Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekizindua Kitabu cha Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Obasanjo cha "Asian Aspiration" Katika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar.

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akionesha Kitabu cha Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Obasanjo cha  “Asian Aspiration“ baada ya kukizindua rasmin leo katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe Olusegun Obasanjo na (kushoto kwa Rais) Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizindua Kitabu cha Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Obasanjo “Asian Aspiration“ uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe Olusegun Obasanjo na (kushoto kwa Rais) Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezindua kitabu cha  “The Asian Aspiration – Why and How Africa should Emulate Asia”  na kuwapongeza watunzi wa kitabu hicho, huku  akibainisha kuwa uamuzi wa kukizindua kitabu hicho hapa Zanzibar ni sahihi.

Hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho umefanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar, na kuhudhuriwa na watunzi wa kitabu hicho Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Mchumi Emily Van der Merwe na Mkurugenzi wa Johannesburg based Brenthurst Foundation.

Kitabu cha “The Asian Aspiration – Why and How Africa should Emulate Asia” kimebeba  maudhui juu ya mambo yaliofanywa na Nchi  za Asia na kupelekea kupiga hatua kubwa za maendeleo ya haraka ya Kiuchumi na kisiasa, hatua ambazo nchi za Afrika zinapaswa kuiga ili kupata mafanikio.

Akizungumza na washiriki wa hafla hiyo Dk. Mwinyi aliwapongeza watunzi wa kitabu hicho ambapo miongoni mwao  ni wanasiasa na viongozi wabobezi katika masuala ya sera, uchumi na siasa .

Alisema  kuna mambo mengi ya kujifunza  kutoka katika kitabu hicho, yanayoonyesha kwa kiasi gani Mataifa ya  Bara la Asia yalivyoweza kupambana hadi kutatua changamoto mbali mbali za maendeleo zilizokuwa zikiyakabili na hatimae kupata mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano.

Alisema kitabu hicho kinafunza kwa kiasi gani nchi za Bara la Asia lilivyoweza kiujikwamua kutoka hali ngumu ya kiuchumi na kufikia mafanikio yanayoonekana leo.

Alitoa mfano wa mafanikio ya nchi hizo, alisema  Vietnam iliweza kujikomboa  kutoka hali duni ya kiuchumi mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1980 na  kupata maendeleo ya haraka  kupitia sekta mbali mbali hadi Taifa hilo likaweza kujinasua kutoka Taifa la kipato cha chini   na kuwa Taifa lenye uchumi mkubwa unaolingana na nchi zenye kipato cha juu.

Aidha, alitoa mfano wa Taifa la Japan ambalo lililofanikiwa kujikwamua  baada ya uchumi wake kuharibika kutokana na  Vita vya Pili vya Dunia, kufuatia hatua yake ya  kuweka mkazo katika sekta binafsi, elimu na  ubunifu,   hususan katika masuala ya Teknolojia pamoja na utafutaji wa mitaji kwa njia mbali mbali.

“Leo hii Japan imejikita katika  sekta ya utengenezaji wa magari, yakiwamo kampuni ya Toyota, mzalishaji wa magari ambapo Zanzibar ni watumiaji wakuu”, alisema.

Dk. Mwinyi alisema suala la umoja katika kutafuta maendeleo ni la msingi na linaweza kuinufaisha jamii,  na akatoa mfano wa Taifa la Singapore lililoweza kupata mafanikio makubwa kutokana na msingi huo.

Alisema Taifa hilo chini ya miongozo sahihi ya mwanzilishi wake Lee Kuan Yew’s aliefariki akiwa na umri wa miaka 91, limeweza kupiga hatua za haraka hadi kufikia kuwa taifa lililoendelea.

Rais Dk. Mwinyi alisitiza haja ya Viongozi wa Afrika katika ngazi mbali mbali pamoja na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata nakala ya Kitabu hicho na kukisoma ili hatimae waweze kuitumia taaluma iliomo ndani yake kwa maslahi ya Taifa.

Alitoa shukurani kwa watunzi wa kitabu hicho kwa kuja na wazo la kukitunga, kwa msingi kuwa kimesheheni mambo mengi ya kujifunza kwa Wachumi, watunga sera, watafiti pamoja na wapenzi wa kusoma vitabu vyenye maudhui mbali mbali.

Sambamba na hayo , aliwashukuru watunzi hao kwa kuichagua Zanzibar kuwa mahala pa uzinduzi wa kitabu hicho na  kubainisha kuwa ni mahala sahihi.

Mapema, Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, alimshukuru Rais wa Zanzibar na  Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha uzinduzi huo unafanyika kwa mafanikio.

Katika hotuba yake, Obasanjo alitoa muhtasari wa maudhui ya kitabu hicho  na kubainisha jinsi alivyotumia uzoefu wake wa uongozi wa kuliongoza Taifa la Nigeria, kama kichocheo kilichofanikisha utunzi wa kitabu hicho..

Alizitaka nchi za Afrika kubaini maeneo yenye mapungufu na kuweka  kipaumbele katika kuyafanyia kazi.

Alisema itakuwa vigumu kupata maendeleo bila ya kutatua matatizo halisi yanayokwamisha maendeleo hayo.

Aidha, alizitaka nchi za Afrika kuweka kipaumbele katika sekta ya elimu ,kwa kuelewa kuwa ndio msingi wa maendeleo.

Alisisitiza  umuhimu wa viongozi kukisoma kitabu hicho na kuitumia kikamilifu elimu na maarifa watakayoyapata.

Nae, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn alibainisha kufanyika utafiti wa kutosha katika nchi mbali mbali Barani Asia wakati wa  utunzi wa kitabu hicho, sambamba na kukusanya uzoefu na taaluma walizonazo watunzi kuhusiana na  sera za kisiasa na kiuchumi katika nchi za Afrika  hadi kukamilisha kazi hiyo.

Akizungumza na washiriki wa hafla hiyo, Desalegn alielezea masuala mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi yanayoihusu nchi aliiyoingoza (Ethiopia) wakati alipokuwa Waziri Mkuu na kuhimiza suala la ubunifu na kujiamini kwa Viongozi wa Afrika ili kutekeleza na kutimiza malengo ya Mataifa wanayoyaongoza ili kufikia matarajio ya wananachi.

Aidha, aliwapongeza wachapishaji wa kitabu hicho Hurst Publishers kwa  kufanikisha kazi hiyo muhimu.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.