Habari za Punde

Vijana Wenye Ulemavu Pamoja na Yatima Wasisitizwa Kujiunga na Veta

Na Hamida Kamchalla, Tanga.

Vijana wenye ulemavu pamoja na wale ambao ni yatima wasiokuwa na msaada wowote walioko mitaani wamehimizwa kujiunga na Wakala wa Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) kupitia ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu yanayoleta kwa awamu ili kuweza kumudu maisha yao kwa kujiajiri au kuajiriwa na kuondokana na maisha tegemezi.

Mafunzo hayo yanatolewa kwa vijana wote nchini ambao wako mitaani bila kazi kwa lengo la kuwapa ujuzi wa aina mbalimbali kulingana na matakwa na mahitaji yao ili waweze kupata ajira au kujiajiri na kujikwamua kimaisha.

Mkuu wa VETA Mkoa wa Tanga Gideon Ole Lairumbe ametoa msisitizo huo juzi wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema VETA inatambua uwepo wa makundi hayo hivyo zinapotokea fursa hizo wajitokeze kuzitumia kwa manufaa yao ya baadae.

"Wito wangu kwa wakazi wa Tanga wajitokeze kuzitumia fursa hizi ambazo zinajitokeza, kitu kimoja kilichojitokeza kwenye usajili wa awamu zilizopita hawajajitokeza watu wenye mahitaji maalumu (walemavu) wa aina mbalimbali, kuna walemavu wa viungo, kusikia, wa ngozi na wa kuona, tunasisitiza wajitokeze kutumia fursa hii" alisema.

"Kwasababu tunawapokea na kuwaangalia kutokana na ulemavu wao na kuwapa mafunzo ya kinadharia na vitendo, vile vile tunawaomba watu ambao ni mayatima wasiokuwa na uwezo wa kujitegemea wala watu wa kuwasaidia wajitokeze, tutawafanyia tathmini na kuwapatia mafunzo hayo" alisisitiza Lairumbe.

Lairumbe amesema katika awamu ya pili ambayo usajili uliofanyika julai, 2021 walijitojeza vijana 2000 lakini walikuwa na nafasi 360 na walianza mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo kuanzia mwezi huo hadi disemba 2021 na sasa wapo katika Kampuni, Taasisi na Gereji mbalimbali kwa ajili ya kufanya majaribio hadi watakapohitimu rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Amebainisha kwamba katika awamu hizo kulijitokeza tatizo moja la wasichana kutokujitokeza kwa wingi kupata mafunzo wakati wanahitajika kutokana na umakini na uangalifu walionao zaidi kuliko vijana wa kiume pindi wawapo kazini.

"Kitu kimoja ambacho ni tatizo, hii niwaombe wananchi na jamii inayotuzunguuka, tuna tatizo la watoto wa kike kujitokeza, hili ni kubwa kwa Mkoa wa Tanga wasichana wengi hawataki kusoma ufundi, lakini nina uhakika kwamba walijitojeza wanakuwa rahisi kwao kuajiriwa au kujiajiri zaidi kwa sababu ya mtazamo wa jamii zetu" alisema.

"Watoto wa kike ni waangalifu katika ufundi ikilinganishwa na watoto wa kiume, kuna wakati makampuni mengi yanajitokeza kutafuta madereva wa kike wakiamini ni waangalifu kwenye gari ukilinganisha na madereva wa kiume, na hata wateja wakitaka watu wa ushonaji au ujenzi wanawaamini mafundi wa kike zaidi" aliongeza.

Hata hivyo ametoa wito kwamba, "vijana wa kike ambao hawajapata ajira wapo tu majumbani wajitokeze waje wasome haya mafunzo yanatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini hata wakitaka haya mafunzo yetu ya muda mrefu na mfupi, vijana hawa wako wachache sana hapa chuoni, hawajafikia hata asilimia 10, ni wachache mno" alisisitiza.

Kuelekea awamu ya tatu ya usajili Lairumbe amesema, "hii ni awamu ya pili, awamu ya kwanza ilikuwa mwaka juzi, tunategemea wakihitimu hawa, wafadhili wetu ambao ni serikali kwamaana ya Ofisi ya Waziri Mkuu itatupa mwongozo tena wa kuendelea kuchukua awamu ya tatu, lakini matumaini yetu kama chuo tutaendelea kuwapokea".

Sambamba na hayo Lairumbe amesema kwa upande wa chuo wanafundisha mafunzo ya nadharia na vitendo kwa muda mrefu mrefu ambayo wanaanza kutoa fomu kuanzia mwezi wa 9 hadi wa 11, mwezi wa 12 wanafanya usaili na mwezi wa kwanza wanaanza masomo na kwa mwaka 2021/22 wamesajili wanafunzi 350 ambao wameshaanza masomo yao.

Alisema, "mafunzo ya muda mfupi tunatathmini kila baada ya mwisho wa mwaka kwa maaana ya kwamba wanaingia kila mwezi na muda wowote, haya hayana muda maalumu na tunaanza kuyatoa kuanzia wiki 2 hadi miezi 6, ambayo ni udereva, kompyuta, saluni pamoja na upishi" alisema Lairumbe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.