Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema dhamira ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la uwekezaji linaanza kufikiwa kwa kuwepo viwanda viwili vikubwa ndani ya mwaka mmoja wa Uongozi wake.
Alieleza kuwa amefarajika kuona kumejitokeza wawekezaji wa ndani kuekeza Kisiwani humo na wananchi kuonesha utayari wao kwa kushirikiana na wawekezaji hao ili kuona wanapata maendeleo katika maeneo yao.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo huko katika kijiji cha Kinyikani
Mchangamdogo, Wilaya ya Wete, wakati akihutubia wananchi mara baada ya kuweka
jiwe la msingi la kiwanda cha maji safi
cha Watercom(T) LTD, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 58 ya
Mapinduzi Zanzibar.
Aliwataka wananchi wa maeneo hayo yaliojengwa kiwanda hicho kuendelea
kutowa mashirikiano kwa Wawekezaji wakati Viwanda hivyo vikianza uzalishaji
kwani kufanya hivyo kutaendelea kumpa moyo na kuona kuwa amekuja kuwekeza
sehemu sahihi.
“Ni dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuona kuwa kisiwa cha
Pemba kimekuwa eneo maalumu la uwekezaji na imepiga hatuwa katika maendeleo ya viwanda
na kiuchumi kwa kuweka mikakati maalumu ambayo kila muwekezaji itamvutia na
kuwa na hamu ya kuekeza katika kisiwa hichi,”alisema.
Alifahamisha kuwa Serikali
pamoja na kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji imeweka vivutio
maalumu ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji .
Rais Dk. Mwinyi aliwatowa hofu Wawekezaji kwamba Pemba iko salama na eneo zuri na linawavutia wawekezaji na anawahamasisha watu wenye nia ya uwekezaji
kuelewa kwamba Pemba kuna fursa ya uwekezaji ambazo hazijafanyiwa kazi hususan
katika uchumi wa Bahari.
Alisema kuwa uchumi wa bahari ndio muelekeo na Sera ya Serikali ya
awamu ya nane, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi
Zanzibar ni Uchumi wa Buluu kwa
maendeleo endelevu.
“Nawakaribisha wawekezaji wote kuekeza katika eneo hili ambalo
linajumuisha miradi inayohusiana na utalii, uvuvi na mazao mengine ya baharini
kama vile Mwani , bandari na shuhuli za mafuta na gesi asilia,”alieleza.
Alifahamisha kuwa Serikali imekwisha andaa na kuongeza jitihada za
kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuona namna bora za kuwaondolea urasimu
na kuhakisha wanashuhulikiwa kwa haraka katika kuhakikisha wanakamilisha
taratibu za uwekezaji kwamuda mfupi
sana.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeiimarisha Mamlaka ya ZIPA
kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha kutowa huduma (onestop center) kwa masuala
yote muhimu yanayohitajika kwa muwekezaji ili kumuondolea usumbufu.
Dk. Mwinyi alieleza hatuwa hiyo itamuwezesha Muwekezaji aliekwisha
kamilisha masharti kupata kibali cha uwekezaji sio zaidi ya siku tatu tu.
Alifahamisha kusikia kwamba kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji
kitachangia ajira zaidi ya 550 zitakazotokana na mnyororo wa thamani katika
uzalishaji wa maji hatua ambayo itaendana na dhamira ya kutoa ajira laki tatu.
“Ni matumaini ya Serikali kuwa
tunaweza kulifikia lengo hilo kwa
kutokana na mipango mizuri tulioiandaa
na ile tulioanza kuitekeleza ni wazi fursa hizo zitatowa mchango pia katika
kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuchangia sana kunyanyuwa uchumi wa
taifa kwa ujumla,”alieleza.
Aliwataka wananchi kuelewa kwamba sekta ya viwanda ni chachu ya
mafanikio kwa maendeleo ya kiuchumi katika nchi mbali mbali duniani, kwani nchi
nyingi zilizoendelea na zile zinazoendelea kwa kasi zimekuwa zikifanya jitihada
mbali mbali katika kuhakisha zinawekeza kwenye sekta ya viwanda na hivyo
Serikali imeamuwa kuweka maeneo maalumu ya viwanda yakiwemo maeneo ya Dunga na
Nungwi kwa Unguja na Chamanangwe kwa upande wa Pemba.
Alisema lengo la kuwepo maeneo hayo ni kuimarisha sekta ya viwanda
ambayo itafunguwa fursa mbali mbali ikiwemo kupatikana ajira kwa wananchi ,
kuchangia pato la Taifa kupitia kodi na
tozo mbali mbali , kupunguza utegemezi
wa bidhaa kutoka nje na kutowa soko zuri la bidhaa za kilimo , uvuvi na
ufugaji.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na
jitihada za kuleta maendeleo ya Viwanda nchini, ikiwemo kujenga kiwanda cha
Mwani katika eneo la Chamanangwe ambapo tayari kupitia mfuko wa Uviko 19
imetenga jumla ya fedha TZS Bilioni 2.5 ambazo zitapatiwa mkopo Kampuni ya
mwani Zanzibar ili kuhakikisha ujenzi wa kiwanda hicho inaanza na kukamilika
ndani ya mwaka huu 2022.
