Habari za Punde

Tanroads Yaahidi Kuboresha Miundombinu ili Kukuza Uchumi Kibiashara Mkoani Tanga.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) wamesema watahakikisha wanaendelea kuimarisha mtandao wao wa barabara ili kuwezesha Mkoa wa Tanga kusafirisha mazao ya biashara katika kuendeleza kuimarisha kwa kukuza uchumi mkoani humo na Taifa.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS Logatus Mativila, kabla ya kumkaribisha mkuu wa Wilaya ya Tanga kufunga mkutano wa Baraza hilo uliofanyika kwa siku mbili mkoani humo.

Mativila amesema sambamba na hilo, katika mkutano huo wajumbe wa baraza hilo wameazimia mambo matano ambayo majibu yake yatapelekwa mwakani katika mkutano mwengine utakaofanyika mkoani Mara mwezi Machi.

"Muheshimiwa mkuu wa   kama ulivyosema wakati wa ufunguzi wa mkutano huu kwamba Mkoa wako unazalisha ni miongoni mwa Mikoa ambayo unazalisha chakula na biashara, pia ni moja ya vyanzo vya malighafi mbalimbali vya madini ya chokaa na saruji" alisema.

"Nipende kukuhakikishia kuwa, sisi tutaendelea kuhakikisha tunainarisha mtandao wetu wa barabara ili kuwezesha malighafi na mazao yaliyozalishwa maeneo mbalimbali katika Mkoa wako yaweze kusafirishwa na kufika kwenye maeneo ya masoko kwa haraka na uhakika, hapa tukimaanisha barabara zetu ziwe bora kusafirisha bidhaa hizo" alisisitiza.

Aidha amebainisha maazimio mengine ni kuwa TANROADS kupitia Mameneja wake mikoani kuandaa mpango wa kudumu wa ujenzi au matengenezo ya barabara na madaraja katika sehemu korofi ili barabara hizi ziweze kupitika wakati wote wa mwaka.

Mativila amesema azimio jingine ni kwamba TANROADS makao makuu na Mikoa waandae utaratibu wa kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Uviko 19 na uhamasishaji wa chanjo kwa watumishi wote kwa kuwatumia wataalamu wa afya katika maeneo yao.

"Pia imeazimiwa kuwa TANROADS iandae mafunzo kwa ajili ya kujenga uelewa kwa wafanyakazi juu ya mwongozo wa kusimamia vihatarishi na kuorodhesha vihatarishi baada ya rasimu kukamilika na taarifa ya utekelezaji itawasilishwa katika mkutano ujao wa mwakani" alifafanua Mativila.

Amesema TANROADS iandae mikataba ambayo ina vigezo au matakwa ya ziada itakayowabana Makandarasi na Wahandisi washauri ili waweze kuwajibika katika kazi walizokamilisha na azimio ni pamoja na kuandaa mafunzo kwa watu hao juu mwongozo kuhusu udhibiti wa ubora wa kazi za ujenzi ikiwa ni pamoja na mwongozo mpya wa uchanganyaji wa lami.

Kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima, mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa alisisitiza kuwa Ofisi zote za Mikoa nchini zitaendelea kutoa ushirikiano kwa TANROADS ili kuhakikisha zinafanya kazi zao bila kero za aina yoyote na kusisitiza ushirikiano baina yao.

"Na niendelee kutoa rai, pahala popote ambapo tutaona patakua pana shida, ni vema wa sisi tukawa wepesi wa kwenda kushiriki na wenzetu kwenye maeneo hayo, mwisho wa siku kazi hizi tunazozifanya ni za wote, inawezekana wewe ukaona ni changamoto lakini ukifika kwa kiongozi wako eneo hilo ikawa si changamoto tena, niendelee kurejea, tuone umuhimu wa kuwatumia viongozi wetu katika maeneo yetu tuliyopo" alisema.

Hata hivyo amewakumbusha suala zima la maadili kazini na kusema "katika ajenda na mada zenu mlizojadili suala kubwa lilikuwa ni maadili, tukiangalia kwa upande wa watumishi wa Umma hususani nyie ambao mnahusika na ujenzi wa hii miundombinu, mara nyingi kuna maeneo mengine serikali imekuwa ikitupiwa mikono na kupigiwa kelele" aliongeza.

Vilevile Mgandilwa amebainisha kwamba sababu ya msingi serikali kulaumiwa ni kutokana na miradi inatekelezwa na baada ya miezi mchache inaanza kuonyesha dosari za wazi na mara nyingi inasababishwa na watejelezaji kwenye mgongano wa kimaslahi ambapo wakati mwingine wanatoa kazi kwa Makandarasi ambao Wana urafiki nao au wanachokipata Makandarasi kinarudi kwao.

"Naomba kuwakumbusha moja ya maazimio tuliyoazimia hapa, ni sisi wenyewe kujitaza na kuangalia ni jinsi gani tutaitekeleza hii miradi pasipokuwa na changamoto za namna hiyo, niwaombe, tungalie tunachokipata kisije kikaharibu maana nzima ya kazi tunazosimamia, maana yake tupo na serikali inatuangalia kwa kazi tunazozifanya" alisisitiza Mgandilwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.