Kuna mtu ameniuliza swali gumu 'nini siri ya mafanikio yako?' Maswali magumu hayajibiwi na majibu rahisi. Hivyo basi haya hapa majibu magumu kwa ambae amepea vizuri kifikra na avune katika haya na kwa atakaeona hayaelewi haya majibu basi afanye hayamuhusu.
MAJIBU
Kwanza ni vyema alieuliza swali anapaswa kutoa tafsiri yake ya neno MAFANIKIO maana wengine tafsiri yao ya mafanikio ni kuwa na nyumba nzuri, wengine kuwa na gari nzuri, wengine kuwa na familia nzuri yenye upendo na furaha, na wengine mafanikio kwao ni kuwa wachamungu na waumini bora, lakini wenye upeo wa juu zaidi MAFANIKIO ya kweli ni zaidi ya hayo niliyoyataja hapo juu.
Mafanikio ya kweli yanapatikana kwa KUAMINI, KUKUBALI na KUTEKELEZA yafuatayo:
1. Kuitambua nafasi yako katika ulimwengu. Daima kumbuka kuwa nguvu ile ile iliyoumba nyota, jua, mwezi, dunia na vilivyomo ndani yake ndio nguvu hiyo hiyo iliyokuumba wewe. Nguvu hiyo hiyo inayoziendesha sayari bila kugongana ndio nguvu hiyo hiyo inayoendesha maisha yako ya kila siku. Unachopashwa kukijua na kukitii ni SHERIA YA ULIMWENGU (LAW OF UNIVERSE ) ambayo pia ni UNIVERSAL LAW kwa maana sheria hii inagusa kila kilichomo ulimwenguni ukiwemo na wewe. Kuishi bila kuijua sheria hii ni sawa na mtu aliyekabidhiwa gari bila ya mafunzo yeyote ya sheria za barabarani, mafunzo ya udereva, wala matunzo ya gari hilo. Kwa kutoijua sheria hii ndio maana walio wengi wanajifunzia maisha barabarani, mpaka wanazeeka wanakufa hawajahitimu.
2. Ujitambue kuwa kichwani kwako umebeba Super Computer ambayo haijawahi kutengenezwa ulimwenguni yaani ubongo (brain). Hadi sasa pamoja na uvumbuzi wote wa binaadamu hakuna aliyeweza kutumia alau robo ya uwezo wa hazina hii kubwa tulionayo. Kumbuka kuwa ukubwa wa ubongo wako ni sawa sawa na na ukubwa wa ubongo wa wavumbuzi, wagunduzi, wanasayansi na mabingwa wate unaowajua wewe. Tafauti yenu ni matumizi tu ya hazina hii. Hakikisha unautumia ubongo wako.
3. Kuielewa vyema nadharia ya KIWILIWILI na roho, MWILI na nafsi (BODY and soul, BODY and spirit). Jiulize kuanzia unapoamka kitandani umeufanyia mambo mangapo mwili wako? umeuosha, umepaka mafuta, umeupulizia marashi umeuvisha nguo nzuri, umeupa lishe kutwa mara tatu na kadhalika. Kisha jiulize tokea umebanduka kitandani umeifanyia nini ROHO (soul) au NAFSI (spirit) yako? hapo utapata jibu kwa nini mwili wako mkubwa lakini fikra duni. Kwa sababu NAFSI za waliowengi hazilishwi ipasavyo zimepata utapiamlo na kudumaa. Ni ugonjwa sugu katika jamii yetu. Usishangae kuona watuwazima wengi wanafanya mambo ya kitoto. Hakikisha unaitunza na kuilisha NAFSI yako kila siku kwa
ELIMU YA KWELI NA YENYE MANUFAA.
4. Tambua vyema mahusiano ya MWILI wako na DUNIA. Miili yetu mahali pake duniani, ardhini ndipo tunapotokana napo na ndipo miili yetu itapoishia. Kumbuka kuwa kila madini yaliyomo katika miili yetu yanapatikana ardhini na kila tunachokula asili yake adhini. Hata asilimia ya maji yaliyopo duniani kulinganisha na asilimia ya ardhi kavu iko sawa na asilimia ya maji katika mwili wa mwanadamu ukilinganisha na madini mengine yaliyomo mwilini. Duniani hapa ndio kwetu kwa ajili yetu. Hali ya hewa muafaka na uwiano wa oxygen na carbon dioxide upo vyema. Hapa ndio nyumbani nje ya hapa tutahitaji msaada wa kupumua. Heshimu na yatunze mazingira kwani wewe ni sehemu ya dunia.
5. Tambua na UAMINI juu ya mahusiano yaliopo kati ya NAFSI (spirit) au ROHO (soul) na ULIMWENGU (THE UNIVERSE). Uelewe kuwa ndani ya SHERIA YA ULIMWENGU (LAW OF UNIVERSE) kuna SHERIA YA MVUTO (LAW OF ATTRACTION). Kwa mujibu wa sheria hii, nguvu ya ULIMWENGU inawasiliana na wewe kupitia FIKRA zako. Chochote unachowaza NGUVU YA ULIMWENGU inatambua kuwa ndicho unachokitaka. NGUVU YA ULIMWENGU haitambui kizuri ua kibaya kwa sababu hakuna kitu kizuri au kibaya, ni tafsiri zetu zinazotokana na malezi mafunzo, imani za dini na uzoefu wetu ndio unaotufanya tutafsiri mambo kuwa mazuri au mabaya. Hivyo basi unachokiwaza ndicho kinachotokea ULIMWENGU hauna ukomo kadhalika na mali, furaha, taalumana upendo wa ULIMWENGU hauna ukomo. Utakachowaza ndicho utakacholetewa. Unakumbuka ule usemi "Akiwazacho Mjinga ndicho kitakachomtokea" hiyo ndio maana yake. Hivyo basi waza mawazo chanya (positive) saa zote na epuka kuwaza mawazo ghasi (negative). Waza unayoyapenda na yatakayokuletea furaha na yatatokea kadhalika na kinyume chake. Unakumbuka zile aya 'Ombeni nitakupeni' na 'Gonga utafunguliwa'? hiyo ndio maana yake halisi.
6. Kuwa mwema, muadilifu na mwenye SHUKURANI. Hakikisha unashukuru kwa dhati kwa kila neema uliyonayo na unayoipata. Waombe RADHI unaowakosea na wasamehe wanaokukosea.
Hiyo ndio siri ya MAFANIKIO yangu. Nakukabidhi KHATIMA ya maisha yako. Chagua unavyotaka kuishi. Kumbuka kuwa hakuna kitu kinachoitwa BAHATI, 'Bahati ni pale fursa inapokutana na maandalizi (Lucky is when opportunity meet preparation). Huo ndio ufunguo wa MAFANIKIO ya kweli. Mwenye dhamira ya kweli na autumie. Asanteni sana
No comments:
Post a Comment