Habari za Punde

Rc Mkoani Tanga Asisitiza Wananchi Kuchukua Tahadhari dhidi ya Corona.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

Mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe.Adamu Malima amewahimiza wananchi mkoani humo kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona kwa kufuata maagizo yaliyotolewa na wataalamu wa afya badala ya kupuuzia na kupelekea kuleta maambukizi ya ugonjwa huo ambao umerudi kwa kasi kubwa.

Malima aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi eneo la Ngamiani jijini Tanga ambapo alisema wananchi mkoani humo wana tabia ya kupuuzia kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo pamoja na kuhamasishwa juu ya hilo

"Nakuombeni, nawasihi kama ninavyojiangalia mimi mwenyewe, hili gonjwa la corona limerudi tena, nimezungumza jana msikitini, nimezungumza juzi na madiwani lakini bado Tanga tunafanya masihara sana na hili jambo" alisema.

"Nakiombeni sana mkashone barakowa, hili jambo lipo na watu wanaondoka na sasa hivi limekuja kivyakevyake, ukija ukishituka leo kesho unaondoka, hatuogopi kufa maana ndio njia ya kila mtu, ukifa kuna jambo la wiki mbili unasumbua watu na unaambukiza ambao hawakuwa nao, tuchukue tahadhari" aliongeza Malima.

Alisema haipaswi watu kukaa kwenye misongamano na ikibidi wavae barakowa ikiwa ni pamoja na kufuata mashariti yaliyotolewa na wataalamu kutokana na mkoa wa Tanga kuwa njia kuu ya mapitio ya watu wanaotoka mikoa mbalimbali.

"Kubwa zaidi ni kuepuka misongamano, nakuombeni ndugu zangu wa Tanga mkiona misongamano kama hii tunavyokaa hapa ni hatari na tukiwa kama hivi vaeni barakowa, na kama hamuamini muupate muende hospitalini mkaone watu, na mpaka dakika hii Mungu ametunusuru Tanga maambukizi sio sana" alieleza.

"Tanga ndio mapitio wanaotoka Dar es salaam kwenda Mombasa wanapitia Tanga, wanaotoka Mombasa ambako upo wanapitia hapa, wanaotoka bara kwenda visiwani wote wanapitia hapa, nyie mtaamini kwamba tuko salama lakini sio salama kama wenzetu hawako salama hii ni balaa" alibainisha.

Hata hivyo aliwaeleza wananchi kuwa ofisi yake imepanga kutoa uzabuni kwa watu maalumu ambao wenye uwezo wa kukidhi kushona barakowa na kuziuza kwa wananchi kwa garama nafuu na zitadumu kuliko kutumia za muda mfupi ambazo ni garama kubwa.

"Hizi barakowa fitina, unaambiwa utumie ndani ya masaa manne halafu unatupa, kwahiyo tunahimizana kuwa na barakowa za kushona na tunekubaliana kwamba tutawapa zabuni watu maalumu wenye uwezo wa kukidhi kishona barakowa hizi ili waziuze shilingi 2000 na ukivaa unafua unaendelea nayo kuliko hizi za masaa manne" alisema.

"Ndugu zangu hali siyo salama sana, kama tupo tunadunda namna hii Mungu mwingi wa rehema anatupenda sana na ana sababu yake ya kuhakikisha Tanga tuko hivi lakini siyo kwa ujanja wetu, kama mambo yenyewe ndio hivi basi hali ni ngumu, nawaomba hili la kuweka tahadhari ni bora kuliko tiba" alisisitiza Malima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.