Habari za Punde

Dkt. Abbasi Aanika mafanikio ya Serikali kwenye michezo kwenye Tamasha la wanawake la Tanzanite

 
Na. John Mapepele, Dsm

Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa mchango mkubwa kwenye tasnia ya michezo hususan michezo ya wanawake katika hiki kifupi ikiwa madarakani kwa kuipa kipaombele michezo hiyo.

 Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 katika siku ya kwanza kati ya siku tatu za Tamasha la Michezo ya Wanawake la Tanzanite lililoratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambapo amesema lengo la tamasha hili ni kutoa hamasa kwa wanamichezo wanawake kushiriki na kufanya vizuri kwenye michezo.

Akifafanua baadhi ya michango mikubwa iliyotolewa na Serikali katika kipindi hiki kwenye tasnia ya michezo amesema ni pamoja na kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 9.5 kwa ajili ya kujenga  viwanja vya  wazi vya michezo na kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuzisaidia timu zote za taifa ikiwa ni pamoja na za wanawake.

Amesema Serikali inakusudia kujenga ukumbi wa kisasa kwa ajili ya kusaidia kuweka michezo mbalimbali kwenye ukumbi huo ambapo amesema  michoro ya ukumbi huo ipo mbioni kukamilika na ikikamilika itapelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.

Pia amesema katika kuboresha miundombinu ya michezo Serikali imesamehe kodi ya nyasi bandia za viwanja vya michezo na kutaka asilimia tano ya mapato ya kwenye michezo ya kubahatisha  kwenda katika mfuko wa kuendeleza michezo hapa nchini.

"Serikali ya awamu ya Sita ya mama Samia Suluhu Hassan, imewakumbuka sana wanawake ndio sababu tamasha hili ni mahususi kwa ajili yenu. Tukiamini baada ya hapo tutapata mageuzi na maboresho mengi," aliongeza Dkt. Hassan.

 

Pia amesema Serikali inajenga shule za michezo kila mkoa zitakazokuwa zikifundisha michezo pamoja elimu ya kawaida ambapo amesisitiza kuwa michezo ni sayansi ambayo inatakiwa kufundishwa.

 

 

 

Wakati huo huo Dkt. Abbas amesema viongozi wanatakiwa kuendesha vyama au Shirikisho za michezo kwa kwa kuzingatia kanuni na katiba walizojiwekea kwenye michezo mbalimbali.

 

Amesema baadhi vyama vya michezo havipati wadhamini wa michezo yao kwa kuwa hawajui namna ya kutangaza mafanikio na mikakati yao ambapo amesisitiza kuwa kupitia kongamano hili watapata ufumbuzi.

 

Kongamano hilo limesheheni mada mbalimbali ikiwemo hali ya ushiriki wa wanawake katika michezo, taaluma na maadili ya wanawake katika kushiriki michezo na umuhimu wa vyombo vya habari, udhamini katika ukuaji wa soko la michezo ya wanawake nchini.

 

Pia baada ya kongamano baadhi ya michezo ikiwemo mpira wa kikapu kwa walemavu kwa timu ya Dar City na Tembo Warriors, mchezo wa kunyanyua vitu vizito, kukuna nazi, karate kutoka chama cha TASHOKA na rede ilichezwa.

 

Tamasha la Michezo kwa Wanawake Tanzanite limeanza leo katika uwanja wa Mkapa na Uhuru linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe, Samia Suluhu Hassani Septemba 18, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.