Habari za Punde

Sheria Rafiki wa Uhuru wa Habari ni Msingi wa Demokrasia Nchini.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akisalimiana na Viongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) alipowasili katika viwanja vya Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhudi Zanzibar kwa ajili ya ufunguzi wa Mafunzo ya Habari kwa Wanasheria, ‘Training of Lawyers on Press Freedom, Freedom of Expression and Related Litigation’.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza wakati wa kuyafungua rasmi Mafunzo ya Habari kwa Wanasheria, yanayojulikana kwa ‘Training of Lawyers on Press Freedom, Freedom of Expression and Related Litigation’, yanayofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii, Maruhubi  Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Habari ya Sheria kwa Wanasheria yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia kazi Sheria mbali mbali zenye mapungufu, kwa lengo la kuimarisha uhuru wa habari na kujieleza, hatua ambayo ni muhimu katika kukuza demokrasia na utawala bora nchini.                                                                                                                                 

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika Hotuba yake, wakati akiyafungua rasmi Mafunzo ya Habari kwa Wanasheria, yanayojulikana kama ‘Training of Lawyers on Press Freedom, Freedom of Expression and Related Litigation’, huko Chuo cha Maendeleo ya Utalii, Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Amesema kuwa sheria rafiki ni sehemu ya mazingira wezeshi katika kulinda na kutetea uhuru wa habari na kujieleza, na kwamba pamoja na juhudi ziliopo, kinachodhihiri ni kuwa bado zipo changamoto katika ufanisi na hivyo kusababisha uhuru wa habari kuwepo mashakani.

Akitolea mfano hapa Zanzibar, Mheshimiwa Othman ametaja Sheria mbili kuu zinazohusu masuala ya habari; ambazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu, Na. 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 1997; na pia Sheria ya Tume ya Utangazaji ya mwaka 1997 pamoja na Marekebisho yake ya mwaka 2010; akisema kuwa hizo bado ni dhaifu katika kulinda uhuru wa habari visiwani hapa.

Amebainisha mapungufu katika Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 ambayo inazo changamoto kadhaa kwa uhuru wa vyombo na uandishi wa habari Zanzibar; na pia Sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar, Na. 7 ya mwaka 1997, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 1 ya mwaka 2010, ambazo kwa ujumla zinahitaji mapitio na marekebisho makubwa. 

Akieleza juhudi za kukabiliana na mazingira hayo, amesema tokea kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nane ya Uongozi wa Zanzibar na Awamu ya Sita kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marais- Dokta Hussein Ali Mwinyi, na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, mara kwa mara wamekuwa wakihimiza haja ya wananchi kupata haki yao ya msingi ya taarifa, sambamba na kuwaelekeza watendaji kushikirikiana na wanahabari katika majukumu yao.

Katika nasaha zake kwa washiriki, Mheshimiwa Othman pia ametoa rai ya kufanyika kwa mapitio ya kina ya Sheria inayohusiana na ‘Uchochezi’ (sedition) kutokana na ukweli kwamba inatoa fursa pana ya kutumika vibaya na baadhi ya vyombo vinavyosimamia sheria hapa Nchini.

“Hii ni moja ya sheria ambayo kwa jinsi ilivyo na mianya mingi ya kutumika vibaya, inaweza kukwaza sio tu uhuru wa habari pekee bali pia uhuru kwa ujumla wake”, ameeleza Mheshimiwa Othman.

Aidha Mheshimiwa Othman amelishauri Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuzichukulia changamoto hizo, kama waanzilishi wa mjadala mpana, na pia kuja na mapendekezo yatayosaidia kuiweka nchi katika ramani ya kisasa ya uhuru wa habari.

Mheshimiwa Othman amesisitiza umuhimu wa kuwepo mashirikiano baina ya Serikali, vyombo vya habari na wadau wote wa Sekta hii muhimu, ili kujenga jamii imara yenye uelewa.

“Lililo muhimu zaidi ni kwa kila upande kutekeleza wajibu wake, na inapobidi kukosoa, kufanyike kwa misingi ya ukweli na haki kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya, tukizingatia kwamba sote tunajenga nyumba moja imara, itakayoheshimu haki na uhuru wa habari na kujieleza”, amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman amewahamasisha washiriki kuyazingatia kwa umakini wa hali ya juu Mafunzo hayo ambayo yana umuhimu wa pekee pamoja na kuwahimiza kuyafanyia kazi, ili lengo la ufuatiliaji wa sheria za habari liweze kufanikiwa, kwani hayo ni dira ya kuongoza katika kurekebisha mapungufu yoyote katika Sheria hizo. 

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Kajubi Mukajanga amesema kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo siyo tu kubaini sheria ambazo zinarejesha-nyuma uhuru wa habari, bali pia kutoa ufafanuzi wa kina kwa sheria kandamizi dhidi ya sekta ya habari kwa azma pia ya kuhoji ili kuleta mabadiliko ya kweli, sambamba na kuimarisha uhuru wa habari hapa nchini.

Mafunzo hayo ya Siku Tatu, yaliyoandaliwa kwa mashirikiano ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Shirika la Maendeleo la Switzeraland (SDC), kupitia Jumuiya ya Kimataifa ya Kusaidia Vyombo vya Habari iliyopo Denmark (IMS), yamebeba maudhui kuhusu Sheria zinazosimamia haki ya kupata taarifa, uhuru wa habari, uhuru wa kujieleza na kwa namna gani wanasheria hapa Nchini wanaweza kuhoji mapungufu mbali mbali ya Sheria, kupitia vyombo vikuu vya kusimamia haki, ambavyo ni pamoja na Mahakama.

Washiriki wapatao 21 na Wakufunzi wa Mafunzo hayo, ambao ni pamoja na Mawakili, Wanahabari na Wanasheria kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wamejumuika na Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakiwemo Maafisa Wakuu wa Miradi, Bi Shifaa Said Hassan, Bi Saumu Mwalimu, Wajumbe wa Tume za Kurekebisha Sheria; na Wawakilishi kutoka Mashirika Wahisani wa Maendeleo.

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

28/03/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.