Habari za Punde

DC Moyo :Wahudumu wa Afya Watakao Wanyanyasa Wazee Iringa Kukiona cha Mtema kuni.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akisisitiza jambo kwa wahudumu wa afya alipokuwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara ambapo ameamua kufanya ziara kijiji kwa kijiji kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo

Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo  wakati akisisitiza jambo kwa wahudumu wa afya alipokuwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara ambapo ameamua kufanya ziara kijiji kwa kijiji kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo

Na Fredy Mgunda,Iringa.

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amewaonya wahudumu wa afya wanaokiuka agizo la serikali linalowataka kutoa kipaumbele kwa wazee kutoa huduma za kiafya na kwamba tabia hiyo haivumiliki na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.


Kauli hiyo imekuja mara baada ya kupokea kero kwenye mikutano ya hadhara katika tarafa ya Kiponzero na Mlolo ambapo baadhi ya wazee wamemlalamikia mkuu huyo wa wilaya kunyanyaswa na wahudumu wa afya wa tarafa hizo.


Wakizungumza kwenye mikutano ya hadhara wazee hao walisema kuwa serikali imewajali kwa kuwapatia kadi za matibabu kwa wazee kwa lengo la kuwawezesha kupata huduma za kiafya bure lakini hali inakuwa tofauti pale wanapokwenye kupata huduma hiyo kwenye vituo vya afya,zahanati,hospitali za wilaya hadi hospitali ya Rufaa ya mkoani Iringa.


Wazee hao walisema kuwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakienda kutaka kupata huduma ya afya lakini wamekuwa hawapati huduma inayostahili kama ambavyo serikali imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa wazee wanapaswa kupewa kipaumbele katika huduma za kiafya.


Walimuomba mkuu wa wilaya ya Iringa kuhakikisha kuwa anapeleka kilio chao kwa serikali kuu ili nao waweze kuhudumiwa vizuri kama wananchi wengine wenye kipato kikubwa kwa kuwa wamelitumikia taifa hili kwa miaka yao yote ya maisha.


Aidha wazee hao waliongeza kuwa licha ya kuwa na kadi hizo bado kumekuwa na tatizo la kuzipata dawa ambazo wanakuwa wanaziitaji wakati huo kulingana na magonjwa ambayo wanakabiliana nayo badala yake wamekuwa wakielekezwa kwenda kununua dawa nje ya vituo vya afya.


Akijibia kero hizo za wazee mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa wazee wote wa wilaya ya Iringa ambao wanaumri wa kuanzia miaka 60 wanatakiwa kupewa kadi za matibabu za wazee kwa kuwa hiyo ni haki yao kwa muji wa sera za serikali ya awamu ya sita.


Alisema kuwa wahudumu wa afya wilaya ya Iringa wanatakiwa kuacha mara moja tabia ya kuwatolea lugha chafu wazee wanapokwenda kupata huduma za kiafya bara yake wanatakiwa kuwahudumia kama wanavyowahudumia wateja wengine wanaokwenda kupata huduma hiyo.


Moyo alisema kuwa akisikia wahudumu wa sekta ya afya wanatoa lugha hizo chafu watachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa lengo la kukomesha tatizo hilo ambalo linaonekama kuwa sugu katika wilaya hiyo.


“Kila zama na kitabu chake mimi sipo tayari kuona wazee hawa wakinyanyaswa bila sababu yoyote ile ya msingi wanapokwenda kupata huduma za kiafya kwa kuwa serikali imeamua kuwadumumia kutokana na mchango wao katika taifa hili hadi hapa lilipofika” alisema Moyo.


Moyo amewaomba wananchi na wazee wote wa wilaya ya Iringa kutoa taarifa kwake endapo watatolewa au hawatahumiwa vizuri na watumishi wa sekta ya afya katika wilaya hiyo ili kuondoa kero hiyo na kuboresha huduma kwa wateja ambao wanakuwa wanaenda kupata huduma za afya.


Moyo alimazia kwa kusema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuboresha sekta ya afya kwa wananchi wa wilaya ya Iringa na Tanzania kwa ujumla hivyo haitaji tena kuona watumishi wa sekta hiyo wakikwamisha juhudi za serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.