Habari za Punde

Wakandarasi watakiwa kuanza kazi miradi ya maendeleo

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakati wa kukagua Miradi ya Maendeleo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiwapa maelekezo kwa wakandarasi wa hospitali ya Wilaya kaskazini B unaojengwa eneo la Pangatupu wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo

Muonekano wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A ulipofikia wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipotembelea kukagua miradi hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Khamis Juma akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman juu ya Ukarabati wa skuli ya Uzini ambao utaanza mapema mwezi Februari mwaka huu


  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiwapa maelekezo kwa wakandarasi wa hospitali ya Wilaya Mwera Pongwe wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo

Na Abdulrahim Khamis , OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewaagiza  wakandarasi wanaosimamia Miradi mbali mbali ya maendeleo ambao hawajaanza kazi kuhakikisha wanaanza kazi hizo ndani ya wiki mbili.

Mhe. Hemed ameeleza hayo katika ziara ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo katika Mikoa ya Kaskazini  na Kusini Unguja.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed ameeleza kufurahishwa kwake  kwa kuona miradi mingi wakandarasi wameanza kazi katika maeneo yao, ambapo amezitaka Wizara na Taasisi husika kuhakikisha wanasimamia vyema miradi hiyo ili iweze kuleta tija kwa wananchi.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema hakuridhishwa na mradi wa Tangi la Maji  Bumbwini, ambapo amemuagiza waziri wa maji, nishati na madini kuhakikisha Wakandarasi wanapatikana na kuanza kazi mara moja ili kuondosha kero ya maji kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.

Akigusia kuhusu fedha za miradi hiyo Mhe. Hemed amesema Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya miradi hiyo ambapo kila mkandarasi atakabidhiwa fedha kwa mujibu wa taratibu na makubaliano ya Mikataba waliofunga na Wizara husika.

Katika miradi Hospital za wilaya pamoja na majengoya Skuli, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza  kufurahishwa na kazi inayofanywa na wakandarasi waliokabidhiwa kazi hizo, na kuwataka kuendelea na miradi hiyo, kwa mashirikiano ya Ofisi za  wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ambapo miradi hio inatekelezwa kwa wakati na viwango kwa mujibu wa makubaliano.

 Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza wakala wa majengo Zanzibar (ZBA) kuhakikisha wanasimamia majengo hayo kuwa ya viwango  bora na yenye kudumu kwa muda mrefu ili kunakisi fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

 Akigusia kuhusiana na Skuli zinazofanyiwa matengenezo Mhe. Hemed amesema serikali imeamua kuzifanyia matengenezo skuli hizo ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri bila ya kikwazo cha aina yoyote na kuutaka uongozi wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha ukarabati huo unasimamiwa ipasavyo kwa Maslahi ya wazanzibari.

Kuhusu suala la Umeme katika ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Kusini na Wilaya ya kati Mhe. Hemed ameagiza uongozi wa Wizara ya Afya Ustawi wa jamii,jinsia, wanawake na watoto kukaa pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuhakikisha umeme unafika katika maeneo hayo ili kurahisisha ujenzi wa miradi hio.

Sambamba na hayo Makamu wa Pilli wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa ujenzi wa miradi hio ili uleta ufanisi nzuri na kupata majengo yenye kudumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wao Wakuu wa Mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini unguja wamemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watatoa mashirikiano ya kutosha kwa wakandarasi hao na kuhakikisha wanatatua changamoto zote zitakazowakabili ili kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar ALI KHAMIS JUMA amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa fedha tayari zimeshaingizwa  za ujenzi na ukarabati wa madarasa ya skuli utaanza haraka iwezekanavyo ili kurahisisha upatikanaji wa elimu bora kwa wananchi wa Zanzibar unafanikiwa

Nae Mkurugenzi Mkuu wizara ya Afya Dr Abdalla Suleiman  ameeleza kuwa ujenzi wa hospital ya Pangatupu, kitogani na mwera Pongwe ni hospital za Wilaya ambapo zitakuwa za kisasa zenye uwezo wa Kutoa huduma mbali mbali ikiwemo huduma za mama na mtoto, upasuaji, kulaza wagonjwa wa maradhi tofauti zaidi ya Mia moja kwa wakati  pamoja na kutoa huduma nyengine

Nao wakandarasi wa miradi hiyo wamemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Miradi hiyo itakamilika kwa muda waliyokubaliana na kumuhakikishia kuwa majengo hayo yatakuwa na viwango vya hali ya juu, kwani hadi sasa hamna changamoto yoyote wanayokumbana nayo

Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed amekagua eneo linalotarajiwa kujengwa  Tangi ka Maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita Milioni moja lililopo Bumbwini, ujenzi wa Hospital za wilaya Pangatupu, kivunge, kitogani pamoja na Mwera Pongwe,na karabati wa skuli ya Uzini, ujenzi wa skuli ya Elimu Mjumuisho Jendele pamoja na Ujenzi wa skuli ya Maandalizi ya Unguja Ukuu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.