji na wafanyakazi kwa kuhusika na Vitendo vya wizi, kutowajibika katika dhamana zao pamoja na Ubadhirifu wa mali za Serikali.

Aliwataja waliohusika na kadhia hiyo kuwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mjini, Magharibi A na B, Kaskazini A na B, Kusini , Wilaya Kati pamoja na Mkurugenzi wa SMIDA.                                                                                                                    

Akizungumzia juu ya ziara aliyofanya katika Mikoa mitatu ya Unguja, Dk. Mwinyi  aliwataka watendaji kubadilika kw akigezo cha kuwepo changamoto mbali mbali hususan katika sekta za kijamii na utoaji huduma, huku baadhi ya changamoto hizo zikisababishwa na ukosefu wa fedha na nyingine zikitokana na  utendaji usioridhisha.

Alisema kumekuwa na Mikataba mingi ya kifisadi inayofanyika katika baadhi ya Halmashauri za Wilaya (ikiwemo Mjini, Kaskazini A na B), na akatoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya Mjini inayoingia mikataba ya aina hiyo na  Kampuni za Simu pamoja na kuingia mikataba katika Uwekaji wa Mabango.

Alisema kumkuwepo ukusanyaji duni wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya Mjini,  kiasi cha Wilaya hiyo kufanana na Halmashauri  zilioko Vijijini.

Aidha, Dk. Mwinyi alieleza hali mbaya inayoikabili sekta ya Afya nchini, na kusema haridhishwi na utendaji kazi wa Wizara  ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, kwa kukosa miundombinu bora, kutokuwa na vitendea kazi , kushindwa kutoa huduma muhimu na hivyo wananchi kukosa huduma sahihi.

Aliiagiza Wizara hiyo kuwa na mipango maalum ya kupata fedha pamoja na kuzitumia vizuri fedha hizo, huku akibainisha Wizara hiyo kuwa na vyanzo mbali mbali vya kuingiza mapato.

Alisema kwamuda mrefu sasa Serikali imekuja na wazo la kuwa na mpango wa Bima ya Afya, lakini kwakipindi chote hicho hakunakitu  kilichofanyika.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wa Idara ya Tiba, Idara ya Kinga pamoja na Idara ya Rasilimali watu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha, akaiagiza Taasisi ya Kupambana Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) pamoja na Jeshi la Polisi kuchunguza suala la Wizi wa Fedha za Shirika la Umeme (ZECO) katika vituo vya Shirika hilo, huku akitaka hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika na kadhia hiyo.

Sambamba na hilo, Dk.  Mwinyi akaagiza kusimamishwa kazi wafanyakazi waliohusika na ung’oaji wa nguzo za umeme katika eneo la Mwachealale.

Rais Dk. Mwinyi aliikumbusha  ZECO wajibu wake wa kupeleka nguzo za umeme pamoja Transfoma katika shughuli za kuwaungia umeme wananchi, “ ZECO wajibu wa kupeleka nguzo za umeme na Transfoma ubaki kwenu, …….suala la ada nalo liitazamwe upya”, alisema.

Akigusia sekta ya Ujasiriamali, Dk. Mwinyi aliagiza Mifuko yote ya Uwekezajiiliopo nchiniiunganishwe (ukiwemo Mfuko waUwezeshaji wananachi kiuchumi, Mfuko wa Walemavu, Vijana , SMIDA n.k), kwa vile haijafanya kazi ipasavyo, kwani fedha zimekuwa zikitolewa ovyo na bila hesabu, pamojana kutokuwepo marejesho.

Aidha, akaitaka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuwawezesha wajasiriamali, huku akitaka fedha zitumike vizuri, na akatoa mfano wa matumizi mabaya ya fedha kwa SMIDA, ambao katika kipindi cha mwaka mzima iliwawezesha wananchi 27 pekee kutoka mtaji wa shilingi Bilioni mbili.

Dk. Mwinyi akatumia fursa hiyo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa taasisi hiyo (SMIDA).

Katika hatua nyengine, Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyi, akazungumzia suala la Usafi katika Jiji la Zanzibar, na kusema ni eneo la Barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kiamatifa wa Abeid Amani Karume kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja pekee, ndio inayosafishwa kwa vile yeye amekuwa akitumia kuelekea Ikulu.

“Hakuna eneo lolote lililo safi zaidi ya ile ya Airport ambayo inasafishwa kwa vile mimi napita”, alisema.

Alisema asilimia tisini (90%) ya fedha za Mradi wa(ZUSP) ambazo ni Dola Milioni 90, zimetengwa kwa ajili ya kupendezesha Mji, lakini hakuna matunzo ya miti iliyopandwa, mbali na fedha nyingi kutumika kwa ajili kuilipa Kampuni ya Usafi

Alisema Serikali inakusudia kuja na mradi maalum wa kupendezesha Mji kwa kuwana barabara zenye Lami, maeneo ya waenda kwa miguu pamoja na mambo mbali mbali, huku jukumu la kusimamia usafi likiwa chini ya usimamizi wa Manispaa.

Alieleza kuwa hadi leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za ujenzi wa masoko au Vituo vya Mabasi na kusema Manispaa imejikita katika mikataba ya ovyo.

