Habari za Punde

TWCC Tabora Waborsha Mjengo Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Wanachama wa Chama Cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) Mkoa wa Tabora wakiyafanyia usafi majengo ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere yaliyoko katika eneo la soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa Tabora ikiwa ni sehemu ya maadhmisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na miaka 59 ya Jamhuri ya Muungnao wa Tanganyika na Zanzibar jana. Picha na Lucas Raphael

Na Lucas Raphael,Tabora.

CHAMA Cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) Mkoani Tabora wameadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na miaka 59 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupaka rangi majengo ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere yaliyoko Mjini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Tabora Amina Madereka alisema wameamua kuboresha majengo hayo kwa kufanya usafi na kupata rangi ili eneo hilo la kihistoria liendelee kuwa kumbukumbu nzuri kwa vizazi vijavyo.

Alibainisha kuwa eneo hilo lina historia kubwa kwani harakati za Baba wa Taifa za kutafuta uhuru zilianzia hapo ambapo vikao vya siri ikiwemo kura 3 za maamuzi magumu ya Wajumbe wa Chama cha TANU zilipigwa katika majengo hayo.

‘Tunataka historia ya eneo hili iendelee kuenziwa na vizazi vyote na hata wageni wanaokuja Tabora watembelee eneo hili ili kujifunza historia ya harakati za uhuru,  nchi yetu kupata uhuru Desemba 9 mwaka 1961’, alisema.

Madereka aliongeza kuwa katika wiki hii ya maadhimisho wanawake wafanyabiashara wa Mkoa huo watafanya maonesho ya bidhaa mbalimbali katika viwanja vya Nane Nane, Ipuli katika Manispaa hiyo.

Alifafanua lengo la maonesho hayo kuwa ni kuonesha jinsi wanawake wa Mkoa huo walivyo na mwamko mkubwa wa kufanya shughuli za kiuchumi katika miaka hii 60 ya uhuru ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Alisisitiza kuwa kabla ya uhuru wanawake wengi walikuwa hawawezi kufanya biashara au kushiriki shughuli za kiuchumi ikiwemo za kisiasa, lakini sasa wako huru kufanya shughuli zozote za kimaendeleo ikiwemo siasa.

Katika mwendelezo wa maadhimisho hayo, alisema Desemba 18, 2021 vikundi mbalimbali vya wanawake wajasiriamali wa Mkoa huo vitakutana kujadili maendeleo, fursa na changamoto zinazowakabili.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Chemchem katika manispaa Tabora Mbuguma Salehe alisema wanawake wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, huko nyuma wengi wao hawakuwa na ujasiri wa kufanya biashara kutokana na vitendo vya ukandamizaji ikiwemo kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Aliwapongeza kwa uamuzi wao wa kuyafanyia usafi na ukarabati majengo yote ya Taasisi hiyo ili yawe na mwonekano mzuri kwani yalikuwa yameanza kuchakaa na kupoteza hadhi yake.

Katibu wa TWCC wilaya ya Tabora Safia Kisecha aliwataka wanawake wote wa Mkoa huo kujiunga na Chama hicho ili kunufaika na fursa za kibiashara, elimu na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali ikiwemo serikali kupitia halmashauri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.