Habari za Punde

Uwekaji Jiwe la Msingi Ujenzi Kiwanda Cha Maji Chamanangwe Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka jiwe la Msingi mradi wa kiwanda cha maji Amos Industries Limited Kilichopo Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akihutubia  wananchi waliohudhuria katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa kiwanda Cha Maji cha Amos kuwa serikali ya Dk. Hussein Mwinyi itatekeleza kwa vitendo yale yote yalioahidiwa kwa wananchi.
Wananchi mbali mbali kutoka kisiwani Pemba wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi alioitoa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa Kiwanda cha Maji cha Amos Industries Limited Chamanangwe Kisiwani Pemba.
Wananchi mbali mbali kutoka kisiwani Pemba wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi alioitoa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa Kiwanda cha Maji cha Amos Industries Limited Chamanangwe Kisiwani Pemba.
Na.Kassim Abdi.OMPR.

Serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaendelea kutoa msukumo maalum katika kuimarisha miradi ya uwekezaji ili kuwasaidia wawekezaji wazawa na wageni kuendeleza miradi hiyo na kufurahia matunda yanayotokana na uwekezaji huo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa kiwanda cha maji cha kampuni ya AMOS INDUSTRIES LIMITED kilichopo chamanangwe mkoa wa kaskazini pemba.

Mhe. Hemed alieleza kuwa, katika kufanikisha uwekezaji wenye tija Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais dk.mwinyi imefanya mabadiliko ya sheria nbari 14 ya mwaka 2018 ya kukuza na kumlinda mwekezaji Zanzibar yaliolenga kufungua fursa ya uwekezaji mkakati kwa upande wa kisiwa cha Pemba.

Alifafanua kwamba, mabadiliko hayo yametoa fursa kwa muwekezaji anaetaka kuekeza kisiwani Pemba kuwa na mtaji wa Dola za Kimarekani Millioni Kumi (10) tofauti na kiwango cha awali kilichokuwepo kwa kumtaka muwekezaji kuwa na kiwango cha Dola Millioni Hamsini (50).

Alisema miongoni mwa hatua nyengine zilizochukuliwa na serikali katika kukuza uwekezaji Nchini ni kukabidhi maeneo tengefu ya aridhi, mashamba ya mipira na visiwa vidogo vidogo kwa Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar ZIPA kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa aridhi na kuongeza wigo wa uwekezaji Nchini.

Mhe. Hemed alisema katika kipindi cha mwaka mmoja kwa serikali ya awamu ya nane tayari jumla ya miradi Tisini na saba Themanini na saba, Laki Sita ishirini na mbili elfu Mia moja na sabiini (787,622,170) na nane ishasajiliwa na ipo katika hatua za utekelezaji.

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais alieleza katika kuhakikisha mageuzi ya maendeleo ya viwanda Zanzibar, serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeshakamilisha utayarishaji wa uchambuzi yakinifu kwa eneo la Micheweni Pemba ambalo litakuwa chachu kwa uwekezaji na upatikanaji wa ajira kwa wananchi

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais kazi uchumi na uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga alisema azma ya serikali ya awamu ya nane imelenga kufungua milango zaidi ya uwekezaji ambapo jitihada mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo kufanywa kwa mabadiliko ya sera na sheria.

Mhe. Mudrik alileza kuwa kutokana na mazingira bora ya uwekezaji yaliofanyiwa marekebisho wawekezaji wamejenga imani kubwa kwa serikali juu ya usalama wa mitaji yao wanayoekeza na kueleza kwamba baadhi ya wawekezaji wameanza kurudi kuekeza Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali Sharif alisema katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya fedha za kitanzania Trilioni Moja nukta 8 zimetumika katika uwekezaji na jumla ya ajira Elfu Saba (7,000)  zinatarajiwa kupatikana kwa wananchi.

Alisema katika kipindi hiki cha Mwaka mmoja wa Uongozi wa Dk.Hussein Ali Mwinyi madarakani ongezeko la miradi limefikia Mia tatu ishirini na tatu 323 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Nae Mkurugenzi  wa AMOS INDUSTRIES LIMITED Husamudin Ali alieleza kampuni hiyo ya kizalendo imeamua kuunga mkono jitihada za serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuekeza jumla ya shillingi Billioni Moja nukta nane mpaka utakapokamilika ujenzi wa kiwanda hicho.

Alieleza kuwa, kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha Maji lita Elfu Tano (5000) ambapo uwepo wa kiwanda hicho unatarajia kuzalisha ajira kati ya 30 hadi 50 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 60 nje ya kiwanda ikijumuisha kupatikana kwa soko la matunda ya wakulima kwa ajili ya kutengenezea Juisi.

Pamoja na mambo mengine Bw. Husamudini Ali aliziomba serikali zote mbili kulipatia ufumbuzi tatizo la kuzuwiliwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kwenda Tanzania bara kwa ajili ya kutanua wigo mpana wa soko la bidhaa za Zanzibar ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kuelekea kipindi hichi cha mwaka mmoja cha Rais Dk. Mwinyi madarakani jumla ya miradi Kumi na mbili (12) imezinduliwa Unguja na Pemba ambayo inatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi, kukuza uchumi pamoja na kuongeza mapato serikalini kupitia ukusanyaji wa kodi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.