Kuhusiana na sekta ya Ardhi na makaazi, Dk. Mwinyi alieleza kuwepo migogoro mbali mbali katika maeneo aliyoyatembelea, na kusema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi imejikita katika utauzi wa migogoro, badala ya kuja na mipango mipya ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliahidi kuunda Tume itakayokuwa na wajibu wa kupitia migogoro yote ya Ardhi na hivyo Wizara kubakia na jukumu la kuendeleza makaazi mapya kwa wananchi.

Alisema watendaji wote watakaobainika kuhusika au kuwa chanzo cha migogoro hiyo, Tume itakayoundwa itawachukuliwa hatua.

Aidha, akazungumzia sekta za Udhalilishaji wa Kijinsia pamoja na Upatikanaji wa  Dawa la Kulevya  na kuzitupia lawama Mamlaka zinazohusika kwa kutokuchukua hatua zozote za msingi  katika kukabiliana na jambo hilo.

Alivitaka vyombo vya Ulinzi na usalama pamoja na wadau kushirikiana kuondoa udhalilishaji nchini, sambamba na kuagiza Watuhumiwa wote wa makosa hayo kuwekwa ndani.

Alisema vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na watoto unaanzia kwenye jamii (skuli, madrasa), hivyo akaitaka jamii kuondokana na muhali.

Akigusia Dawa za Kulevya, alisema mihadharati hiyo imekuwa ikiingia nchini kupitia njia za Banadari na Uwanaj wa Ndege na kubainisha uwepo wa baadhi ya watendaji wanaoshirikiana na wahalifu kupitisha dawa hizo na kuleta athari kubwa kwa vijana, ambapo wengi wao hujiingiza katika vitendo vya wizi.

“Vyombo vya Ulinzi na Usalama wawe wakali, tunataka kusikia katika vyombowatu wanafungwa”, alisema.

Kuhusiana na sekta ya Elimu, Dk. Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali kuja na mpango utakaobainisha mahitaji yote ya kitaalamu, ili Serikali iweze kujenga madarasa ya kutosha , sambamba na kuainisha ukosefu wa walimu uliopo, hususan katika masomo ya sayansi, jambo linalosababisha wanafunzi kushindwa kufaulu.

Alisema pamoja na kujenga madarasa na mahitaji mengine ya kitaaluma kama vile vyoo na  maabara lakini pia itatoa mwanga wa kuboresha maslahi ya  walimu, ili kuimarisha kiwango cha elimu nchini.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi akatumia fursa hiyo kuelezea aliyoyabaini katika sekta ya Barabara pamoja na kuelezea mipango ya Serikali katika ujenzi wabarabara za ndani kilomita 220 kwa kiwango cha Lamipamoja  barabara kuu (km 220), zikiwemo zile zinazohusu  Ilani ya CCM.

Alisema ili kuokoa fedha, Serikali imeamua kuchukua mikopo na kujenga barabara hizo, hivyo tozo zitatumika kulipia mikopo hiyo.

Akigusia sekta ya Maji, Dk. Mwinyi, alisema bado kuna tatizo kubwala ukosefu wa maji katika maeneo mbali mbali aliyoyatembelea.

Alimpongeza Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Salha Mohamed Kassimkwakuonyesha Dira ya kuleta mabadiliko, akionya uwepo wabaadhi ya watendaji wasio na azma ya kubadilika katika Mamlaka hiyo.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuiagiza ZAECA kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watendaji wote waliohusika na Tenda ya Vifaa ‘dhaifu’, kwani mazingira yanaonyesha kuwepo viashiria vya rushwa katika kadhia hiyo.

Aidha, akaliagiza Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kufuatilia na kuwafikisha Mahakamani wafanyakazi wote waliohusika na Wizi wa Mabomba ya ZAWA.

Aliutaka Uongozi wa ZAWA kusimamia kwa umakini mkubwa maendeleo ya Mradi wa maji wa Exim Bank ambao utawanufaisha wananchi waWilaya za Magharibi A na B pamoja Wilaya ya Katina kuwataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha Mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.

Mapema. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akavishukuru Vyombo vya ulinzi na Usalama kwakazi kubwa ya kudumisha amani  na usalama pamoja na kuwataka wananchi kuendeleza amani iliopo.

Aliwataka Viongozi wa Mikoa pamoja na Vyombo vya Ulinzi kuwaelimisha  wananchi (wavuvi) juu ya matumizi ya zana sahihi zinazohitajika katika shughuli zao, na akabainisha umuhimu wa vyombo hivyo kutumia zaidi busara badala ya nguvu pale kasoro zinapojitokeza.

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa, alitoa nenola shukurani na  kuwashukuru Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo pamoja na watendaji  wa Mkoa huo kwamashirikiano makubwa yaliofanikisha kukamilika ziara hiyio kwa ufanisi mkubwa.

Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwsenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mmwinyi alipata fursa ya kuangalia mfano wa  Mji mpya wa Kilimani , unaolengwa kuwa mlango wa Jiji la Zanzibar, ambapo  unahusisha matumizi ya eneo la makaazi ya wastani wa Square metre 2,000,700. 

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.