Habari za Punde

Utambuzi wa Mifugo kwa Hereni za Kieletroniki Kudhibiti Mifugo Holela Mipakani.

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora (wa kwanza kulia), akizungumza na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiongozwa na Dkt. Audifas Sarimbo kutoka Idara ya Huduma za Mifugo, wakati walipofika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kutambulisha mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki kabla ya kuonana na maafisa mifugo wa mkoa na wilaya pamoja na wafugaji kabla ya kuanza rasmi zoezi la uwekaji hereni hizo, zoezi ambalo linafanyika nchi nzima.
Dkt. Uledi Kimbavala kutoka Kampuni ya S & J inayozalisha hereni za kieletroniki hapa nchini akifafanua na kuonesha kwa maafisa mifugo (hawapo pichani) wa Mkoa wa Kagera na wilaya zake namna hereni za kieletroniki zinavyokaa katika sikio la mfugo pamoja namba zake huku akiwaeleza hereni hizo hazitoki kirahisi kwenye sikio na hudumu kwa muda mrefu. 
(Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema zoezi ambalo imezindua la uhamishaji na mafunzo kuhusu uvalishaji wa hereni za kieletroniki kwa mifugo, litasaidia kupunguza migogoro na wizi wa mifugo yakiwemo maeneo ya mipakani ya Tanzania na nchi zingine kwa kulinda maeneo ya malisho.

Akizungumza wakati wa zoezi la uhamishaji na mafunzo hayo kwa maafisa wa mifugo Mkoani Kagera kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya zake, Dkt. Audifas Sarimbo kutoka Idara ya Huduma za Mifugo, amesema zoezi hilo litasaidia mikoa iliyopo mipakani kudhibiti mifugo kutoka nchi za jirani kuingia nchini na kusababisha wingi wa mifugo inayoharibu mazingira kutokana na uwepo wa mifugo mingi inayoingia bila utaratibu tofauti na uhitaji wa eneo husika.

 

Dkt. Sarimbo amefafanua kuwa lengo la kuweka hereni za kieletroniki kwa mifugo ni mfugaji kutambua mifugo yake na serikali iweze kujua mifugo iliyopo na kupunguza wizi na migongano ya mifugo yakiwemo maeneo ya mipakani ambapo kuna uingiliano wa mifugo pamoja na kudhibiti mifugo dhidi ya magonjwa kwa kufuatilia taarifa za mifugo hiyo.

 

Ameongeza kuwa kwa sasa katika ngazi za kimataifa wafanyabiashara wanataka kufuata mifugo ya aina fulani ambapo utambuzi wa mifugo umewekewa alama kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji, mfugo alipo pamoja na jina la mmiliki wa mfugo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Ziwa Victoria Bw. Charles Bwanakunu amesema zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo lina faida nyingi zikiwemo za wafugaji kuweza kupata mikopo kupitia benki mbalimbali pamoja na kuzuia wizi wa mifugo.

 

Aidha, amewahamasisha wafugaji kote nchini kushiriki vyema katika zoezi hilo na kuachana na kuweka alama kwa njia ya moto hali ambayo imekuwa ikisababisha mifugo kukosa soko katika baadhi ya nchi kwa kuwa ngozi za mifugo zinakuwa zimeharibiwa kwa njia ya moto.

 

Nao baadhi ya maafisa wa mifugo waliohudhuria zoezi la uhamishaji na mafunzo ya uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo wamesema mfumo wa kutambua na kusajili mifugo utarahisisha kufuatilia utaratibu wa mifugo kuingia nchini pamoja na kufuatilia na kudhibiti magonjwa pamoja na wizi wa mifugo.

 

Pia, wamewashauri wafugaji kuhakikisha wanashiriki vyema katika zoezi hilo ili mifugo yao itambuliwe rasmi na kuwa rahisi kwa serikali kupanga mipango ya upatikanji wa huduma mbalimbali za mifugo pamoja na kuondokana na mfumo wa kuweka alama kwenye ngozi kwa njia ya moto ambayo imekuwa ikiharibu ngozi ya mifugo.

 

Zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa hereni za kieletroniki ambalo linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2011 linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya Shilingi 1,750/= kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000/= kwa mbuzi na kondoo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.