Alieleza mara kiwanda hicho kitakapo kamilika na kuanza kazi kitatowa
ufumbuzi wa changamoto wa bei ya mwani kuongeza thamani ya zao hilo na bidhaa zake
na kila mwenye nia ya uwekezaji Serikali atawapatiwa kila aina ya msaada anaohitaji ili kuhakikisha mazingira ya
uwekezaji yanaimarika Zanzibar na mchango wa sekta ya Viwanda unaongezeka.
Aliwataka vijana wa kisasa kutafsiri
Mapinduzi ya mwaka 1964, kwa vitendo kwa kuchangamkia fursa za kiuchumi
na kuleta maendeleo ya nchi yao.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliahidi kutekeleza ombi la wananchi
wa eneo hilo la kutiliwa lami barabara yao inatoka Mzambauni kupitia Kinyikani
hadi Mchangamdogo.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said
Shaaban, alisema uwepo wa viwanda vya vinywaji vitakuwa mkombozi mkubwa wa
kisiwa cha Pemba na wananchi wake kwa kupata ajira.
“Maji ni muhimu sana mwekezaji vizuri kupeleka maji hayo nje ya
Tanzania, kwa lengo la kuyatangaza maji ya Pemba katika baadhi ya nchi ikiwemo
Kenya,”alisema.
Aidha, alimshukuru mwekezaji huyo mzalendo kwa jihudi zake za kuekeza
ndani ya kisiwa cha Pemba, kupitia vinywaji mbali mbali nchini, huku
akimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwamba ndani ya uongozi wake tayari viwanda viwili
vimeshajengwa ndani ya kisiwa hicho.
Aidha, alisema Wizara ya Biashara bado inaendelea kuwa na imani na
uongozi wake wa awamu ya nane, katika mikakati ya kukitangaza kisiwa cha Pemba
kuwa ni eneo la uwekezaji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema
kumalizika kwa miradi hiyo itatoa faida kubwa kwa vijana wa Kisiwa cha Pemba,
hususan wazawa na wataalamu kunufaika na ajira ya moja kwa moja na ile isiyo ya
moja kwa moja.
Akitoa salamu za wananchi wa Jimbo la Kojani Mbunge wa Jimbo la
Kojani, ambaye pia, ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira, Hamad Hassan Chande alimshukuru mwenkezaji huyo kwa kuekeza kiwanda
chake katika Jimbo la Kojani, kwani asilimia 75 ya ajira wanufaika wa kwanza ni
wananchi wa Jimbo hilo.
Aidha, aliwataka wananchi kutambua kuwa tayari mwekezaji mwengine
kutoka kampuni ya Alhasab yupo njiani kuekeza katika meneo hayo, kujenga
kiwanda cha Juisi kitakachotoa fursa kwa wananchi kuuza bidhaa zao moja kwa
moja katika kiwanda hicho zikiwemo embe.
Mwakilishi wa Jimbo la Kojani Hassan Hamad Omar, alisema wananchi wa
Jimbo la Kojani na Pemba nzima, bado wanaendelea kuwa na imani na Serikali
inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi, kutokana na mikakati mbali mbali aliyoiweka
ikiwemo katika eneo la uwekezaji na uchumi wa buluu.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na
Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dk. Islam Seif Salim alisema mradi huo wa
kiwanda cha maji ulianza Oktoba 2 mwaka 2021, kufuatia maelekezo yake na Mamlaka
ya ZIPA kuhamasika kuhimiza wawekezaji na kuondosha urasimu katika eneo la
kimkakati la kisiwa cha Pemba.
Alifahamisha kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu TZS Bilioni
1.2, kiwanda kikijumuisha maeneo mbali mbali pamoja na kisima cha kuzalisha
lita 30 elfu za maji kwa saa, huku kikitarajiwa kuanza kuzalisha maji mnamo
mwezi Machi, 2022.
Katibu huyo alisema uwezo wa kiwanda ni kuzalisha maji lita 72 elfu
kwa masaa 12 au lita laki moja na 44 kwa
siku, huku bidhaa zitakazozalishwa ni maji, soda, askirim, na kuuzwa katika
masoko mbali mbali ya Tanzania bara na nje ya Tanzania.
Alisema sekta ya Viwanda imekua ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa
nchi nyingi duniani, Zanzibar uwepo wa vianda vya kati vinaweza kutoa ajira kwa
wasiopungua 230 na viwanda vikubwa vimeweza kutoa ajira 10417 2019 hadi 11601
2020.
Naye mwakilishi kutoka kampuni ya Watercom (T) Aboubakar Ali Faraji,
alisema uwepo wakiwanda hicho ni kuunga mkono Uchumi wa buluu na juhudi katika
kukipa kisiwa cha Pemba maendeleo.
Alisema kukamilika kwake kitatoa ajira za moja kwa moja 50 na zisizo
za moja kwa moja 500, na kuzalisha maji 72000 kwa saa.
Katika hafla hiyo burudani mbali mbali zilitumbuiza ikiwa ni pamoja na
burudani ya vijana kutoka Micheweni.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment